Na ABDUL DUNIA
SIKU moja baada ya Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, kusisitiza umuhimu wa usawa katika kalenda za soka duniani kote, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), imesema wazo hilo ni muhimu na litakuwa na manufaa makubwa katika soka hapa nchini.
Infantino alitoa maoni hayo katika Kongamano la FIFA kuhusu Uongozi lililofanyika jijini Doha, Qatar juzi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa soka akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA), Mtanzania Mhandisi Hersi Said.
Rais huyo alisema FIFA na wadau mbalimbali walijadiliana mambo mengi ikiwemo uhitaji wa kutafuta usawa sahihi katika kalenda ya klabu, kuhakikisha timu zinacheza idadi sahihi ya mechi na juu ya yote, mechi zenye maana.
“Kombe la Klabu Bingwa Dunia 2025 (lililofanyika Juni hadi Julai mwaka huu) lilionyesha ni kwa kiasi gani klabu kutoka maeneo yote duniani zinaweza kushiriki katika jukwaa kubwa na kuungana na mashabiki duniani bila ya kuathiri ratiba nyingine,” alisema Infantino.
Pia, Infantino alisema: “FIFA ina jukumu muhimu katika kusaidia soka ngazi ya klabu kukuwa duniani kote kwa kuwa wabunifu na kuunda matukio ambayo yatavuka mipaka na kuzipa klabu majukwaa wanayostahili,”.
Akizungumzia uhitaji wa kutafuta usawa sahihi katika kalenda ya klabu, Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda, amesema wazo hilo ni bora na anaamini litakuwa na manufaa makubwa katika soka ikiwemo la Tanzania.
“Wazo hilo ni bora, unapokuwa na kalenda iliyo sawa na sahihi maana yake itatoa fursa kubwa kwa wachezaji kucheza mechi zinazoedana na uwezo wao wa ufiti na kupunguza baadhi ya majeraha tofauti na mechi zinaporundikana.
Pia, itasaidia kufanya ratiba ya michuano fulani katika shirikisho moja kutoingiliana na ratiba nyingine, jambo ambalo litatoa nafasi kubwa ya ushindani na ufanisi katika kushiriki mashindano,” alisema.
Pia, Boimanda alisema kunapokuwa na usawa katika kalenda ya soka kiuhalisia viwango vya wachezaji upanda na hali ya ushindani huongezeka.




