Na MUSSA YUSUPH, Rufiji
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amepata mapokezi ya aina yake yaliyoacha simulizi kwa wananchi wa Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, waliofurika katika mkutano wake wa kampeni.
Kupitia mkutano huo, Dk. Samia amewahakikishia maelfu ya wananachi endapo CCM itashinda Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu, serikali yake itakuja na mkakati wa kudhibiti mafuriko Mto Rufiji, hivyo kuleta matumaini mapya kwa wakazi wa Rufiji.
Mkakati huo utakaogharimu sh. bilioni 245, utahusisha ujenzi wa kingo za kuzuia mafuriko, uanzishwaji skimu za umwagiliaji hekta 13,000, ujenzi wa mabwawa mawili, kilometa 90 za barabara na makalavati.
Akihutubia mbele ya maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Ujamaa wilayani Rufiji, Dk. Samia amesema mkakati huo utaondoa adha ya mafuriko katika wilaya hiyo.
“Katika bonde lile tunakwenda kujenga mabwawa mawili makubwa. Bwawa la Mbakimtuli na Bwawa la Ngorongo. Pia tunakwenda kutengeneza skimu za umwagiliaji hekta 13,000.
Aliongeza: “Hekta hizo zinatokana na hekta 60,000 ambazo zipo (Bonde la Rufiji) kule za umwagiliaji. Pili ni ujenzi wa zuio la mafuriko yale mambo ya mvua roho zipo juu tunakimbia, wajukuu zangu sasa hayapo.”
“Mkituchagua tunakwenda kujenga zuio la mafuriko. Mkandarasi tayari ameshapatikana gharama yake ni sh. bilioni 245. Pamoja na mradi huu, kutakuwa na ujenzi wa barabara kilometa 90 na makalavati.”
MNADA WA KOROSHO
Dk. Samia aliwapongeza wakulima wa korosho nchini, kwani korosho za Tanzania zimeanza kupata soko zuri duniani.
Hata hivyo, alisisitiza uzalishaji wa zao hilo ufanyike kwa wingi ni lazima serikali iendelee kutoa pembejeo ambazo ni mbolea, dawa na salfa.
“Tumeamua kutumia fedha nyingi mzalishe korosho kwa wingi, mpige mnada alafu fedha iingine kwa mkulima. Nataka kuwaambia Pwani mmeweza kuongeza uzalishaji wa korosho.
Alibainisha: “Rufiji mmeongeza uzalishaji mazao ya chakula kutoka tani 87,829 kwa sababu ya ruzuku tunazowapa na mbolea, ambapo hivi sasa mmefikia tani 112,118.”
Kwa mazao ya biashara, Dk. Samia alisema wilaya hiyo uzalishaji wa zao la korosho umeongezeka kutoka kilo milioni 2.5 hadi kilo milioni 4.2 kwa msimu uliopita.
Alitumia wasaa huo kuwaeleza wananchi hao mnada wa korosho utaanzaa Oktoba 30, mwaka huu, baada ya kukamilika uchaguzi mkuu.
Vilevile, alisisitiza serikali itaendelea kugawa pembejeo kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika.
Aidha, Dk. Samia alisema mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya ufuta na mbaazi bado unaendelea, kwani shabaha iliyopo ni kuona vijiji vinapata maendeleo.
“Kwa wafugaji tumetoa chanjo kwa ruzuku, ng’ombe, mbuzi, kondoo wanachanjwa kwa nusu bei, lakini kuku ni bure. Lengo letu kuangalia afya za wanyama wetu,” alieleza.
Dk. Samia alisema Tanzania imepata soko kubwa la nyama na wanyama hai nje ya nchi, hata hivyo kikwazo ni kukosekana rekodi za dunia kama wanyama hao wamechanjwa au wanatambuliwa.
Kwa sababu hiyo, alisema serikali imeanza kutoa chanjo hiyo Tanzania iingie katika rekodi.
Alieleza serikali inatoa chanjo, kujenga majosho na minada ya mifugo kisha kutafuta masoko ikiwa ni hatua ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
“Lengo la awamu ya sita ni kumtazama mwananchi kiuchumi. Wawekezaji wanaokuja katika maeneo yetu wanapaswa kurudisha hisani katika maeneo waliyowekeza.
“Kurudisha hisani ni kuzungumza na halmashauri watakubaliana kufanya jambo fulani. Wananchi ndiyo watakaofaidika na hisani itakayorudishwa,” alibainisha.
Pia, alisema jambo la pili ambalo wawekezaji wanapaswa kufanya ni kutoa ajira kwa vijana na ndiyo sababu serikali inajenga shule za ufundi.
Kuhusu sekta za uzalishaji ambazo ni kilimo, uvuvi na viwanda, alisema upande wa kilimo wilaya hiyo ina wakulima wa mazao ya chakula na biashara.
Katika elimu, alisema kabla ya kuingia madarakani wananchi walilazimika kuchanga fedha za ujenzi wa madarasa hali ambayo kwa sasa haipo.
“Huo ni uwezeshaji wananchi kiuchumi badala ya kuchangia fedha, kaa nayo fanya mambo mazuri katika familia.
“Tunajenga stendi, masoko, taa za barabara katika miji. Nimefurahi wakati nakuja huku (Rufiji) si chini ya nusu kilometa yote ina taa ndani ya mji wa Rufiji,” alisema.
Dk. Samia alieleza miundombinu hiyo ni fursa za kibiashara, kwani watatumia maeneo hayo kufanya biashara hata nyakati za usiku.
Kwa upande wa uvuvi, alisema serikali ilipeleka boti mbili kubwa za abiria ambazo zimechangia kupungua uvuvi haramu kutoka asilimia 70 hadi 30.
Alieleza katika kipindi hiki imeshuhudiwa kuongezeka mazao ya samaki wa maji baridi na chumvi kutoka tani 610,000 hadi tani 900,000.
Kadhalika, Dk. Samia alisema serikali itajenga kiwanda cha kusindika mazao ya samaki na kujenga mabwawa matano ya kufugia samaki katika kata za Utete, Mbwara, Mkongo, Ngorongo na Ikwiriri.
KATIBU MKUU WA CCM
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, alisema Wilaya ya Rufiji imefunguka, kwani mambo makubwa yamefanyika kwa kuimarika huduma za kijamii.
Pia, alisema miradi mikubwa ya kimkakati ipo katika wilaya hiyo hatua ambayo imechochea ongezeko la fursa za kiuchumi na ajira.
“Umetajwa kama kinara wa maendeleo, kama daktari bingwa wa maendeleo na hilo halina ubishi, kwani kila tulipopita tumeshuhudia kwa macho yetu,” alisisitiza.
Aliongeza: “Rais Samia anafahamu vizuri mikakati ya maendeleo itakavyonufaisha wilaya yetu ya Rufiji, itakavyonufaisha maendeleo ya taifa letu.”
“Tutakapokwenda kupigakura tunakwenda kuchagua maendeleo ya taifa letu. Ni wakati wa kuvuna matunda mema ambayo Dk. Samia ameyapanda,” aliongeza.
MCHENGERWA ATAJA NEEMA
Naye, Mgombea ubunge Jimbo la Rufiji, Mohemmed Mchengerwa, alisema Wilaya ya Rufiji imepokea wawekezaji wa kilimo cha ndizi kwa zaidi ya sh. trilioni moja.
Alisema uwekezaji huo utaiwezesha Rufiji kuwa kinara kwa uzalishaji ndizi Afrika, hatua ambayo itatanua wigo wa uchumi na ajira.
Pia, alisema wamepokea wawekezaji katika kilimo cha chikichi ambapo zaidi ya sh. bilioni 400 zitawekezwa.
Mgombea huyo alieleza baada ya karne na nusu historia mpya inakwenda kuandikwa, kwani Oktoba 29 mwaka huu, Watanzania watamchagua Rais wa kwanza mwanamke kupitia sanduku la kura.
Mchengerwa alimpongeza Dk. Samia kwa kutoa kipaumbele cha utekelezaji miradi ya maendeleo, kwani katika kipindi cha miaka minne ametoa sh. trilioni sita kuboresha maisha ya Watanzania.
Alisema katika fedha hizo, sh. trilioni moja zimetumika kujenga hospitali mpya za wilaya zaidi ya 100, ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 500 na zahanati zaidi ya 1,400.
Katika elimu alisema Dk. Samia alitoa sh. trilioni nne zilizotumika kujenga shule za msingi zaidi ya 600, shule za sekondari zaidi ya 400 na shule 22 za mchepuo wa sayansi kwa wanawake.
“Rufiji ilikuwa na shule nne za sekondari, kipindi chako umejenga shule mpya za sekondari 22. Tulikuwa na shule za msingi 19 wakati wako umejenga shule za msingi 63,” alieleza.
Piam zaidi ya sh. trilioni moja zimetumika kuboresha mtandao wa barabara za mjini na vijijini huku madaraja zaidi ya 5,000 yamejengwa.
“Ulikuwa mstari wa mbele kuwafariji Watanzania. Umetupatia sh. bilioni 17 kujenga daraja la Bibi Titi, umejenga mtandao wa barabara za lami hapa Rufiji zaidi ya kilometa 20.
“Ulikuja ukaamsha ndoto ya Mwalimu Nyerere kukamilisha mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere. Tunakushukuru sana kwa kuiingiza katika ilani ya uchaguzi barabara ya Mloka- Mkongo na Ikwiriri-Mkongo,” alisema Mchengerwa.
Alimshukuru Dk. Samia kwa kuridhia ujenzi wa barabara ya Nyamwage -Utete ambayo kwa muda mrefu imekuwa changamoto.
Hata hivyo, Mchengerwa ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), alimuomba Dk. Samia kugawanywa kwa mkoa wa Pwani kisha kuanzishwa Mkoa wa Rufiji.
Alisema hatua hiyo itarahisisha utoaji huduma kwa wananchi wanaolazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma.
“Maelekezo uliyoyatoa kwa wakuu wa wilaya kote nchini wanakwenda kuyafanyia kazi. Umeelekeza tarehe 29 ni siku ya kupigakura. Kila mkoa utahakikisha unaweka ulinzi. Kila Mtanzania ajitokeze kumchagua Dk. Samia,” alisema.




