AMINA KASHEBA Na NASRA KITANA
BAADA ya Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Zungu kuibuka mshindi wa kinyang’anyiro cha Kiti cha Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambapo anakuwa Spika wa tisa wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadau wa soka wamempongeza kwa kuibuka kidedea.
Zungu aliibuka mshindi na kutangazwa jana jijini Dodoma, kwa kupata kura 378 dhidi ya wapinzani wake Veronica Charles Tyeah wa Chama cha NFA ambaye hakupata kura, Anitha Alfan wa Chama cha NLD, aliyepata kura moja, Ndoge Said Ndonge wa AFP aliyepata kura moja na Amin Alfred Yango wa ADC ambaye hakupata kura.
Zungu ambaye ni mdau mkubwa wa soka, amekuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 20 hadi hivi sasa, ambapo aliingia bungeni rasmi mwaka 2005 na kushika nyadhifa mbalimbali kama Mwenyekiti wa Bunge 2012-2021, Naibu Spika 2022 mpaka 2025 kabla ya jana kuwa Spika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa kama Simba wanampongeza Zungu kwa kuteuliwa kuwa Spika wa Bunge.
Alisema kuwa hiyo ni fahari kubwa kwa Simba wanajivunia kuwa na Spika wa Bunge ambaye ni mdau mkubwa wa mchezo wa soka.
“Sisi kama Simba tunampongeza Zungu kwa hatua kubwa ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge, tuna imani kuwa atafanya vyema katika majukumu yake kwani pia ni mdau mkubwa wa soka,” alisema Ahmed.
Mchezaji wa zamani Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema ushindi wa Zungu ni fahari kwa wanamichezo kutokana na yeye kuwa mdau mkubwa wa sekta hiyo.
Alisema anampongeza Zungu kwa hatua hiyo kwani imeonyesha hata sekta ya michezo kuna watu mahiri ambao wanaweza kuongoza bunge.
“Nampongeza kwa ushindi huo kwani Zungu amekuwa mdau mkubwa wa michezo hasa ni shabiki wa Simba, hivyo kwetu wanamichezo ni furaha kwa sababu ni mwenzetu,” alisema.
Mongella alisema hiyo ni hatua kubwa ambayo amefikia Zungu ana imani atafanya vyema kazi kutokana na uzoefu aliokuwa nao.
“Mwanzo alikuwa Naibu Spika alifanya kazi vizuri na kuaminiwa, hivi sasa ni Spika wa Bunge nina imani ataendelea kufanya kazi kwa umakini na kusimamia bunge vizuri,” alisema Mongella.




