Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
BAADHI ya Wajumbe wa Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), wamesema wanatarajia kusikia hotuba yenye mikakati madhubuti na Dira ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo anatarajiwa kulihutubia baraza hilo.
Wakizungumza na UHURU kwa nyakati tofauti, wajumbe hao, walisema hotuba za Dk. Mwinyi, mara zote huwa ni fupi, zenye uzito na kujaa mipango inayotekelezeka.
Hivyo, wanatarajia ujumbe wenye msukumo wa maendeleo na mwongozo wa awamu ya pili ya uongozi wake.
MWAKILISHI JIMBO LA KIJINI
Mwakilishi wa Jimbo la Kijini, Badria Atai Masaoud, alisema wanasubiri kwa hamu kusikia namna Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), itakavyotekeleza ilani mpya ya CCM kwa kipindi kijacho, ambayo imeweka vipaumbele 10 muhimu vilivyotangazwa na Rais Mwinyi wakati wa kampeni.
“Tunatarajia kusikia mkakati mahsusi wa namna ambavyo vipaumbele hivyo 10, vitafanyiwa kazi kwa ufanisi.
“Rais Dk. Mwinyi, siku zote amekuwa akisisitiza utawala bora, uwajibikaji na uadilifu kwa viongozi, hivyo tunatarajia kuona msisitizo zaidi katika maeneo hayo,” alisema Badria.
Aliongeza kuwa jukumu lao kama wawakilishi ni kuhakikisha wananchi wanasimamiwa ipasavyo, wanapata huduma bora na kwamba, mipango yote ya maendeleo inayotangazwa na serikali, inatekelezwa kikamilifu.
“Sisi tupo tayari kushirikiana na Rais (Dk. Mwinyi) kwa karibu katika kuhakikisha ilani ya CCM, inatekelezwa kwa vitendo. “Wananchi wametupa dhamana, hivyo ni wajibu wetu kuwasemea na kuwasimamia katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza.
MWAKILISHI JIMBO LA JANG’OMBE
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe, Ali Abdulghulam Hussein, alisema hotuba ya Rais Mwinyi, itakuwa dira ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuendeleza ahadi ambazo alizitoa wakati wa kampeni.
Alisema Dk. Mwinyi ni kiongozi mwenye maono makubwa na dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu, hivyo hotuba yake, itatarajiwa kutoa mwongozo wa wazi wa kuimarisha sekta mbalimbali.
Aidha, wajumbe hao, walisema kipindi cha pili cha uongozi wa Dk. Mwinyi, kinatarajiwa kuwa cha kasi zaidi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hususan inayolenga kuimarisha uchumi wa visiwa hivyo.




