Na Happiness Mtweve,
Dodoma
UAMUZI wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutoa msamaa kwa vijana waliohusika kwa kufuata mkumbo katika vurugu zilizotokea Oktoba 29 mwaka huu, umepongezwa baada ya serikali kuanza utekelezaji wake ambapo watu zaidi ya 1,000 wanatarajiwa kupata msamaa huo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, amesema mchakato wa kuwaachia huru watuhumiwa hao unaendelea ambapo jumla ya watu 1,736 kati ya 2,045 waliokamatwa wanatarajiwa kuachiwa baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika.
Dk. Homera aliyasema hayo alipotembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa madhumuni ya kujionea utendaji kazi na hatua zinazoendelea katika usimamizi wa mashtaka nchini jijini hapa.
“Hadi kufikia Novemba 25, 2025, jumla ya watuhumiwa 607 kati ya 1,736 wanaotakiwa kuachiwa, tayari wameachiwa huru na wengine waliobaki wataendelea kuachiwa baada ya upekuzi wa kina wa kuridhisha kukamilika,” alieleza.
Amefafanua kuwa watu 309 kati ya 2,045 waliokamatwa kazi ya ufuatiliaji inaendele ambapo alitaja mikoa na idadi ya watu walioachiwa huru ni Manyara mmoja, Mwanza 164, Dar es Salaam 263, Rukwa 10, Mbeya 69, Shinyanga wawili, Geita 74 na Arusha 24 ambao jumla ni 607.
“Tuchukue nafasi hii kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hiki alichokifanya. Huu ni upendo kwa sababu yeye kama mlezi na mzazi ameamua kuchukua hatua kama hizo,”amesisitiza.
MAONI YA WANANCHI
Wakizungumzia uamuzi wa kuachiwa huru watuhumiwa hao, baadhi ya wananchi mkoani hapa wameeleza namna walivyoguswa na hatua hiyo.
Mkazi wa Chidachi, Annastazia Malegesi, amesema hatua hiyo imeonyesha dhamira ya dhati ya Dk. Samia kutaka wananchi wake waishi kwa amani na upendo.
“Tunajua wapo walioingia katika changamoto hiyo kwa kufuata mkumbo. Wengi vijana wetu hawakujua mipango mibaya ya watu kutaka kuichafua nchi yetu. Vurugu zimeichafua nchi yetu ambayo imekuwa yenye amani na utulivu kwa muda mrefu.
Amesisitiza: “Tunaomba vyombo vya dola kuendelea kuimarisha usalama wa nchi yetu kwani wapo watu wenye nia mbaya ambao hawapaswi kupewa nafasi kwa sababu ndiyo wamekuwa wakiwarubuni vijana wetu kuingia katika matatizo.”
Naye, Mkazi wa Mpunguzi, Amos Lichelile amesema Rais Dk. Samia ni kiongozi mwenye mapenzi ya dhati kwa wananchi wake na ndiyo maana mara zote amekuwa akisisitiza umoja, amani na mshikamano nchini.
Ameeleza kuwa, upendo wa Rais Dk. Samia kwa wananchi wake ndiyo sababu ya kuchukua uamuzi wa kuwasamehe vijana waliojikuta katika mikono ya dola wakati wa vurugu.
“Ninawaomba Watanzania wenzangu tukajifunze katika mataifa mengine ambayo yalikuwa yenye neema lakini sasa yameangukia katika umaskini wa kutupwa. Ukienda Libya na Sudan zilikuwa nchi zenye neema lakini sasa hazikaliki kwa sababu ya vita.
“Walichonganishwa kwa sababu ya rasilimali zilizopo, wakakubali kutumbukia katika vita ambavyo hadi leo amani wanaisikia tu. Tusikubali kugeuzwa mfano mbaya, Tanzania ni yetu kwani ikichafuka hakuna tutakapokimbilia,” amesisitiza.




