Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais wa Comoro ambaye pia ni Spika wa Bunge la Taifa hilo, Moustadroine Abdou, amesema Serikali ya Comoro itaendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na Tanzania, hususan katika sekta ya afya ambayo imekuwa mfano wa mafanikio ya ushirikiano wa kikanda.
Akizungumza alipotembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasili nchini kumwakilisha Rais wa Comoro katika sherehe za uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Abdou amesema amevutiwa na maendeleo makubwa ya huduma za afya nchini.
“Nimefika Tanzania kwa mara ya tatu. Nchi hii ni tulivu, yenye amani na watu wenye upendo. Nawapongeza kwa uchaguzi mzuri na kumpata kiongozi bora, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema Abdou.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro katika sekta ya afya umeendelea kuimarika, ambapo madaktari wa Tanzania wamekuwa wakitoa huduma na mafunzo nchini humo, sambamba na wananchi wa Comoro kufika Tanzania kupata matibabu kutokana na vifaa vya kisasa na miundombinu bora iliyopo.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Said Yakoub, amemshukuru Makamu wa Rais huyo kwa kuitembelea ORCI na kueleza kuwa amekuwa balozi mzuri wa kuitangaza Tanzania kwa wananchi wa Comoro kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo kwa nchi hii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Diwani Msemo, amesema uhusiano wa Tanzania na Comoro ni wa kihistoria na umejikita katika misingi ya urafiki wa watu na serikali zao, ambao sasa unaendelea kuimarishwa kupitia sekta mbalimbali ikiwemo afya.
“Tuna furaha kuona viongozi wa Comoro wanatambua mchango wa Tanzania katika afya na kuendeleza ushirikiano huu wa kidugu,” amesema Dk. Msemo.




