Na MWANDSIHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali kama mkakati wa kudhibiti vifo vinavyotokana na ajali za barabarani pamoja na makosa ya usalama barabarani.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Simbachawene, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo ya kikazi.
Amesema kukamilika kwa mifumo hiyo ya kidigitali, ikiwemo matumizi ya taa za kuongozea magari (Traffic Lights) pamoja na uwekaji wa rada za kudhibiti mwendo kasi, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makosa ya barabarani, vifo vinavyotokana na ajali pamoja na gharama za huduma za afya zinazobebwa na Serikali baada ya ajali kutokea.
Akizungumzia suala la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, ikiwemo vitendo vya ubakaji, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali imechukua hatua madhubuti kudhibiti vitendo hivyo, ikiwemo kuondoa dhamana kwa watuhumiwa wa makosa hayo pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.
Vilevile, akizungumzia matukio ya uhalifu katika maeneo ya utalii, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuchukua juhudi za kuimarisha usalama katika maeneo hayo, ikiwemo kuwataka wamiliki wa hoteli kufunga kamera za usalama (CCTV) ili kusaidia kudhibiti vitendo vya kihalifu.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha utendaji wa pamoja wa taasisi za Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Jeshi la Polisi, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. George Simbachawene, ameonesha kuridhishwa na mchango pamoja na ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha utendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, ikiwemo Uhamiaji, NIDA na Polisi.




