Na ZIANA BAKARI
BAADHI ya viongozi wa dini, wasomi na wadau mbalimbali, wamewashauri vijana kutumia vyema mitandao ya kijamii, kujiajiri na kuacha kuiga utamaduni wa kigeni.
Pia, wamezisihi taasisi za kielimu, kuendelea kuwaelimisha vijana kutumia vizuri mitandao ya kijamii, huku wazazi na walezi, wakishauriwa kuwalea watoto katika maadili mema yenye hofu ya Mwenyezi Mungu.
Wakizungumza na gazeti hili jana, kwa nyakati tofauti, viongozi hao na wadau mbalimbali, walisema ni vyema mitandao ya kijamii ikatumika vizuri, siyo kuharibu maadili yaliyopo nchini.
METHODIUS KILAINI
Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Methodius Kilaini, alisema siku zote, maadili yanajengwa kutokana na malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi.
“Mtu asipokuwa na maadili ni rahisi kuiga utamaduni wa kigeni kupitia mitandao ya kijamii, hivyo, niwasihi viongozi wenzangu wa dini, kuendelea kuwafundisha watoto misingi mizuri ya dini inayotakiwa,” alisema.
SHEIKH ZAIRAY HASSAN
Sheikh wa Wilaya ya Temeke, Zairay Hassan, aliwasihi wazazi na walezi, kuwa karibu na vijana wao na kuwafundisha namna nzuri ya utumiaji wa mitandao ya kijamii.
DK. PHILIP DANINGA
Mhadhiri wa Idara ya Uongozi, Maadili na Utawala wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Julius Nyerere, Dk. Philip Daninga, aliwashauri vijana kutumia vyema mitandao ya kijamii kwa kujiajiri.
Alisema hivi sasa fursa zipo nyingi katika mitandao ya kijamii, hivyo wanapaswa kuzingatia namna ya utumiaji huo unavyotakiwa.
“Natamani kuona vijana wakitumia mitandao ya kijamii muda mwingi kuangalia vitu vitakavyowasaidia kujikimu kimaisha na siyo vitakavyowapotezea muda, taasisi za kielimu ziendelee kuwaelimisha vijana namna ya utumiaji unavyotakiwa kwa kutengeneza fursa zao,”alisema.
GREYSON MWIKOLA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, wilayani Kigamboni, Greyson Mwikola, alisema suala la mmomonyoko wa maadili unatokana na namna ya mitandao ya kijamii inavyotumika.
Akizungumzia chimbuko la mmomonyoko wa maadili linapoanzia, alisema linatokana na utandawazi ambapo baadhi ya vijana hutumia kwa kuiga tamaduni za kigeni, ambazo siyo maadili ya taifa.
“Niishauri jamii kupenda maisha yetu halisi, tunajua simu zina mambo mengi, tunategemea kutengeneza vizazi vyenye maadili na kuja kuisimiamia vyema nchi yetu hivyo, wazazi na walezi wanapaswa kuwalea watoto katika maadili mazuri.
“Sisi kama Jumuiya kupitia CCM, wajibu wetu ni kupambana na kuhakikisha tunazungumza na vijana, watoto wetu kuwa maadili mema katika jamii,”alisema.
JANETH MAWINZA
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, alisema jamii inapaswa kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu ambayo itamsaidia mtu kuwa na tabia njema.
Alisema mtu yeyote akiwa na hofu ya Mwenyezi Mungu itamsaidia hata kuacha kuiga tabia zisizokuwa na maadili katika mitandao ya kijamii.