Na IRENE MWASOMOLA
BAADHI ya Wataalamu wa Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa, wametaja faida tano za umuhimu wa kudumisha amani nchini, huku wakishauri serikali kuendelea na juhudi za kuimarisha umoja wa kitaifa.
Pia, wameshauri vijana na wananchi wote kwa ujumla kujiepusha na chuki na propaganda zenye lengo la kuligawa taifa.
FAIDA ZA AMANI
Faida hizo ni pamoja na kuvutia wawekezaji na watalii, kuchochea maendeleo, kujenga umoja wa kitaifa, kukuza diplomasia, kuongeza fursa za ajira na kukuza shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Akizungumza na UHURU, Mhadhiri wa Diplomasia kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk. Salim Ahmed Salim, Godwin Gonde, alisema uwepo wa amani nchini una mchango mkubwa katika kuvutia wawekezaji wa kigeni kuja kuwekeza hapa nchini , hatua ambayo inaongeza fursa za ajira.
Pia, Gonde alisema amani ya Tanzania ndio inabeba sura ya nchi kimataifa na ni msingi wa diplomasia ya taifa lolote duniani.
Alisema, uwepo wa amani nchini unasaidia kuwepo uwanda mpana wa kushirikiana na mataifa mbalimbali, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha tunu hiyo inalindwa .
“Amani ina mchango mkubwa sana nchini, kwa sababu ndio ina weka mwanya wa nchi yetu kuwa na mashirikiano na nchi yoyote duniani, amani ndio inabeba taswira ya taifa mnapokuwa na amani ndio mnawahakikishia wageni usalama hata wakuja kufanya uwekezaji .
“Amani ni msingi katika mawanda ya kidiplomasia na mawanda ya mashirikiano ya kimataifa, changamoto tulizopitia (Oktoba 29) ziliweza kutia doa kidogo, lakini bado tuna nafasi ya kufanya juhudi za kuendeleza umoja wa kitaifa,”aliongeza.
Kwa upande wake Mhadhiri kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk. Salim Ahmed Salim, Dk. Innocent Shoo, alisema vijana na wananchi kwa ujumla wana wajibu kulinda tunu ya amani kwa heshima na kujiepusha na propaganda na chuki zinazo chochea kuligawa taifa.
“Vijana wana wajibu wa kutunza amani kutatua migogoro kwa njia ya utulivu, kujiepusha na chuki na propaganda hatarishi.
“Tukumbuke kwamba amani ndio inaleta wawekezaji, fursa za kazi na maendeleo ya kweli na Tanzania imejenga historia ya utulivu na mshikamano, ni jukumu la kila Mtanzania kuhifadhi na kuendeleza urithi huo,”aliongeza.
Mchambuzi wa Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk. Salim Ahmed Salim, Denis Konga, alisema amani endelevu inajengwa kwa ushirikiano wa pamoja, hatua ambayo ina chochea uwepo wa maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Aidha, Konga alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa maridhiano kwa ajili ya kuwepo kwa mustakabali wa kujenga taifa moja.
“Ili maendeleo yaendelee kuwepo lazima kuwe na amani endelevu na amani endelevu inajengwa, hata diplomasia ina kuwepo katika maeneo ambayo kunakuwa na utulivu na utengamano,”aliongeza.




