Na SUPERIUS ERNEST
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema msingi wa uimara wake umeanzia katika mashina na ndiyo sababu kimeendelea kuwa imara.
Hayo yalisemwa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, aliposhiriki kikao cha Shina Namba ya Moja, Tawi la Puma, Kata ya Puma, wilayani Ikungi wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani Singida.
“Nimefurahi kushiriki kikao hiki cha Shina Namba moja, niwapongeze viongozi wote wa Tawi kwa uimara wenu. Niwajulishe tu kwamba CCM ni tofauti na vyama vingine, kwani msingi wa Chama chetu ni nguvu ya mashina na wajumbe wa mashina,”alisema.
Alisema kwa msingi huo, ndiyo maana ziara yake inalengo la kukagua na kuimarisha uhai wa mashina ili Chama kiendelee kuwa imara.
Kihongosi alisema CCM ilipata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana ambapo Rais Dk. Samia alipigiwa kura nyingi za ushindi.
Alisema wale wanaoibua hoja kuhusu ushindi wa Chama, niwakupuuza kwani hawaijui msingi wa CCM umeanzia katika mashina siyo wakushtukiza.
Aliwataka wanachama kuendelea kushiriki vikao vya mashina kwani ndiyo msingi na uimara wa Chama.
“Katika ziara hii mkoani hapa, mimi napita katika mashina machache, lakini Katibu Mkuu wetu wa Chama, Balozi Dk. Rose Migiro, amenieleza kuwa atakuja kufanya ziara kupita kila shina kuzungumza na wajumbe wake,”alisema.




