• ePaper
Friday, May 8, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

RAIS DK. SAMIA ATIA NENO BEI MAFUTA

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
May 8, 2026
in Habari, Kitaifa
0
RAIS DK. SAMIA ATIA NENO BEI MAFUTA
0
SHARES
5
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na MUSSA YUSUPH, Dodoma

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kudhibiti upandaji wa bei ya mafuta nchini.

Alisema miongoni mwa hatua ambazo serikali imechukua ni kutoa ruzuku kwa waagizaji wa mafuta, lengo ni kusaidia mafuta kutopanda bei maradufu.

Aidha, Rais Dk. Samia, alitoa wito kwa vijana kutokubali kushawishiwa kuharibu usalama wa nchi, kwa kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana, hayapaswi kujirudia.

Pia, aliwasisitiza vijana kulindana kuhakikisha hakuna mtu atakayetumika kuvuruga amani iliyopo.

Rais Dk. Samia aliyasema hayo kwa nyakati tofauti, ambapo awali alizungumza katika mkutano wa kawaida wa Shina Namba 1 la CCM, Tawi la Chamwino, Kata ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.

Alisema serikali imeendelea kutoa ruzuku katika mbolea na pembejeo za wakulima.

“Lakini lingine mfano uliopo sasa hivi, duniani huko watu wanapigana na kusababisha mafuta kupanda bei. Mafuta yakipanda bei kila kitu kitapanda bei. Kazi ya serikali ni kutoa ruzuku kwa wanaoleta mafuta kushusha bei ili wananchi wapate manufaa na vitu visipande bei kwa kasi kubwa.

Alieleza: “Hiyo ndiyo kazi ya serikali iliyowekwa na Chama Cha Mapinduzi, kwa hiyo yale yote yanayofanywa na serikali yanafanywa na Chama Cha Mapinduzi.”

WITO KWA WANACHAMA

Rais Dk. Samia alisema msingi wa uimara wa CCM ni kuzingatia kanuni kama zinavyoelekezwa na Katiba ya Chama.

Aidha, Rais Dk. Samia alisisitiza umoja na mshikamano ndani ya CCM ni suala muhimu na linapaswa kupewa kipaumbele, hususan wakati huu Chama kinapoelekea katika uchaguzi mkuu wa ndani, utakaofanyika mwakani.

“Mwenyekiti nisisitize tu, umoja na mshikamano ndani ya chama chetu. Wakati tunapoingia kwenye chaguzi zetu, wengi tunatamani kushika nafasi mbalimbali kuanzia ngazi ya shina, ngazi ya tawi na ngazi za juu.

“Nitazungumzia hapa kwenye shina langu. Mwaka ujao tunaenda tena kwenye uchaguzi. Niombe sana umoja na mshikamano ndani ya Chama. Wanasema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,” alisema Rais Dk. Samia.

Akiendelea kusisitiza jambo hilo, Rais Dk. Samia alisema msingi imara wa kudumisha umoja na mshikamano ndani ya Chama kuanzia ngazi ya shina hadi taifa ni kuzingatia kanuni mbalimbali zinazohusika kuendesha shughuli na utendaji wa Chama. 

Aliwasisitiza wanaCCM katika ngazi zote kutoruhusu utengano na migawanyiko ndani ya chama kwa sababu itatoa mwanya kwa maadui kupita.

“Niombe sana umoja na mshikamano ndani ya Chama chetu. Lakini Umoja na mshikamano unakujaje? Tukifuata kanuni za Chama chetu, kama tulivyowekewa kwenye Katiba yetu.

“Tukifuata kanuni zile hakuna haja ya kugawana wala kutengana. Kwa hiyo ndugu Mwenyekiti, mimi nimalizie kwa kusisitiza tena uhai wa Chama, lakini umoja mshikamano ndani ya Chama chetu,” alisema Rais  Dk. Samia.

Rais Dk. Samia alihudhuria mkutano huo wa kawaida ulioitishwa na Mwenyekiti wa Shina la CCM Namba 1, Paulina Mkasanga, akiwa ni mmoja wa wajumbe wa shina hilo lililoko wilayani Chamwino, ambako pia ni makazi yake.

WITO WA AMANI

Akizungumza na mamia ya wananchi wakiwemo waendesha bodaboda, wafanyabiashara wadogo maarufu machinga, mama na baba lishe kando mwa barabara ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Rais Dk. Samia alisisitiza amani ya nchi inapaswa kuendelea kulindwa.

Rais Dk. Samia alitoa wito kwa vijana kutokubali kushawishiwa kuharibu usalama wa nchi, kwa kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana, hayapaswi kujirudia.

Rais Dk. Samia alisisitiza vijana wanapaswa kulindana kuhakikisha hakuna mtu atayaketumika kuvuruga amani.

“Nimemaliza kazi zangu nilikuwa narudi Dar es Salaam, sikujua kama nitawakuta hapa vijana wangu wa Dodoma. Nilipoona watu wamesimama nikawa najiuliza kuna nini?. Lakini nikaona kuna fulana zimevaliwa zikiandika ‘Never Again’ (Yasijirudie) na bendera ya Tanzania,” alieleza.

Rais Dk. Samia alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kutoa ufafanuzi wa kile kilichoandikwa katika fulana za vijana, ambapo alieleza maandishi hayo yanamaana vijana wa Dodoma hawataki tena yaliyotokea huko nyuma (Oktoba 29, 2025) wao ni wazalendo na wanalipenda taifa lao.

“Vijana wa Dodoma ni wasomi, wakasema wakuambie hawataki tena yaliyotokea huko nyuma. Wao ni wazalendo, wana utu, wanaijali nchi yao na wanaithamini,” alieleza Senyamule.

Baada ya ufafanuzi huo, Rais Dk. Samia aliwapongeza vijana hao kuendelea kuthamini na kuilinda amani ya nchi.

“Vijana wangu nimepokea ujumbe wenu na niwaombe kama kweli mmekusudia kuwa haitajirudia tena kama fulana zenu zilivyoandikwa, hakikisheni mnalindana wenyewe. Msikubali kutiwa maneno kuharibu usalama wa nchi yetu.

“Lililotokea nyuma halikuwa jema kwa yeyote na mtego ule ulihusisha watu waliokuwemo na wasiokuwemo. Kama mnakumbuka kumbo lile lilikumba vijana wengi ambao asilimia kubwa walifuata mkumbo, lakini walipokamatwa kama mama nikasema waachieni, watajifunza kwa sababu waliona yaliyotokea,” alisema.

Rais Dk. Samia aliwaeleza vijana hao umuhimu wa kuendelea kuhubiri amani na utulivu nchini, wanapokutana kwa kuwa matukio ya Oktoba 29, mwaka jana yalichafua taswira ya nchi.

“Niwaombe vijana katika vijiwe vyenu, kazi zenu, ambianeni yasitokee tena kwani yaliyotokea yametia doa taifa letu. Tanzania ni nchi ya amani, hayajawahi kutokea yale, hivyo yalipotokea yalisababisha doa. Tuonyeshe ulimwengu kuwa yaliyotokea sio ya Kitanzania bali ni mambo ya kupandikizwa. Nashukuru mmesema haitajirudia tena,” alisema.

MAKUNDI YA WAJASIRIAMALI
Baada ya hotuba yake, Rais Dk. Samia, alitoa fursa kwa wawakilishi wa makundi ya mama na babalishe, bodaboda na machinga kuwasilisha ujumbe wao.

Mwenyekiti wa Mama na Babalishe Mkoa wa Dodoma, Ester Mwansasu, alisema kundi hilo linaendelea kumuunga mkono Rais Dk. Samia kwa kuwa amewawezesha kupata mikopo iliyowanyanyua kibiashara.

“Tunashukuru kwa mikopo ambayo umetuletea ambayo haina riba, ila muhimu tunaomba masharti yapunguzwe ili watu wengi wanufaike,” alieleza.

Mwenyekiti wa Machinga Dodoma, Christian Msumari, alimpongeza Rais Dk. Samia kuunda Tume kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana.

Pia, alimshukuru kwa ujenzi wa masoko mbalimbali ya wajasiriamali hao likiwemo Soko Kuu la Machinga ambalo limegharimu sh. bilioni tisa.

Hata hivyo, alimwomba Rais Dk. Samia kuuagiza uongozi wa mkoa huo kuhakikisha wafanyabiashara walioondoka katika soko hilo kwenda mitaani, wanarudishwa kuendelea na biashara zao katika eneo rasmi.

Previous Post

YANGA MBELE KWA MBELE

Next Post

MWIGULU ATAJA MWAROBAINI MAFURIKO DARAJA LA DUMILA

Next Post
MWIGULU ATAJA MWAROBAINI MAFURIKO DARAJA LA DUMILA

MWIGULU ATAJA MWAROBAINI MAFURIKO DARAJA LA DUMILA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

DK.NCHIMBI AMTAJA ASKOFU MFUMBUSA NGUZO YA UMOJA

DK.NCHIMBI AMTAJA ASKOFU MFUMBUSA NGUZO YA UMOJA

2 weeks ago
MRADI WA BILIONI 18.9/- BUKOBA WAMPA SIFA RAIS DK. SAMIA

MRADI WA BILIONI 18.9/- BUKOBA WAMPA SIFA RAIS DK. SAMIA

1 month ago

Popular News

  • MWIGULU ATAJA MWAROBAINI MAFURIKO DARAJA LA DUMILA

    MWIGULU ATAJA MWAROBAINI MAFURIKO DARAJA LA DUMILA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. SAMIA ATIA NENO BEI MAFUTA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • YANGA MBELE KWA MBELE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • WATAALAMU WAFUNGUKA MITAZAMO YA MIKATABA 8

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. SAMIA AKEMEA VIONGOZI ‘KUVIMBA’

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?