Na ABDUL DUNIA
ALHAMISI hii hadi Januari 18, mwakani michuano ya 35 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), inatarajiwa kufanyika nchini Morocco.
Fainali hizo zinatarajiwa kufanyika katika majiji ya Rabat, Casablanca, Agadir, Fez na Marrakech.
Michuano hiyo inayoshirikisha timu 24, jumla ya makundi sita yamepangwa ambapo kila kundi limehusisha timu nne.
KUNDI A
Kundi hilo linaundwa na mwenyeji Morocco pamoja na timu za Mali, Zambia na Comoros.
Morocco imewahi kucheza fainali hizo mara 20, Zambia 19, Mali mara 14 na Comoros ikicheza mara mbili.
KUNDI B
Misri inaunda kundi hilo pamoja na timu za Afrika Kusini, Angola pamoja na Zimbabwe.
Misri imefuzu fainali hizo mara 27, Afrika Kusini mara 12, Angola mara 10 wakati Zimbabwe ikicheza mara sita.
KUNDI C NA UNDANI WAKE
Tanzania ‘Taifa Stars’ inaunda kundi hilo na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.
Katika kundi hilo, Taifa Stars ndiyo timu iliyofuzu fainali hizo mara chache (4), Tunisia mara 22, Nigeria mara 21 wakati Uganda ikitinga mara nane.
Wakati Taifa Stars ikifuzu fainali hizo mara nne, Tunisia imefuzu fainali hizo kwa mara ya 22, Nigeria mara 21 wakati Uganda maarufu kama ‘The Cranes’ ikitinga mara nane.
Katika kundi hilo, Taifa Stars ndiyo timu pekee ambayo haijawahi kupenya hatua ya mtoano wakati Nigeria ikiwa ni bingwa mara tatu mwaka 1980, 1994 na 2013, Tunisia mara moja mwaka 2004 huku Uganda ikiwahi kushika nafasi ya pili mwaka 1978.
Pamoja na kuzidiwa na namba dhidi ya wapinzani wake, lakini wadau wa soka wanaamini Taifa Stars chini ya Kocha Miguel Gamondi, ina kila sababu ya kufanya vyema mwaka huu kama itajipanga vyema.
Wakizungumza kwa nyakati tofati na gazeti hili, straika wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Abdallah Kibadeni, alisema hivi sasa ni wakati wa Stars kufanya vyema na kufikia katika hatua nzuri.
“Kutokana na viwango vya wachezaji wetu na tayari tumeshatambua tunakutana na kina nani, nina imani tutafanya vyema na kuliletea heshima taifa letu,” alisema.
Kibadeni ambaye pia amewahi kuinoa timu ya soka ya Ashanti United, alisema wachezaji wa kikosi cha Taifa Stars katika fainali hizo, wanapaswa kujituma kwa hali ya juu kuibeba timu hiyo.
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alisema: “Jambo kubwa ni maandalizi ya kutosha na wachezaji kujitoa kila kitu kinawezekana, kwa sababu tuna timu nzuri ambayo inaweza kutupatia matokeo mazuri,”.
Mogella alisema ana imani Stars ikiandaliwa mapema na wachezaji wakitambua kitu cha kufanya, watafanya vyema katika michuano ya AFCON na kuacha historia nchini Morocco.
GAMONDI AKINGIWA KIFUA
Wakongwe wamemkingia kifua kocha wa kikosi hicho, Gamondi kutokana na kile kinachodaiwa ameita wachezaji wengi wa nafasi ya ulinzi (mabeki) kuliko viungo na washambuliaji.
Wakati wakipa ni Yakoub Suleiman, Hussein Masalanga na Zuber Foba, mabeki ni Bakari Mwamnyeto, Shomari Kapombe, Lusajo Mwaikenda, Mohamed Hussein, Nickson Kibabage, Wilson Nangu, Pascal Msindo, Ibrahim Bacca, Haji Mnoga na Dickson Job.
Viungo wanaounda timu hiyo ni Morice Abraham, Feisal Salum, Yusuph Kagoma, Habib Idd, Kelvin Nashon, Novatus Dismas na Alphonce Mabula huku washambuliaji ni Mbwana Samatta, Simon Msuva, Kelvin John, Kibu Denis, Idd Nado, Abdul Sopu, Charles M’mombwa na Tarryn Allarakhia.
Mogella, alisema anaamini Gamondi ana mpango madhubuti ambao utamsaidia katika fainali hizo.
“Ni mpango mkakati wake, naamini kuna kitu anataka kuona, binafsi sioni tatizo katika hilo ninaamini mwalimu kuna kitu kakiona na ndiyo maana kafanya hilo chaguo,” alisema.
“Taifa Stars ya sasa ni bora na soka limebadilika, sasa mpira wa miguu ni sayansi zaidi, hivyo naamini kila kitu kitakuwa sawa,” aliongeza.
Mtemi Ramadhani ambaye pia aliwahi kukipiga Taifa Stars, alisema anaamini Gamondi ana mpango mzuri ambao utaiongoza timu hiyo kufanya vyema katika AFCON.
“Ninafikiri mwalimu anajua nini anakifanya, pengine anahitaji kuingia na mpango wa kujilinda zaidi katika mechi ngumu, lakini naamini kabisa kikosi kilichoitwa ni kizuri kwa mashindano,” alisema.
KUNDI D
Senegal inaunda kundi D na timu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Benin na Botswana.
DRC imefuzu fainali hizo mara 21, Simba wa Teranga (Senegal) mara 18, Benin mara tano wakati Botswana mara mbili.
KUNDI E
Algeria ipo kundi E na timu za Burkina Faso, Guinea ya Ikweta na Sudan.
Katika michuano hiyo, Algeria imewahi kufuzu mara 21, Burkina Faso mara 14, Sudan mara 10 na Guinea ya Iketa ikifuzu mara tano.
KUNDI F
Bingwa mtetezi Ivory Coast ipo kundi F na timu za Cameroon, Gabon na Msumbiji.
Ivory Coast imefuzu fainali hizo mara 26, Cameroon mara 22, Gabon mara tisa wakati Msumbiji ikifuzu michuano hiyo mara sita.
TANZANIA ILIVYOFUZU
Taifa Stars ilifuzu fainali hizo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Guinea katika mchezo wa mwisho wa kundi H, kuwania kufuzu AFCON uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Bao la mshambuliaji nyota, Simon Msuva katika dakika ya 61, limeipeleka Tanzania katika AFCON baada ya kufikisha pointi 10 na kukwea hadi nafasi ya pili katika kundi hilo.
Msuva aliiandikia Stars bao katika dakika ya 61, akiuweka mpira kimiani kwa kichwa baada ya kuunganisha pasi ya Mudathir Yahya.
Bao hilo liliibua shangwe la aina yake kutoka kwa wachezaji na mashabiki walioujaza uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000.
MCHANGANUO WA POINTI
Wakati Stars ikishika nafasi ya pili, Guinea imeshindwa kufuzu fainali hizo baada ya kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tisa huku Ethiopia ikiburuta mkia kwa alama nne wakati kinara Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikipata pointi 12.
Katika mchanganuo wa pointi hizo, Stars imeanza michuano hiyo kwa suluhu dhidi ya Ethiopia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kushinda mabao 2-1 ilipocheza na Guinea katika dimba la Charles Konan Banny, Ivory Coast.
Katika mchezo dhidi ya Guinea, mabao ya Tanzania yaliwekwa kimiani na Feisal Salum ‘Fei Toto’ pamoja na Mudathir Yahya.
Pia, miamba hiyo ilikubali kichapo cha baop 1-0 ugenini dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kabla ya kufungwa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano.
Pia, Taifa Stars ilifufua matumaini yake ya kufuzu AFCON baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia katika Uwanja wa Martry’s, DRC. Katika mechi hiyo, mabao ya Stars yalifungwa na Msuva pamoja na Fei Toto.
Na baadaye, kikosi hicho kilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Guinea na kutinga AFCON.
Hiyo ni mara ya nne kwa Taifa Stars kufuzu fainali za AFCON, ambapo awali Tanzania ilianza kucheza AFCON katika fainali za mwaka 1980 zilizofanyika Nigeria, kabla ya kufuzu mwaka 2019 zilizochezwa Misri na pia za mwaka 2023 zilizofanyika mapema mwaka jana nchini Ivory Coast.
TAKWIMU AFCON ZILIZOPITA
Katika fainali zote tatu zilizopita ambazo Stars ilishiriki, timu hiyo haijawahi kutinga hatua ya mtoano hata mara moja.
Katika michuano ya mwaka 1980 iliyofanyika Nigeria, Taifa Stars ilipangwa kundi A na timu za Nigeria, Misri na Ivory Coast.
Taifa Stars iliburuta mkia kwa pointi moja baada ya kutoka sare na Ivory Coast. Awali, ilifungwa mabao 3-1 dhidi ya Nigeria na mabao 2-1 ilipovaana na Misri.
Katika AFCON mwaka 2019 zilizofanyika nchini Misri, Tanzania ilipangwa kundi C na timu za Algeria, Senegal na Kenya.
Taifa Stars ilimaliza katika kundi hilo ikiwa nafasi ya nne baada ya kufungwa mechi zote tatu.
Kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na Amunike, kilianza kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Senegal, kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Kenya na kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Algeria.
Pia, Taifa Stars iliburuta mkia katika hatua ya makundi ya AFCON mwaka 2023 zilizofanyika nchini Ivory Coast.
Ikiwa imepangwa kundi F, Stars ilivuna pointi mbili (nyingi zaidi ya AFCON ilizoshiriki awali), ikianza kwa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Morocco, sare ya bao 1-1 kutoka kwa Zambia na suluhu dhidi ya DRC.




