Na HANIFA RAMADHANI, Zanzibar
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kusimamia ajenda ya utunzaji mazingira na kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Amesema suala la mazingira ni miongoni mwa nguzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo ni uhifadhi wa mazingira na ustahamilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Dk. Samia, aliyasema hayo katika tukio la upandaji mitiKusini Unguja, lililoambatana nakumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwake, iliyofanyikaKijiji cha Bungi,Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema msingi huo, unaakisi matumizi endelevu ya rasilimali za asili na kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Rais Samia, alisema upandaji miti ni sehemu ya taifa, kuunga mkono jitihada za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kurutubisha uoto wa kijani ya asili.
“Nitoe maelekezokwamamlaka za upimaji ardhi na upangaji miji nchini kote, kuhakikisha kuwa, katika upimaji wa maeneo mapya, wazingatie kutenga maeneo ya kijani na nafasi ya upandaji miti maeneo ya makazi na matumizi ya ardhi,” alisema
Alisema kufanya hivyo, kutawezesha wananchi kupanda miti na kujenga makazi yenye ustahamilivu wa mazingira.
Rais Samia, alisema mabadiliko ya tabianchi, siyo hadithi wala maneno ya nadharia,baliuhalisia uliopo na nchi zote duniani, zinakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile ongezeko la ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko makubwa, kuongezeka kwa kiwango cha joto na kina cha bahari.
Alisemakwa Tanzania, athari hizo, zimegusa moja kwa moja maisha ya wananchi na ustawi wa taifa kwa ujumla, ikiwemo kadhia ya kukosekanamajisafi na salama, lakiniuchache katika uzalishaji chakula, sambamba na kuathiri afya ya mwanadamu.
“Upandaji miti ni moja kati ya njia mahsusi za kukabiliana na athari hizi, lakini mti unaopanda leo na kutunzwa, utaleta mvua siku zijazo.
“Utaifanya ardhi iwe salama kwa uzalishaji wa chakula, itahifadhi vyanzo vya maji na kuifanya nchi iwe na maji ya kutosha, lakini ustawikwa wananchi.
“Ndugu zangu, tunapopanda miti leo, hatufanyi kama sherehe tu, bali tunatekeleza kwa vitendo ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu na hususani lengo namba 13 la kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ya kupunguza madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa na kuongeza ustahamilivu wa jamii zetu,”alisema.
Alisema upandaji miti hiyo, ni utekelezaji wa lengo namba 15 la ajenda ya 2030, ambayo ni kulinda uhai katika ardhi kwa sababu, kupanda miti na kuitunza ni hatua ya kulinda misitu, kurejesha uoto wa asili, kuhifadhi baianowai, kuhakikisha ardhi inaendelea kuwa na rutubakwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema kuwa, wanapopanda miti, wanatekeleza lengo namba mbili, ambalo ni kuondoa hali ya kutokua na chakula, lakini kutekeleza lengo namba tatu la afya na ustawi wa jamii.
Alisemayote hayo kwa pamoja, yanatekeleza lengo moja kubwa la kuondoa umasikini.
Alifafanua kuwa,wananchi wakiwa na afya njema, chakula cha kutosha, ardhi nzuri, hewa nzuri na nchi kufanya vyema katika biashara ya hewa ukaa, fedha zinapatikana,ni hatua ya kuondoa umasikini.
“Nitoe wito kwa wananchi na wadau wote wa mazingira, kupanda angalau kila nyumba mti, shuleni, kazini au katika maeneo ya jamii na kuhakikisha inatunzwa hadi ikue,” alisema
Aliwataka wananchi kujenga utamaduniwa kulinda na kuhifadhi mazingira kisha kurithishwa kwa watoto.
Alieleza kuwa, mtoto akikabidhiwa mti, akautunza tangu akiwa mdogo, lazima atayapenda mazingirana kumbukumbu ya kulinda maliasili za nchi.
Pamoja nahayo, Rais Samia, aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya, kusimamia maeneo ambayo yameathirika kama vile kuchimbwa mchanga.
Wahakikishe yanapandwa miti kurudisha mazingira katika hali ya kawaida.
“Ndugu zangu, kupanda miti, nimechagua jambo hili katika kila siku yangu ya kuzaliwa kutimiza wajibu wangu kama Mtanzania.
“Kama binadamu, nawajibika kuitunza nakuihifadhi sayari yetu ya dunia tuliyokabidhiwa na MwenyeziMungu na kuacha urithi kwa vizazi vijavyo,” alisema
Alieleza kuwa, kama walivyorithi uoto wa asili mwingi kutoka kwa wazee waliotangua, nao wanapaswa kurithisha vizazi vijavyo.
“Tulirithi miti mingi ya matunda iliyopandwa mashambani, ile iliyojiotea maporini, lakini leo mtoto wetu akitaka kula pera, lazima aendele akalinunue sokoni.
“Sisi tulikuwa tunapita tu msituni, tulikuwa tunakula, sasa miti hiyo, imepotea,ni wajibu wetu kuirudisha miti ya asili ya nchi yetu ili kuleta urithi wa watoto wetu,” alisema
Alisema kuwa, zoezi hilo la upandaji miti ni wajibu wa Watanzania wote wa kutunza mazingira ya nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alieleza kuwa, anaungana na kaulimbiu ya tukio hilo, inayosema; ‘Uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti.’
WAZIRI MASAUNI
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira,Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alisema uongozi wa Rais Samia, umetoa mchango mkubwa uliowezesha taifa kupiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi.
Alisemasekta ya mazingira, inamtambua Rais Samiakama Mwana – mazingira namba moja nchini na miongoni mwa wana-mazingira mahiri duniani.
“Katika kipindi hiki cha uongozi wako, nchi yetu imefanya mageuzi makubwa katika suala la mazingira.
“Hii ni pamoja na wewe mwenyewe kwa shauku yako kubwa ya kimageuzi, umeratibu maandalizi na kuendelea kusimamia utekelezaji wa mkakati wa taifa wa nishati safi ya kupikia, ambao una malengo ya kufikia zaidi ya asilimia 80ya watumiaji ifikapo mwaka 2034,” alisema.
Masauni, alisema imezoeleka kuwa, watu wengi mashuhuri na wenye mamlaka ya uongozi au wananchi wa kawaida kusherehekea kumbukizi ya siku za kuzaliwa kwa sherehe kubwa.
Waziri Masauni, alisemaRais Samia kwa miaka kadhaa, amekuwa na utaratibu wa kuadhimisha siku hiyo kwa kuwa na shughuli za kielelezo zinazohusu uhifadhi wa mazingira kama vile upandaji miti na shughuli nyingine za huduma kwa jamii.
Alisema kuwa, Rais Samia, amenyesha njia ambayo wananchi wanapaswa kuifuata.
MKUU WA MKOA
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, alisema miti 1,705, imepandwa katika eneo hilo la Bungi, kati ya hiyo, 105 ya matunda na 1,600 ya kivuli.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, mkoa huo umepanda miti 62,630, ikiwemo ya matundana mingine 10,000 ya mikoko pembezoni mwa bahari ili kuhifadhi mazingira katika fukwe.





