Na SELINA MATHEW,
Dodoma
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuhusu ushindani mkubwa uliopitiwa katika mchakato wa uteuzi wa Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba.
Pia, amempa maagizo matatu yenye lengo la kuimarisha zaidi utendaji kazi wa serikali.
Amesema uteuzi wa Dk. Mwigulu, umepitia mchakato mrefu huku akimtaka kiongozi huyo, kusimamia mapato, uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kudhibiti makundi.
Hayo aliyasema jijini hapa katika hafla ya kumwapisha Dk. Nchemba, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
“Dk. Mwigulu uteuzi wako umepitia ushindani mkubwa na katika vigezo kadhaa, umeibuka kuwa na sifa nyingi kidogo kuliko wengine ulioshindana nao.
“Vigezo vyote ulivyopimwa, tumepima maeneo mbalimbali ya kuitumikia nchi hii na taifa hili, kubwa zaidi, kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Alisema kazi zake na maelekezo yote, yapo katika katiba, lakini amemkabidhi vitabu vinavyoeleza majukumu na mambo yote anayotakiwa kuyaangalia.
“Umepokea kijiti kutoka kwa Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa, ambaye amefanya kazi nzuri kufanikisha tunayotamba nayo leo.
“Tukitamba na ujenzi wa shule, vituo vya afya, hospitali za kanda za rufaa, kila tunachotamba nacho leo, yeye alikuwa nyuma yangu kuhakikisha yanakwenda vizuri.
“Kwa hiyo, umepokea kijiti kutoka kwa mfanyakazi mzuri, sina shaka utafuata majukumu yake na kutengeneza pale unapohisi panahitajika kuongezwa nguvu,” alisema.
Alimpongeza na kumtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake mapya, huku akimtaka kwenda kusimamia utekekezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2025-2030.
“Tuna Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030, kuna mengi tumeahidi kuwafanyia wananchi, ukiangalia mambo yote na muda tulionao ni finyu, hivyo hatuna budi kuongeza kasi katika utendaji wetu.
“Wewe utakwenda kusimamia mawaziri ambao nao wanaongoza sekta tofauti, ni wajibu wako kuhakikisha kasi ya utekelezaji wa yale tuliyopanga, inaongezwa tuweze kuyatimiza ndani ya muda mfupi,” alieleza.
Alisema utekelezaji wa kazi hizo zote unahitaji fedha na kwa kuwa ametoka sekta ya fedha kwa muda wa miaka mitano anajua vichochoro vyote vya kutafuta fedha, hivyo amsimamie atakayekaa katika nafasi aliyotoka kupita njia aliyopita ili fedha ipatikane na kazi ifanyike.
“Kwa ufupi una kazi kubwa sana, leo (jana), nitalifungua Bunge la 13 ambapo nitaeleza yote tunayotakiwa kuyafanya ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano.
“Kuna ambayo umesema juzi bungeni, naamini hukuyasema tu, una moyo wa dhati kuyasimamia.
“Mzigo huu siyo mdogo na kwa umri wako, vishawishi ni vingi vya marafiki, ndugu, jamaa na wengine, nafasi yako haina rafiki, ndugu wala jamaa ni nafasi ya kulitumikia taifa hili,”alisisitiza Dk. Samia.




