Dodoma
NA MUSSA YUSUPH
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amekemea urasimu unaofanywa na baadhi ya watumishi wa umma katika kutatua kero za wananchi kwa kisingizio cha taasisi kuandikiana barua kama sehemu ya utekelezaji wa utatuzi wa changamoto ilhali ofisi husika zipo karibu.
Kwa sababu hiyo, ameagiza kukomeshwa vitendo hivyo kwani kwa sasa ofisi zote za wizara zipo katika eneo moja na hakuna sababu ya kuchelewa kuwahudumia wananchi kwa kigezo cha kusubiri majibu ya barua.
Pia, Dk. Mwigulu ameitaka Wizara ya Madini kuongeza kasi ya utafiti kubaini maeneo yenye rasilimali madini ambazo zitatumika katika kuliletea Taifa maendeleo.
Waziri Mkuu aliyasema hayo alipokagua majengo ya Wizara ya Maji na Wizara ya Madini yaliyopo Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
“Tunataka kazi za serikali zifanyike makao makuu ya nchi ili kuwasogezea huduma Watanzania. Tumeendekeza sanduku la Posta mpaka ofisini, ofisi zote za serikali zipo hapa (Mji wa Serikali) linapokuja jambo linalohusu Watanzania yenye kuhitaji utatuzi, ofisi zetu zipo karibu.
“Hakuna haja kuandikiana barua, hapa mnaweza kutembea hata kwa miguu kutatua jambo husika, nimekuwa nikiona katika kikao taarifa ya utekelezaji jambo ninataarifiwa kwamba barua imeshaandikwa. Mnaandikaje wakati ofisi zinatizamana, si mkae muandike muhtasari wa kikao kama mnatafuta kumbukumbu.
Dk. Mwigulu alisisitiza: “Barua ni nusu ya kuonana, sasa si mpo hapa kwanini mnaonana nusunusu? tunapoandika barua tunamia muda mrefu, haya mambo yalikuwa zamani. Kama tunataka kumbukumbu zibaki katika nyaraka za serikali, tuandike yale mambo katika vikao ili twende kwenye utekelezaji. Hii ya kuripoti kumbukumbu ya barua kwamba ni utekelezaji ni kuchelewesha utatuzi wa kero za wananchi.”
MAJENGO YASIYOTUMIKA
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliagiza kuundwa timu kuchunguza majengo ya serikali ambayo hayatumiki licha ya uwepo wa baadhi ya taasisi za umma ambazo zimekuwa zikipanga hatua ambayo imekuwa ikiibebesha mzigo serikali kulipa gharama za pango.
Alisema Dodoma ndiyo Makao Makuu ya Serikali na siyo kambini ambapo alisisitiza kamwe nchi haitokuwa na makao makuu katika maeneo mawili.
“Serikali ilikuwa inaingia gharama kuweka taasisi zake katika mejengo ya kupanga, Makao makuu ya nchi ni Dodoma na tumehamia.Hapa (Dodoma) ndipo makao makuu, hii siyo kambi. Ukienda kambini unawaza kuna muda utarudi nyumbani lakini hapa ndipo makao makuu ya nchi, wala hatutakuwa na makao makuu mbili.
“Wale ambao ofisi zimeshakamilika na bado wameshikilia ofisi zingine wakati bado zipo taasisi za serikali ambazo zinapanga. Nimuagize Katibu Mkuu kuunda timu kupata orodha ya majengo yasiyotumika ili tuyagawe kwa taasisi ambazo zinapanga wakati kuna majengo ambayo hayatumiki,” alisisitiza Dk. Mwigulu.
UTEKELEZAJI DIRA 2050
Waziri Mkuu alisema dira ya maendeleo ilikuwepo tangu enzi za uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya kuhamishia makao makuu ya serikali mkoani Dodoma.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na Hayati Dk. John Magufuli ilianza utekelezaji kwa kujenga majengo na miundombinu ya muda ili kuhamia wakati masuala mengine ya ujenzi majengo ya kudumu yakiandaliwa.
“Ilipoingia Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, majengo rasmi ya kudumu yakaanza kujengwa. Twendeni tukachapekazi kuhakikisha tunatekeleza yale ambayo yapo katika majukumu yetu.
Aliongeza: “Na sasa tunaanza utekelezaji Dira 2025 hadi 2050, kuna mambo yalikuwa yakifanyika mfano kugawana maji 50 kwa 50 mfano wananchi asilimia 50 na 50 yanapotea, natolea mfano. Lakini nilichokuwa nataka kusema ni kwamba ni kukomesha kabisa upotevu wa maji.”
“Tunapokwenda kutekeleza dira mpya tunatakiwa kwenda na ustaarabu na miundombinu inayomwakikishia Mtanzania kupata maji. Dira ya Rais Dk. Samia ambayo imeonyesha katika ilani ni kwenda kuwa na gridi ya taifa ya maji, tunatakiwa kama ilivyorasilimali zingine tujihakikishie matumizi bora na kulinda miundombinu ya maji,” alifafanua.
WIZARA YA MADINI
Akiwa katika jengo la Wizara ya Madini, alitoa wito kwa wizara hiyo kuongeza kasi ya utafiti kubaini maeneo yenye rasilimali madini.
“Dunia ya sasa ni ya rasilimali, dunia ya misaada imeshakwisha, utajiri ni rasilimali, tuendeleze utafiti ili Watanzania waweze kunufaika kupitia rasilimali zao. Usipojua una utajiri kiasi gani ni rahisi kuibiwa.
Alisisitiza: “Maandalizi ya bajeti yanaendelea, lazima kila mwaka tujiwekee lengo tunaongezaje kiwango cha utafiti kama kuwekeza rasilimali tuwekeze kwa sababu maeneo ambayo tumegundua madini huwa yanaisha. Najua tume (Tume ya Maidini) ipo kwenu, tuendelee kukomesha migogoro hasa ile yenye sura ya uonevu.”




