ATHNATH MKIRAMWENI
NA REHEMA MAIGALA
WANASIASA na wadau wa maendeleo nchini, wametaja ushindi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa wa kihistoria.
Watanzania wametakiwa kumuunga mkono katika jitihada zake za kuliletea taifa maendeleo.
Kauli hiyo, waliitoa wakati wakizungumza na UHURU na kusema kuwa, katika ushindani wa kisiasa, lazima kuwepo na mshindi, hivyo ni vyema wakaweka tofauti zao pembeni na kuleta maendeleo.
Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele, alipongeza ushindi wa Rais Dk. Samia na kusema kuwa, katika ushindani wa kisiasa lazima kuwe na kushinda na kushindwa.
Mwaijojele, alisema ushindi wa Rais Dk. Samia ni wa kisheria na kidemokrasia, hivyo Watanzania wote, wanapaswa kukubali matokeo na kuungana naye kwa maendeleo ya taifa.
Aliongeza kuwa, wakati wa kampeni, kila mgombea alikuwa na nia njema ya kulitumikia taifa, sasa ni wakati wa kuunganisha nguvu, kumsaidia katika kutekeleza yale aliyoyaahidi kwa wananchi.
Alifafanua kuwa, jukumu kubwa kwa sasa ni kuhakikisha Rais Samia, anatekeleza yale ambayo Watanzania wanatarajia, hususan katika kusikiliza kero za wananchi na kuhakikisha haki inatendeka kwa wote.
Pia, alisema pale ambapo hakuna haki, amani hupotea, ndiyo maana ni muhimu kwa serikali kuimarisha misingi ya usawa na utawala bora.
Vilevile, alisema vyama vya siasa, vina wajibu wa kujifunza kutokana na matokeo ya uchaguzi, kurekebisha kasoro zilizojitokeza na kuendelea kuchangia katika maendeleo ya demokrasia nchini.
Alimshauri Rais Dk. Samia kwa kuendeleza mapambano dhidi ya ubadhirifu wa mali ya umma na mianya ya ufisadi, huku akihakikisha hakuna mtu anayeonewa.
Mwaijojele, alisema misingi ya amani inajengwa katika kuhakikisha haki inatendeka kwa kila raia, bila upendeleo na kuwataka waandishi wa habari, kuendelea kuandika habari zenye ukweli, zinazojenga umoja wa kitaifa badala ya kueneza taarifa zinazoweza kuvuruga amani au kuchochea migawanyiko miongoni mwa wananchi.
Pia, aliishukuru serikali, waandishi wa habari na wananchi wote kwa uvumilivu waliouonesha kipindi cha uchaguzi, licha ya changamoto zilizojitokeza kama vurugu na usumbufu wa huduma za kijamii.
Alisema sasa ni wakati wa kutunza amani na kujikita katika kazi za maendeleo, kwani hakuna maendeleo bila utulivu.
Naye, aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha ADA–Tadea, George Busungu, alipongeza ushindi wa Rais Dk. Samia, akisema ni wa haki na unaonesha imani kubwa ya Watanzania kwa uongozi wake.
Alisema hana pingamizi lolote dhidi ya matokeo hayo, bali anaunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia, kuendeleza kazi alizozianza, hususan katika maeneo ya ajira na maendeleo ya wananchi.
Busungu, alisema sasa ni wakati wa Watanzania wote kuungana na kumuunga mkono Rais katika kutekeleza ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni.
Aliongeza kuwa, badala ya vurugu na malalamiko yasiyo na msingi, wananchi wanapaswa kutulia na kuruhusu serikali iendelee na kazi zake kwa manufaa ya wote.
Alisisitiza kuwa, amani na utulivu ni nguzo muhimu za maendeleo na hivyo kila Mtanzania anapaswa kuchangia katika kulinda hali hiyo.
Kwa upande wa aliyekuwa mgombea Urais wa Chama cha UPDP, Twalib Kadege, alisema ushindi wa Rais Dk. Samia ni wa historia nchini.
Alisema utekelezaji wake umemsababisha Watanzania wengi kumpigia kura za ndiyo, baada ya kumwamini ufanisi wake wa kazi.
“Miradi ya maendeleo aliyoitekeleza imemsaidia kupata kura nyingi kutoka kwa wananchi na ushindi alioupata ni sifa kubwa.
“Katika ushindani ni lazima mshindi apatikanike hivyo kati ya wagombea 17 wa kiti cha Urais mshindi mmoja amepatikana ambaye ni Rais Dk. Samia,” alisema.
Hivyo, Kadege aliwaomba Watanzania washikamane na Rais Dk. Samia katika kukuza uchumi wa Taifa na kudumisha amani ya utulivu.
Vilevile, aliyekuwa mgombea wa kiti cha Urais wa chama cha NLD, Hassan Doyo, alisema ushindi alioupata Rais Dk. Samia ni wa kishindo kwa sababu katika uongozi wake wa miaka minne aliwafanyia mambo mazuri Watanzania.
“Uongozi wake wa miaka minne, umemfanya apate kura nyingi kutoka kwa wananchi na sisi wagombea wenzake tutahakikisha tupo naye katika kulijenga taifa,” alisema.
Katibu Mkuu wa chama cha UMD, Moshi Kigundula, aliwaomba Watanzania washikamane kwa pamoja kuleta maendeleo nchini, kwa sababu Rais Dk. Samia ni kiongozi mwenye kupenda maendeleo kwa watu.
MWANASIASA MKONGWE
Kwa upande wake, Mwanasiasa Mkongwe nchini, Anna Abdallah alitoa pongezi za dhati kwa Rais Dk. Samia kutokana na ushindi wake mkubwa na kusisitiza kuwa, ni wa kihistoria na haujawahi kushuhudiwa.
Anna alisema matokeo hayo, yanaonyesha wazi kuwa, wananchi walimwamini na walikuwa wanamtaka Dk. Samia kuendelea kuongoza nchi, jambo linalothibitisha mapenzi makubwa ya Watanzania.
“Wale waliodhani kwamba, wanaweza kumharibia Rais Dk. Samia wamepata funzo muhimu, kwani huwezi kumharibia mtu ambaye tayari amebarikiwa na Mungu na anapendwa na wananchi wake,” alisema.
Alisema ushindi huo, umeleta faraja kubwa kwa Watanzania, kwani sasa taifa lina kiongozi halali ambaye amechaguliwa na kuapishwa rasmi, hivyo wananchi wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kuijenga nchi badala ya kugawanyika kwa misimamo ya kisiasa isiyo na tija.
Pia, alihimiza umoja na ushirikiano miongoni mwa wananchi na kuwa, ni muhimu kila mmoja kutumia muda wake kufanya kazi kwa bidii, kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia katika kuleta maendeleo ya taifa.
ALIYEKUWA MTAKWIMU MKUU
Aliyekuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa, aliupongeza ushindi wa kishindo wa Rais Dk. Samia na kusema umetokana na kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha miaka minne ya uongozi wake ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu mizuri na miradi ya maendeleo.
Alisema Rais Dk. Samia alitekeleza vyema miradi ya maendeleo aliyoachiwa na Hayati Dk. John Magufuli na ndio maana, amepata kura nyingi kwa sababu ya utekelezaji wake.
“Ushindi wa Rais Dk. Samia umetokana na utekelezaji wake mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao umesababisha Tanzania kupata miradi ya maendeleo ukiwemo treni ya kisasa ya Umeme (SGR),” alisema.
MWENYEKITI CCM MKOA WA TANGA
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, alimpongeza Rais Dk. Samia na Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kwa ushindi mkubwa wa kihistoria uliotokana na kazi kubwa ya Chama katika kutekeleza Ilani yake.
Alisema kuwa, ushindii huo unawapa deni CCM kuendelea kuwatumikia zaidi wananchi na kutekeleza Ilani ya Maendeleo kupitia ilani ya Chama ya 2025 hadi 2030.



