Na REHEMA MAIGALA
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetoa pole kwa madhila waliyoyapata baadhi ya Watanzania, yaliyotokea siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu, katika baadhi ya mikoa nchini, huku ukiwasihi vijana kutojiingiza katika vitendo vya machafuko.
Pia, umelaani vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani na kuwataka vijana, wazazi na jamii, kushikamana kwa pamoja kwa sababu, amani ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Kawaida, alisema hayo jijini Dar es Salaam, alipotoa tamko la umoja huo na kusema kilichotokea Oktoba 29 ni vitendo vya uvunjifu wa amani ndani ya nchi, ambavyo vilifanywa na vijana.
“Leo ni tofauti na siku nyingine, nimesimama mbele yenu waandishi wa habari siyo kwa furaha, ila ni huzuni moyoni mwangu kutokana na kile kilichofanyika Oktoba 29, ninawapa pole Watanzania wote waliofikwa na madhila hayo,” alisema.
Kawaida, alisema uchaguzi ulikuwa na matokeo mazuri ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini ndani yake ulikuwa na vurugu ambazo zimeacha alama za maumivu na hasara kubwa.
“Katika hili, nina huzuni zaidi na vijana wetu ambao tunaamini ni nguzo na nguvu kazi ya taifa katika uzalishaji,” alisema.
Kawaida, alisema analaani kwa dhati vitendo hivyo, kwa sababu vinakiuka sheria na utaratibu wa jamii, pia vinahatarisha maisha ya watu wengine, yakiwemo maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Ninaumia zaidi kuona vurugu hizo zikirabitiwa na vijana wenzetu, ambao wengi hawapo nchini na baadhi siyo raia wa nchi yetu, tena huenda hawatarudi tena hapa nchini, huku wakiwashawishi vijana wa Kitanzania kupitia mitandao ya kijamii, huku wao wakiwa wamestarehe nchi za nje wakitunzwa na wale waliowatuma.
“Nchi yetu wanaichoma moto huku wao wakipokea malipo, bahati mbaya waliwarubuni vijana waliokuwa na nia njema, wakidhani ni kusanyiko la halali kuelezea maoni yao, kumbe wenzetu walikuwa na nia mbaya,”alisema.
Kawaida aliwaomba wazazi na walezi, kuwakumbusha vijana kuwa uhuru wa kuandamana siyo haki ya kutoa maangamizi na kuhatarisha maisha ya watu wengine, siyo sahihi kuchoma mali ambazo zimejengwa kwa kodi za Watanzania.
“Taa za barabarani, vituo vya mabasi, vituo vya polisi, zahanati ni vituo vinavyotoa huduma kwenu wenyewe na walioshiriki vurugu, wengine walipoumia, ilitakiwa wapelekwe zahanati zilizopo jirani, lakini zilichomwa moto, hali iliyosababisha baadhi ya watu kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma ya afya mapema,”alisema.
Alisema kilichotokea anakiita ni vurugu, badala ya maandamano kwa sababu, sheria ya nchi ya maandamano ni lazima yawe na kibali, njia na muda.
ATHARI ZA VURUGU
Mwenyekiti huyo wa UVCCM, alisema kutokea kwa vurugu hizo, kulisababisha kufungwa biashara nyingi, hususan maeneo makubwa jijini Dar es Salaam, ambako masoko makubwa hayakuwahudumia Watanzania.
Alisema hali hiyo, ilisababisha hasara kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa na kuathiri maisha ya kila mwananchi.
“Katika hili sote ni mashahidi, kwani amri ya kukaa ndani, imetutesa wengi na kuathiri familia nyingi zenye kipato cha chini, ambazo ni asilimia kubwa ya Watanzania,” alisema.
Aliongeza vurugu hizo, zimeathiri biashara ya Kikanda kwa nchi jirani, zikiwemo Kenya, Malawi, Zambia, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Uganda, ambao hutegemea Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha bidhaa muhimu kama mafuta na mazao mengine.
“Vijana wenzangu, tunapofanya vurugu hapa nchini, athari zake haziishi hapa hapa Tanzania, maumivu yanasafiri hadi kwa vijana wenzetu wa nchi jirani.
“Vijana wenzangu wapendwa, mnapoamka kila asubuhi kwa vurugu za aina ile, wafikirieni wale wanaotegemea amani ambayo inawaongoza kupata chakula au mahitaji muhimu,” alisema
FAIDA ZA AMANI NCHINI
Kawaida, alisisitiza amani ya nchi ina nguvu kubwa kwa sababu, siyo udhaifu, bali ni nguvu ya kutoa maendeleo endelevu.
“Tushikamane na tuzungumze kwa pamoja, siyo kuwa na mitazamo ya kufanya vurugu. Amani inatufanya kushiriki pamoja katika mchakato wa kidemokrasia kupitia chaguzi na mazungumzo na siyo vurugu,” alisema.
Aidha, alisema amani ndiyo kitu pekee kinachofungua milango ya maisha bora na siyo vurugu, hivyo aliwahamasisha vijana kuendelea kuitunza amani.
PONGEZI
Kawaida alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi katika Uchaguzi Mkuu na kumtakia kila la kheri katika kazi iliyo mbele yake ya kuwatumikia Watanzania.




