SIMON NYALOBI NA ZIANA BAKARI
BAADHI ya wasomi, viongozi wa dini na wanasaikolojia, wagusia umuhimu wa wananchi kuwa wazalendo kwa taifa lao kwa kuwa, ni nguzo ya maisha na maendeleo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na UHURU hili, walisema wananchi wanapaswa kuupa umuhimu uzalendo katika maisha yao ya kila siku.
DK. PHILIP DANINGA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dk. Philip Daninga, alisema wananchi wanatakiwa kuthamini uzalendo kwa nchi yao.
“Katika nchi yoyote na mahali popote, maisha na maendeleo ni lazima, wananchi wawe na uzalendo, kwa hiyo mimi nasema uzalendo ndiyo msingi wa maisha na maendeleo katika nchi, yaani wananchi wake, wanafanya mambo mema kwa nchi yao.
“Wananchi wanapaswa kuelewa iwapo utaharibu rasilimali za nchi, maana yake unajiua mwenyewe na kuishi unaishi nchi hii na unaishi mara moja tu,”alisema.
Dk. Daninga, alisema wananchi wanapaswa kuonesha uzalendo kwa kushirikiana kulinda amani ya nchi na kujituma kufanya kazi kwa faida yake na taifa kwa ujumla.
Alisema kwamba, wananchi wanatakiwa kuendeleza mshikamano na kushirikiana na serikali katika mipango yake ya kuleta maendeleo.
Mhadhiri mwandamizi huyo wa MNMA, alisema wananchi wanatakiwa kujenga tabia ya kuvumiliana na kusikilizana katika kujadili mambo yao.
“Tujenge tabia ya kusikilizana na kulinda amani yetu, kwa kuwa bila ya amani hatuwezi kwenda mbele,”alisema.
Alishauri matukio ya uvunjifu wa amani na uhalifu uliotokea Oktoba 29, mwaka huu, yasahaulike na ukurasa mpya wa maisha, uanze.
“Wito wangu ni kusahau yaliyotokea, tujifunze kutokana na matukio hayo, tuanze kutenda mema kwa taifa letu kwa ubora zaidi na tusonge mbele,”alisema.
DK. SYLIVESTER RUGEIHYAMU
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Sylivester Rugeihyamu, alisema suala la uzalendo hivi sasa, linapaswa kupewa kipaumbele kwa watu wote.
Dk. Rugeihyamu, alisema matukio ya uharibifu wa mali za umma na binafsi yaliyotokea hivi karibuni, yametoa taswira elimu ya uzalendo inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi.
Mhadhiri mwandamizi huyo wa UDSM, alisema elimu ya uzalendo inapaswa kuanza kutolewa kwa wote.
“Tunatakiwa sasa uzalendo ueleweke kuanzisha ngazi ya viongozi wa juu hadi mwananchi wa chini, aelewe umuhimu wa uzalendo kwa taifa lake,”alisema.
Alisisitiza elimu ya uzalendo isibakie kwa wanafunzi walioko shuleni pekee, isipokuwa isambazwe kwa wananchi walioko mitaani kupitia njia mbalimbali.
Pia, aliwashauri wananchi kila mtu kwa nafasi yake mahali alipo, kuhamasisha hali ya uzalendo kwa mwenzake, ndiyo maana halisi ya suala hilo itakapotamalaki nchini.
DK. NKWABI SABASABA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni (FDC), Dk. Nkwabi Sabasaba, alisema wananchi wanapaswa kuwa wazalendo kwa kubadilisha mitazamo kuhusu nchi.
“Kitu cha msingi, wananchi wanachopaswa kufanya ni kuwa na mtazamo chanya kuhusu nchi yao, wasiwe na mtazamo hasi kuhusu maendeleo ya nchi yao kwa kuwa, haikuanza sasa.
“Wajiulize iwapo babu na bibi zetu waliishi nchi hii bila ya matatizo, basi na wao, wadumishe amani na kuipenda nchi yao na kupendana wenyewe kwa wenyewe,”alisisitiza.,
Dk. Nkwabi, alishauri katika kuendeleza uzalendo na kulinda amani, kunatakiwa kuwepo kwa mawasiliano mazuri kati ya viongozi na wananchi kwa ujumla.
Mhadhiri mwandamizi huyo wa FDC, ambaye ni mwanasaikolojia maarufu nchini, alifafanua mawasiliano mazuri kati ya viongozi na wananchi yakidumishwa, ndiyo yataleta umoja na ushirikiano katika kujenga nchi.
MWANASAIKOLOJIA
Mwenyekiti wa Kamati Endelevu ya Taaluma kutoka Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA), Jesusa Malewo, alisema uzalendo unatokana na uwajibikaji, uaminifu na uwazi, ambapo vitu hivyo vikifuatwa vizuri, vitasaidia taifa kuliweka na hali nzuri.
Kwa mujibu wa Malewo, wananchi wanapaswa kuheshimiana na kuthaminiana kwa sababu, taifa lililokuwa bora, linahitaji jamii yake kuwa kitu kimoja.
“Niwasihi wananchi, kutafuta taarifa na maarifa sahihi kutoka vyanzo husika, tusipende kuchukua taarifa au kusikiliza taarifa zisizokuwa sahihi na tujitahidi kutafuta ufumbuzi wa kutatua changamoto zetu wenyewe zinazotukabili,”alisema
VIONGOZI WA DINI
Askofu Mkuu wa Kanisa la Shalom Gospel Assembly Tanzania, Elias Mwakalukwa, alisema kuwa, umuhimu wa uzalendo ni hali ya mtu kuipenda, kuithamini na kujitoa kwa nchi yake na kuweka maslahi ya nchi mbele.
Alifafanua kuwa, unapoithamini nchi yako basi, unapaswa kuwathamini na viongozi waliopo madarakani, ambao huchaguliwa na Mwenyezi Mungu.
Akizungumzia nini kifanyike kulinda uzalendo na thamani ya taifa, Askofu Mwakalukwa, alisema jambo la msingi ni kudumisha amani na kutanguliza mbele maslahi ya taifa na siyo ya mtu binafsi.
“Niwaombe sana wananchi, tuilinde nchi yetu, tusikubali kuichafua, niwaombe vijana wanapaswa kutambua kuwa, jambo muhimu la kulipa kipaumbele ni kudumisha amani kwa kuwa, bila ya amani, hakuna maendeleo yoyote nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Yussuph, aliwasihi wananchi kulipenda taifa lao na kutii mamlaka zilizopo nchini.
Pia, aliwahimiza wananchi kuwa wazalendo na kuendelea kudumisha amani ambayo ni nguzo muhimu inayopaswa kupewa kipaumbele.




