Na ABDUL DUNIA
KWA mara ya pili mfululizo, timu ya soka ya Azam FC inaweka historia ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).
Azam FC ilitinga hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya Zed FC ya Misri, kufuatia jana kushinda 1-0 huku mchezo wa kwanza ukimalizika kwa sare ya bao 1-1 nchini Misri.
Azam FC inayonolewa na Kocha Florent Ibenge, ilitakata kwa asilimia kubwa katika mtanange huo wa hatua ya pili ya mtoano uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Iddy Seleman ‘Nado’ alifunga bao hilo dakika ya 63, akiuzungusha mpira kwa mguu wa kulia, baada ya kuwachambua mabeki wawili wa Zed FC, mchezaji huyo alipokea pasi hiyo kutoka kwa Paschal Msindo.
Tangu kuanza kwa mchezo huo, Azam FC ilikuwa katika kiwango cha juu, kuanzia safu ya ulinzi, kiungo hadi washambulliaji ambao walikuwa wakihaha mara kwa mara kuhakikisha bao linapatikana.
Kutokana na ushindi huo, sasa Azam FC ina uhakika wa kuvuna dola za Marekani 400,000 (sh. bilioni moja) hata kama haijaendelea hatua ya robo fainali.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kila timu itakayoishia makundi itavuna kiasi hicho cha fedha huku zitakazoishia robo fainali zikiweka kibindoni dola za Marekani 550,000 (sh. bilioni 1.4).
Pia, timu zitakazoishia nusu fainali zitaondoka na dola za Marekani 750,000 (sh. bilioni 1.979) huku itakayomaliza mshindi wa pili ikiondoka na dola za Marekani milioni moja (sh. bilioni 2.6).
Bingwa wa michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi za klabu Afrika, anatarajiwa kubeba dola za Marekani milioni 4 (sh. bilioni 10.5).




