NA MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza neema kwa wakulima nchini baada ya kuahidi ujenzi wa vituo vya zana za kilimo vitakavyotoa huduma za ukodishaji kwa gharama nafuu.
Akizungumza (Agosti 29, 2025) katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Michezo Njia Nne, Tarafa na Kata ya Ngerengere, wilayani Morogoro, Dk. Samia amesema serikali itajenga vituo viwili vya ukodishaji zana za kilimo, ambapo wakulima watalipa nusu ya gharama zinazotozwa na watu binafsi kwa sasa.
Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto ya gharama kubwa za kukodisha matrekta na zana nyingine za kilimo.
Aidha, Dk. Samia ameahidi ujenzi wa maghala mawili ya kuhifadhia mazao, ikiwemo moja litakalojengwa katika kituo cha reli ya SGR kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ili kuimarisha ushoroba wa viwanda na kuchochea uchumi wa eneo hilo.
Akieleza utekelezaji wa miradi iliyokwisha kufanyika, alisema serikali tayari imejenga maghala matatu ya kuhifadhia chakula, kugawa bure miche 82,000 ya michikichi kwa wakulima, na kutoa pikipiki 68 kwa maofisa ugani na vipima udongo.
Kwa upande wa masoko ya mazao, alisema wakulima wa ufuta, mbaazi na korosho wamenufaika kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 11 zimeingizwa.
Katika sekta ya mifugo, Dk. Samia alisema wilaya hiyo itanufaika na ujenzi wa mashamba darasa 15 ya malisho na uzalishaji mifugo.
Vilevile, aliahidi mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 kwa wajasiriamali 7,015 kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Kuhusu upatikanaji wa nishati vijijini, alisema jumla ya vijiji 149 na vitongoji 417 tayari vimeunganishwa na umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
AHADI BARABARA YA BIGWA – KISAKI
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia alitoa ahadi kujengwa barabara ya Bigwa – Mvuha- Kisaki kwa kiwango cha lami kufuatia ombi la mgombe ubunge jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale maarufu kama Babu Tale.
Mgombea huyo alisema kwa sasa amepachikwa jina la Bigwa Kisaki kutokana na ujenzi wa barabara hiyo kutokamilika, hivyo alimuomba Rais Dk. Samia kujenga barabara hiyo yenye umuhimu kwa uchumi wa wakazi wa eneo hilo.
Kufuatia ombi hilo, Dk. Samia alisema serikali itahakikisha barabara hiyo itajengwa kwani ni muhimu kwa kuunganisha maeneo mbalimbali na makao makuu ya halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, aliwahakikishia Watanzania kwamba Chama kimejipanga kuhakikisha kinafanya kampeni za kistaarabu katika uchaguzi mkuu.
“Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na mgombea Urais wetu, ulitupa maelekezo CCM iwe mfano wa uendeshaji bora na kistaarabu katika kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka huu. Napenda kuhakikisha CCM tumejipanga kufanya kampeni za kistaarabu,” alieleza.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Zuberi Mfaume, aliishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya kimkakati iliyowanufaisha wananchi ikiwamo reli ya SGR, shule ya sekondari ya wasichana na kuimarisha mawasiliano hatua ambayo imewasaidia wananchi kutopanda juu ya miti kupata mawasiliano ya simu.
Mgombea udiwani, Kata ya Ngerengere, Kibena Nasoro, aliishukuru serikali kuwaletea miradi maendeleo huku akiioma serikali baada ya uchaguzi mkuu, iwaletee fedha kujenga kituo cha kikubwa afya kitakachokidhi mahitaji ya sasa, ombi ambalo Dk. Samia alilikubali.