NA MUSSA YUSUPH,
Morogoro
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, amewahakikishia Watanzania kuwa chama hicho kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Mwenyekiti wa CCM na mgombea urais wetu alitupa maelekezo kuwa chama chetu kiwe mfano wa uendeshaji bora na wa kistaarabu katika kampeni hizi.
Napenda kuwahakikishia kwamba CCM tumejipanga kikamilifu kufanya kampeni za kistaarabu,” amesema Dk. Migiro.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Zuberi Mfaume, aliishukuru serikali kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), shule ya sekondari ya wasichana na kuboresha mawasiliano, hali iliyosaidia wananchi kuachana na tabia ya kupanda miti kutafuta mtandao wa simu.
Naye mgombea udiwani wa Kata ya Ngerengere, Kibena Nasoro, alishukuru serikali kwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa, huku akiomba baada ya uchaguzi serikali itoe fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha afya kitakachokidhi mahitaji ya sasa. Ombi hilo lilikubaliwa na mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisema amelipokea.