Na NJUMAI NGOTA,
Rukwa
MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema CCM ni Chama pekee chenye dhima ya kuwatumikia Watanzania, kwa kuwa, kimejengwa katika misingi ya uadilifu, utekelezaji wa sera, ahadi na dhamira ya dhati ya kujenga maisha bora kwa kila Mtanzania.
Pia, Chama kimetekeleza kwa vitendo, Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 kwa mafanikio makubwa mkoani Rukwa, huku akitaja miradi ya kimkakati iliyoleta mageuzi kwa maisha ya wananchi.
Balozi Dk. Nchimbi, alisema hayo Sumbawanga Mjini, mkoani Rukwa, , alipohutubia mamia ya wananchi, waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama, kuelezea utekelezaji wa Ilani na kuwaombea kura wagombea wanaotokana na CCM, akiwemo Dk. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema wananchi wa Rukwa, wameonesha imani kubwa kwa CCM na uongozi wa Rais Dk. Samia, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa kipindi cha miaka minne na nusu iliyopita.
“Tunaona fahari kukitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimejikita katika dhamira ya kuwatumikia Watanzania, Chama ambacho muundo, sera na utekelezaji wake, umejielekeza katika nia ya kutoa utumishi uliotukuka kwa Watanzania.
“Chama ambacho muda wote, kinatoa Ilani kwa watu wake, kinaitekeleza, kinaipima na kinatoa Ilani mpya, ambayo inaendeleza mazuri yaliyofanywa katika awamu inayopita.
“Kama wenzangu walivyosema, Chama chetu tangu kuasisiwa kwake, kilikuwa na mifumo inayohitaji kutanguliza mbele maslahi ya watu. Ndiyo maana miradi yote mikubwa katika nchi yetu, imetekelezwa katika kumhudumia mwananchi wa kawaida.
“Hakuna nchi nyingine yoyote inayozungumzia maeneo muhimu ya sekta ya afya, elimu. Isipokuwa kama mna Chama na serikali inayojali maisha ya watu,”alisema.
Aliongeza kuwa, Chama na serikali, vina wajibu wa kuwatumikia Watanzania kupitia viongozi wa CCM.
Pia, alisema iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi, watajielekeza katika matumizi endelevu ya ardhi, ndiyo maana kila sehemu kuna utaratibu unafanyika ikiwemo kupimwa, kugawanywa huku wakijali vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo.
Alisema Dk. Samia miaka minne na nusu iliyopita, alitoa vipaumbele muhimu yeye na Chama katika mambo ya msingi.
Aidha, Balozi Dk. Nchimbi, alisema Dk. Samia, alijelekeza katika afya za Watanzania kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya afya inayostahili.
Vilevile katika miaka mitano iliyopita, serikali ya CCM ilijielekeza kukuza kilimo, viwanda, ufugaji na kukuza uvuvi.
“Haya ni mambo ambayo yamegusa wananchi wetu,” alisema.
Balozi Dk. Nchimbi, alisema serikali chini ya uongozi wa Dk. Samia, Ilani imetekelezwa kwa mafanikio makubwa mkoani Rukwa.
Alisema ushahidi wa mafanikio hayo, unaonekana katika sekta za afya, elimu, barabara, maji na ajira kwa vijana kupitia miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya mtu moja kwa moja.
“Nitakwenda kumwambia Dk. Samia kuwa, wananchi wa Sumbawanga wameniambia nikuambie kura zako na za CCM ni za kishindo,”alisema.
Alitaja mambo yaliyotekelezwa katika Ilani hiyo ni kuongezeka kwa barabara za kiwango cha lami ikiwemo ya Matai -Kalambo.
Pia, alisema Bandari ya Kasanga imefanyiwa uboreshaji kwa viwango vya kisasa, kilometa za lami Sumbawanga Mjini zimeongezeka kutoka 29.2 hadi 46.7, hospitali za halmashauri zimeongezeka kutoka 17 hadi 20.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa vituo vya afya kutoka viwili hadi sita, wataalamu wa afya kutoka 206 hadi 450, Shule za msingi 58 hadi 62, fedha za elimu zimeongezeka kutoka sh. bilioni 3.6 hadi sh. bilioni tisa, maji safi mijini yameongezeka kutoka asilimia 86 hadi 95, vijijini kutoka asilimia 57 hadi 79.
Ilani Mpya 2025-2030
Alielezea vipaumbele vya CCM katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030 kuwa, mpango wa Serikali ijayo ya CCM kuongeza kasi ya maendeleo mkoani Rukwa na maeneo mengine ya nchi kwa kujikita katika huduma za jamii, sekta za uzalishaji na viwanda.
Katika sekta ya afya, alisema vituo vipya vya afya vitatu vitajengwa, zahanati mpya nane kuanzishwa, magari ya wagonjwa matano.
Aidha, Balozi Dk. Nchimbi alisema wamekusudia kujenga shule mpya za sekondari mbili za msingi nane madarasa 188 mapya.
Katika kuendeleza sekta ya uzalishaji mali, Balozi Dk. Nchimbi alisema skimu mpya za umwagiliaji tatu zitaanzishwa, mabwawa mapya ya uvuvi 220 kuchimbwa, vizimba vya uvuvi 30 kuanzishwa kuongeza tija na ajira kwa wavuvi.
Aliwaomba wanaRukwa kumpigia kura Dk. Samia, wabunge na madiwani kwa kuwapa kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu.
Akiwa katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama uliofanyika Majimoto, mkoani Katavi, Balozi Dk. nchimbi alisema katika miaka mitano ijayo watahakikisha vitongoji vyote 97 ambavyo havijapitiwa na umeme vitafikiwa.
Pia, alisema wanakusudia kuboresha maeneo ya barabara za ndani za mji kwa kuongeza kilometa mpya 10 na za changarawe kilometa 204.
Alisema katika kuboresha kilimo, wamedhamiria kuongeza skimu za umwagiliaji tano na kuimarisha miundombinu ya mifugo ikiwemo kuanzisha minada mipya Majimoto.




