AGADIR, Morocco
STAA wa timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo amesema anafurahia kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), msimu huu nchini Morocco.
Alisisitiza kuwa ana furaha tele kucheza michuano ya msimu huu baada ya kuzikosa fainali za msimu uliopita zilizofanyikia Ivory Coast kutokana na majeraha yaliyokuwa yakimkabili.
Akizungumza, staa huyo anayekipiga katika kikosi cha Manchester United, alisema hiyo ni fursa ya aina yake kuhakikisha anaisaidia timu ya Cameroon kufanya vizuri katika michuano ya AFCON 2025.
“Nina msisimko mkubwa kucheza michuano ya AFCON 2025, niliisubiri kwa muda mrefu na nina furaha kuwa mmoja wa wachezaji wa kuitumikia timu yangu ya taifa katika msimu huu,” alisema Mbeumo.
Mchezaji huyo wa zamani wa Brentford tayari alishacheza michuano ya Kombe la Dunia msimu uliopita iliyofanyikia Quatar akiwa na Cameroon.
“Hii ni sehemu ya kujivunia kwa Afrika kwani hata familia yangu inanifuatilia jinsi ninavyocheza katika michuano ya AFCON, ni heshima ya aina yake na ni kitu pekee katika maisha yangu.
“Kwangu sina presha kwani mipango niliyonayo ni kuisaidia timu kufanya vyema na kufika mbali zaidi katika michuano ya msimu huu ikiwemo kuweka historia,” alisema.
Katika michuano ya AFCON 2025, Cameroon imepangwa kundi F ikiwa na timu za Ivory Coast, Gabon na Msumbiji.
Staa huyo alishafunga mabao sita katika mechi 16 alizocheza Ligi Kuu ya England ndani ya Manchester United.
(BBC)




