Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nishati, Dk. Juma Homera, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha Kampeni ya “Washa Umeme Vitongojini” inazinduliwa katika kila mkoa nchini, kwa lengo la kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Amesema katika kila mkoa, Meneja wa REA anapaswa kuandaa uzinduzi wa kampeni hiyo utakaoongozwa na Mkuu wa Mkoa husika, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme na kuhakikisha vitongoji vyote vinapata huduma hiyo ifikapo mwaka 2030.
Homera ametoa agizo hilo leo, Oktoba 25, 2026, akiunganisha umeme katika Kitongoji cha Lindi B, Kijiji cha Kumbara, Kata ya Litola, Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Amesema jumla ya Shilingi milioni 95.4 zimetumika kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika kitongoji hicho, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Akizungumzia hali ya usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Namtumbo, Homera amesema wilaya hiyo ina jumla ya vitongoji 424, ambapo zaidi ya vitongoji 300 tayari vimepata umeme, vitongoji 72 viko katika mpango wa kuunganishiwa umeme, huku vitongoji 38 pekee vikiwa vimesalia.
Amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030, huku kampeni hiyo ikilenga kuimarisha uhamasishaji, uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya umeme katika ngazi ya mikoa na wilaya.




