Na NJUMAI NGOTA,
Bariadi
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unakamilika katika kipindi cha miaka mitano ijayo, iwapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchini.
Kimesema kitafanya hivyo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha demokrasia na haki sawa kwa Watanzania.
Pia, kimeahidi kuimarisha utawala bora, demokrasia nchini, kuhakikisha kila mwananchi anajishughulisha katika shughuli za kisiasa, kijamii na maendeleo ya taifa.
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema hayo, Dutwa, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, alipowahutubia mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM za kuwanadi wagombea.
Balozi Dk. Nchimbi amesema Chama kimedhamiria katika kipindi miaka mitano ijayo kuhuisha mchakato wa katiba mpya kuhakikisha inapatikana.
“Tutakamilisha mchakati huu wa Katiba mpya ambao umeshaanza na tutakuwa na Katiba yetu, jambo hilo litasimamiwa na CCM,” amesema.
AMANI, UTULIVU NA UMOJA
Pia, Balozi Dk. Nchimbi amesema katika miaka hiyo mitano Chama kimedhamiria kuendeleza, kuimarisha na kusimamia zaidi amani, utulivu na umoja wa nchi.
“Kwa kila Watanzania 100 walioulizwa kipaumbele chao cha kwanza ni nini, Watanzania 90 walisema amani, CCM inawahakikishieni kwamba suala la amani ndilo kipaumbele chake cha kwanza kabla ya vingine vyote, niwahakikishie hili tutalisimamia,” amesema.
UTAWALA BORA
Aidha, amesema katika kipindi hicho, Chama kimedhamiria kuimarisha utawala bora, kila mtu afuate sheria, azingatie sheria na haki sawa kwa kila Mtanzania.
“Isibague mkubwa na mdogo, tajiri na maskini, hiyo ni moja ya mipango ya Chama katika miaka mitano inayokuja,” amesema.
MAFANIKIO BARIADI
Balozi Dk. Nchimbi ametaja baadhi ya mambo yaliyotekelezwa wilayani humo chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia ni sekta ya afya ambapo hospitali mpya imejengwa Dutwa, zahanati zimeongezeka kutoka 26 hadi 39, vituo vya afya kutoka kimoja hadi vitatu, huku wataalamu wa afya wakiongezeka kutoka 38 hadi 301.
ELIMU
Amesema sekta ya elimu imeimarishwa kwa kujengwa shule mpya 29 za msingi, shule za sekondari zikiongezeka kutoka 24 hadi 32, madarasa kutoka 192 hadi 1,193 na mabweni kutoka matatu hadi 26.
HUDUMA YA MAJI
Mgombea huyo amesema upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 63 hadi 80 kupitia miradi 23 yenye thamani ya sh. bilioni 9.3, huku miradi saba ikiwa katika Kata ya Dutwa.
MIFUGO
Amesema miradi ya mifugo imeboreshwa kwa kuongeza majosho kutoka 12 hadi 21 na mabwawa kutoka 18 hadi 23, mtandao wa barabara umeongezeka kutoka kilometa 922 hadi 2,307 za changarawe na lami kutoka kilometa 17 hadi 27.
YATAKAYOTEKELEZWA 2025-2030
Balozi Dk. Nchimbi ametaja baadhi ya vipaumbele vitakavyotekelezwa wilayani humo ni pamoja na kujenga vituo viwili vipya vya afya, shule mpya 10 za sekondari, shule tano za msingi na madarasa 146.
Pia, amesema kupitia mradi wa maji wa Ziwa Victoria, upatikanaji wa maji Bariadi utaongezeka hadi kufikia asilimia 90.
KILIMO
Mgombea Mwenza huyo amesema Chama kimejipanga kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za ruzuku, mbegu bora na dawa za kilimo kwa kuongeza tija kwa wakulima.
NISHATI
Amesema serikali itamaliza tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kwa kuimarisha miundombinu ya kupoza nishati hiyo na kuhakikisha kinamama wanapata nishati safi.




