Na NASRA KITANA
WAKATI kikosi cha timu ya Yanga kikitarajiwa kushuka dimbani leo kumenyana na Silver Strikers ya Malawi, kaimu kocha Mkuu wa Yanga, Patrick Mabedi amesema ushindi dhidi ya Silver Strickers ni muhimu, kuhakikisha timu inatinga hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), mwaka huu.
Yanga leo itashuka dimbani katika mchezo wake wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver utakaochezwa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam saa 11:00 jioni.
Timu hiyo itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza bao 1-0 katika mchezo wake wa kwanza uliochezwa nchini Malawi, hivyo Yanga anahitaji ushindi kutinga hatua inayofuata.
Akizungumza jijini Dar es Salaam,jana, Mabedi alisema mchezo huo ni muhimu kwa Yanga kushinda na kuwapa furaha mashabiki.
“Yanga ni klabu kubwa ina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuyapindua matokeo ya kufungwa ugenini na kushinda nyumbani hivyo naamini watafuata kile ambacho nimewafundisha katika uwanja wa mazoezi kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema Mabedi.
Kocha huyo alisema kuwa baada ya kutua nchini Jumatatu wakitokea Malawi, walianza mazoezi Jumanne na kufanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika pambano la kwanza na wapo tayari kukabiliana na wapinzani wao.
Kocha huyo alifafanua kuwa mpira wa miguu kila mechi ina presha yake, lakini hilo halimpi tabu kwa sababu ametoka katika timu yenye presha, ana imani kila kitu kitaenda sawa.
Kocha wa Silver Strickers, Etson Kadenge amesema anafahamu anakutana na Yanga yenye wachezaji bora, lakini kwa upande wao wapo tayari kumalizia dakika 90 za uamuzi wa kufuzu hatua ya makundi na kwamba anatarajia mchezo mzuri na wa ushindani.
“Wachezaji wangu wapo tayari na wameahidi kutumia dakika 90 kushindana na Yanga kupata nafasi ya kufuzu hatua inayofuata wanatambua wanakutana na wapinzani bora ambao pia wanataka matokeo ili kutinga hatua inayofuata,” alisema Kadenge.
Nyota wa Yanga, Dikson Job alisema kuwa kama wachezaji wamejipanga kuhakikisha wanapambana kwa jasho na damu ili kupata ushindi.
“Sisi tupo tayari kwa ajili ya mchezo na tunatambua umuhimu wa mchezo huu, tutahakikisha tunapata ushindi, niwambie tu mashabiki na wapenzi wa Yanga wanatakiwa kutupa sapoti ya kutosha tufikie malengo ya kutinga hatua ya makundi,” alisema Job.
Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuelekea katika mchezo huo ambao hautakuwa na kiingilio mageti yatafunguliwa saa nne asubuhi na kufungwa saa nane na nusu mchana.
Alisema kuwa sababu kubwa ya kupanga muda huo wa mashabiki kuingia uwanjani ni kuepusha msongamano wa watu pamoja na kuwapa nafasi timu kuingia bila ya shida yeyote.
“Tumekaa kikao na wenzetu wa ulinzi na usalama hivyo tumekubaliana mageti yatafungulia rasmi saa nne kamili asubuhi na kufungwa saa nane na nusu mchana hiyo yote kuepusha msongomano wa watu,” alisema Kamwe.
MCHEZO MWINGINE
Wakati Yanga ikishuka dimbani kumenyana na Silver katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu ya Singida Black Stars nayo itashuka dimbani katika mchezo wake wa marudiano Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Flambeau ya Burundi.
Singida Black Stars inatarajiwa kucheza mchezo wake huo wa marudiano katika Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi saa 1:00 usiku huku ikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wake wa kwanza.
Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo na kutinga hatua ya makundi.
“Tunatakiwa kushinda au kupata sare katika mchezo wetu huo, tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi na kusonga mbele hatua inayofuata,” alisema Gamondi.




