Na JOE NAKAJUMO
MOJA ya malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni Tanzania kuwa mzalishaji mkuu wa chakula Afrika na kuwa miongoni mwa nchi 10 bora katika uzalishaji wa chakula.
Kwa miaka kadhaa mfululizo, uzalishaji wa mazao ya chakula umekuwa ukiongezeka. Tani milioni 18 za mazao ya chakula zilizalishwa mwaka 2020/2021 na ziliongezeka hadi tani milioni 22 mwaka 2023/2024.
UTOSHELEVU WA CHAKULA
Ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula, kunaifanya Tanzania kuwa na utoshelevu wa chakula. Kiwango cha utosholevu kiliongezeka kutoka asilimia 114 hadi 128 kwa mwaka 2024/2025.
Hii inamaanisha Tanzania ina ziada ya chakula na hailazimiki kuagiza chakula kutoka nje. Kwa takwimu za mwaka 2024, Tanzania ilikuwa inajitegemea kwa chakula kwa asilimia 120 na asilimia 20 ilikuwa inauzwa nje ya nchi. Chakula kinachouzwa nje ni mahindi na mchele.
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kwa takwimu za Mei mwaka jana 2025, ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 776,000 za chakula. Lengo ni kufikia tani milioni tatu ifikapo mwaka 2030.
Serikali inasema Dira ya 2050 imebainisha Tanzania kuwa ghala la chakula barani Afrika ifikapo mwaka 2050. Hii itafanyika kupitia utekelezaji wa kilimo cha kisasa na kidijitali.
Utekelezaji wa maendeleo ya Taifa chini ya Dira ya 2050, utafanyika kwa ushirikiano wa pande tatu. Serikali itachukua sehemu ya utekelezaji kwa asilimia 30, sekta binafsi itapewa jukumu kubwa zaidi katika utekelezaji kwa asilimia 70, mashirika ya umma nayo yatakuwa sehemu ya mchakato kwa asiilimia 8 kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi.
Dira ya 2050, ilianza kutekelezwa Julai Mosi, 2026 na itaendelea na malengo yake kwa kipindi cha miaka 25 ijayo. Ingawa yapo mafanikio makubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na kuifanya nchi kuwa na utoshelevu, bado kuna eneo ambalo kwa miaka mingi lina upungufu.
Mafuta ya kupikia ni bidhaa ambayo imekuwa na upungufu kwa miaka mingi. Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na viongozi wa serikali tangu awamu ya kwanza kwa kuhimiza kilimo cha mbegu za kuzalisha mafuta ya kula.
MAELEKEZO YA NYERERE
Rais wa serikali ya awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, katika ziara zake mikoani aliwahimiza wananchi kulima mazao ya mbegu za kuchakata mafuta ya kula. Septemba 2, 1976, alitoa wito kwa wakulima kupanua kilimo cha mazao ya mbegu za mafuta kukabili upungufu wa mafuta ya kupikia.
Mwalimu Nyerere alisema mazao ya mbegu za mafuta ya chakula kama vile karanga, ufuta, nyonyo, alizeti na mengineyo yanahitajika kulimwa kwa wingi kwa mahitaji yetu wenyewe.
Alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Endakiso, wilayani Hanang, wakati ikiwa katika mkoa wa Arusha.
Mwalimu Nyerere alisema serikali inafanya mpango wa kupandisha bei ya mazao hayo kwa wakulima kwa kuwa hayatauzwa nchi za nje ambapo bei hupangwa na wanunuzi, bali yatanunuliwa nchini na kutunufaisha wenyewe.
NUSU KARNE
Sasa ni nusu karne yaani miaka 50 tangu Baba wa Taifa alipohimiza kilimo cha mazao ya mbegu za mafuta. Lakini bado nchi inaupungufu na serikali inalazimika kutumia fedha za kigeni kuagiza kutoka nje.
Kwa mfano, mahitaji ya mafuta ya kula Tanzania kwa mwaka 2021, yalikuwa ni tani 570,000. Kiasi kilichozalishwa kilikuwa tani 205,000 na kuwepo upungufu wa tani 365,000 hadi 400,000 ambazo ziliagizwa kutoka nje kwa gharama ya sh. milioni 474.
MIKOA 14
Tanzania kuna mikoa 14 inayolima alizeti. Mwezi Juni 2021, ulifanyika mkutano wa kampeni ya kitaifa mkoani Singida kuzungumzia mikakati ya kuongeza kilimo cha alizeti, nchi ipate mafuta ya kula ya kutosha. Takwimu zilionesha tani milioni 1.6 za alizeti zinahitajika kupata mafuta tani 450,000.
Pamoja na alizeti, kuna mbegu za mafuta zinazopatikana kutoka mazao ya karanga, pamba, chikichi (mawese) na mbata inayotokana na nazi.
Mazao hayo yanapatikana kwa wingi katika mikoa kadhaa. Ufuta unapatikana Lindi na Mtwara, Chikichi (Kigoma), pamba huzalishwa zaidi mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Mara. Mbata zinapatikana katika ukanda wa pwani, Lindi, Mafia na Tanga.
Hivyo karibu kila mkoa wa Tanzania unaweza kuzalisha zao moja la mbegu za mafuta na nchi ikajitosheleza.
Gazeti moja katika toleo lake la Juni 22, 2021, lilimnukuu Mzee Samwel Kasori, aliyekuwa Katibu wa Mwalimu Nyerere akisema, ni kujiabisha Tanzania kushindwa kujilisha kwa mafuta ya kula.
TAMKO LA WAZIRI CHONGOLO
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai 2026, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo alinukuliwa akisema: “Tanzania haina sababu ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje. Ardhi na maji tunavyo, taasisi zinazosimamia uzalishaji tunazo, sekta binafsi zenye uwezo tunazo na wakulima wenye ari na nia tunao. Kilichobaki ni kuongeza kasi ya uwekezaji, kuimarisha ushirikiano na kutekeleza kwa vitendo mikakati tuliyojiwekea.”
Waziri Chongolo aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Tasnia ya Mafuta mjini Dodoma na kwamba serikali imebadili mwelekeo kutoka nchi inayotegemea uagizaji wa bidhaa kuwa Taifa la uzalishaji. Kwenye mkutano huo serikali ilitangaza mkakati mpya wa kuongeza uzalishaji mafuta ya kula.
WAWEKEZAJI
Kwa kuzingatia mkakati huo, serikali haitaruhusu wawekezaji kuendelea kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi bila kuonesha kiasi walichowekeza katika uzalishaji wa mafuta ya kula.
“Miaka miwili ijayo ili uruhusiwe kuagiza mafuta ya kula kutoka nje, lazima utuonyeshe umewekeza katika uzalishaji wa ndani. Baada ya miaka minne, lazima uwe tayari umefanya uwekezaji na kuanza kuzalisha,” alisisitiza Waziri Chongolo.
Alisema kuendelea kutegemea mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, kunaiweka Tanzania katika hatari ya kukumbwa na uhaba wa bidhaa hiyo kunapotokea misukosuko ya kiuchumi au kisiasa duniani.
“Lazima tubadilike kutoka nchi ya wachuuzi na kuwa nchi ya wazalishaji. Huo ndiyo mwelekeo wa serikali katika kujenga uchumi imara wenye ushindani,”alifafanua.
UPUNGUFU
Takwimu zilizotolewa kwenye mkutano huo, zilionesha mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 732,974 kwa mwaka, wakati uzalishaji ni tani 305,906.
Upungufu ni tani 427,068, sawa na asilimia 58.3 ya mahitaji ya Taifa. Kutokana na upungufu serikali inatumia dola milioni 200 kila mwaka kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.
Mahitaji ya mafuta ya kula yanaongezeka karibu kila mwaka. Kwa mfano takwimu za Novemba 2022, zilionesha mahitaji nchini yalikuwa tani 650,000 na uzalishaji ulikuwa tani 290,000 na serikali ililazimika kutumia sh. milioni 471 kwa mwaka kuagiza kutoka nje.
Agosti 2023, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji, alisema kwa wakati huo,Tanzania ilikuwa na viwanda 771 vya mafuta ya kula. Alisema serikali ilikuwa ikiagiza zaidi ya asilimia 60 ya mafuta ya kula kutoka nje.
(Mawasiliano na Mwandishi WhatsApp 0784291434; email nakajumoj@gmail.com)



