Na MWANDISHI WETU
TANZANIA imetoa wito wa kuimarishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN) na ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia, ikiwamo migogoro, mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usalama na changamoto za maendeleo.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais Deogratius John Ndejembi, akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Mjadala wa Jumla wa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81), jijini New York, Septemba 22, 2026.
Akizungumzia maendeleo, Ndejembi amesema Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050 na Ajenda ya 2030 kwa kuwekeza katika watu, miundombinu, teknolojia na ubunifu.
Pia, ameomba kuboreshwa kwa mfumo wa fedha wa kimataifa ili nchi zinazoendelea ziweze kupata mikopo nafuu kwa ajili ya maendeleo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Katika sekta ya afya, Ndejembi amesema Tanzania imeongeza kiwango cha uzazi katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza ajenda ya Sifuri Tatu inayolenga kuondoa vifo vya mama na watoto vinavyoweza kuzuilika, kujifungua majumbani na watoto kutopata chanjo.
Kuhusu amani na usalama, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na utatuzi wa migogoro kwa njia za amani.
Aidha, Ndejembi ametangaza azma ya Tanzania kugombea kiti kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, huku ikiendelea kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili kuhusu Israel na Palestina.
Rais wa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Khalilur Rahman, amesisitiza umuhimu wa kurejesha imani katika Umoja wa Mataifa kupitia hatua za vitendo, mageuzi na ushirikishwaji mpana. Amesema taasisi hiyo inapaswa kuimarisha utii wa sheria za kimataifa, ulinzi wa raia na utoaji wa misaada ya kibinadamu, pamoja na kuhakikisha uwakilishi wa Afrika katika vyombo vya maamuzi.



