Na MWANDISHI WETU
BAO pekee la Allan Okello limeifanya Yanga kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Hilo ni bao la tatu kwa Okello tangu alipotambulishwa Yanga, Januari 13, mwaka huu, akianza kufunga dhidi ya Singida Black Stars kisha katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons kabla ya jana kufunga bao la ushindi dhidi ya KMC.
Katika mechi ya awali iliyozikutanisha Yanga na KMC, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-1, katika mechi iliyopigwa dimba la Benjamin Mkapa.
Ushindi huo, umeiwezesha Yanga yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam kufikisha pointi 51, ikiwa kileleni mwa msimamo huku KMC ikiendelea kuburuza mkia ikiwa na alama tisa baada ya timu zote kushuka dimbani mara 21.
Katika mechi hiyo, mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu na kutafuta ushindi, dakika ya 10 Prince Dube alipata nafasi ya kufunga lakini shuti alilopiga liliishia mikononi mwa kipa wa KMC, Ismail Mpank.
Yanga iliendelea kufanya mashambulizi na dakika ya 25, mchezaji Maxi Nzengeli alishindwa kufunga baada ya kupiga shuti kali lakini mpira ulipaa angani.
Yanga iliyokuwa ikihitaji ushindi wa hali na mali iliendelea kucheza kwa kasi na kutafuta alama tatu muhimu kabla ya dakika ya 37 Laurindo Dilson ‘Depu’ kupiga shuti kali na mpira kutoka nje, Depu alimalizia pasi safi kutoka kwa Dube.
Dakika ya 51, Yanga ilipata nafasi nyingine kupitia kwa Okello baada ya kupiga shuti kali na mpira kupaa angani, Okello alimalizia pasi safi kutoka kwa Duke Abuya.
Mashambulizi yaliyofanywa na Yanga yaliiwezesha timu hiyo kuandika bao la kuongoza dakika ya 65 baada ya Okello kupiga shuti kali na mpira kujaa kambani baada ya kumalizia pasi safi kutoka kwa Shekhan Ibrahim.
KMC nayo ilijibu shambulizi dakika ya 89 baada ya mchezaji wake Darueshi Saliboko kupiga shuti kali na mpira kutoka nje kabla ya
Yanga kujibu mapigo dakika ya 90 wakati Dube akimalizia pasi safi kutoka kwa Emmanuel Mwanengo.
KMC: Ismail Mpank, Juma Shemvuni, Nikson Mosha, Ken Ally, Samson Mwaituka, Redrmtus Mussa, Erick Mwijage, Mudathir Nassor, Kelvin Tondi, Darueshi Saliboko na Oscar Paulo.
Yanga: Djigui Diarra, Frank Assik, Ibrahim Abdullah, Maxi Nzengeli, Laurindo Dilson, Chadrack Boka, Allan Okello, Aziz Andambwile, Prince Dube, Koussi Yao na Duke Abuya.
Wakati huo huo, uongozi wa klabu ya Yanga umemfuta kazi kocha mkuu wa timu hiyo, Pedro Goncalves.
Taarifa iliyotolewa jana, imeeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo unamshukuru kocha huyo kwa mchango wake alioutoa ndani ya klabu hiyo na unamtakia kheri.
Taarifa imesema timu hiyo itakuwa chini ya kocha Abdihamid Moalin na kocha Patrick Mabedi hadi mwisho wa msimu.



