Na MWANDISHI WETU
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Dk. Mahimbo Mndolwa, amesema Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, itaipeleka nchi pazuri.
Kauli hiyo aliyoitoa Dar es Salaam, imekuja kipindi ambacho Tume ya Kuchunguza Matukio Kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu, ikiendelea na kazi zake katika hatua ya mwisho.
Askofu huyo Mkuu wa Kanisa Anglikana, Dk. Mndolwa, alisema Tume hiyo imeonesha mwanga kuwa tunakwenda mahali sahihi.
Dk. Mndolwa alifafanua katika vikao vyake vya Umoja wa Mataifa, amekuwa akieleza Tanzania haijafikia hatua ya kuomba nguvu za nje katika kutatua matatizo yake, kwa kuwa imekuwa ikichukua hatua.
“Ukweli kwa aina ya watu tulio nao mle ndani ya Tume, tunaamini tunaelekea mahali sahihi na kujenga taifa sahihi zaidi,” alisema Askofu Dk. Mndolwa.
Alisema, hata katika maandiko ya Mungu yanasisitiza umuhimu wa ndugu kutatua matatizo yao wenyewe kwanza kabla ya kueleza au kutafuta suluhu kwa watu wa nje.
Akifafanua mantiki ya maandiko hayo akihusisha na Tume, Askofu Dk. Mndolwa alisema hatua ya Tanzania kufanya uchunguzi ni uthibitisho kuwa Tanzania imeamua kutafuta ufumbuzi wa matatizo yake ya ndani yenyewe.
“Ukweli, hata katika maandiko ya dini tunaelezwa ndugu yako akikukosea unakwenda kuzungumza naye. Kama hakukusikia ndipo utaenda kueleza Kanisa, ” alifafanua Askofu Dk. Mndolwa.
Alisema hatua ya Tanzania kujichunguza imeonyesha ukomavu mkubwa, ambao umekuwa ukifanyika kwa nyakati tofauti na kwa miaka mingi.
“Tumefanya hivi kwa miaka mingi sana. Hatukwenda huko nje kupiga parapanda. Tutapiga parapanda tutakapoona tumeshindwa,” alisema.
Dk. Mndolwa alisema hatua hiyo pia inaonesha Tanzania ni huru huku akisisitiza, inapokea maoni kutoka nje lakini haiwezi kuyakimbilia.
“Mawazo kutoka nje tutayasikiliza ila hatuwezi kuyakimbilia. Mimi mwenyewe ni mjumbe wa Kanisa Anglikana katika UN, wanatuuliza ninyi Watanzania mbona hamtukaribishi. Tuna wajibu bado tunaweza kuongea wenyewe,” alisisitiza.
Dk. Mndolwa alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuunda Tume hiyo chini ya Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande, itafute kwanza suluhu ya ndani.
Dk. Mndolwa alisema Tume huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Vurugu zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka jana inaonesha mwanga kuwa tunakwenda mahali sahihi.




