Na NJUMAI NGOTA,
Mwanza
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Msigwa, amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amelifanya taifa liendelee kuwa na umoja, mshikamano, kufanya shughuli za maendeleo na ameonesha weledi mkubwa.
Pia, amesema Tanzania ipo salama katika mikono ya Chama na kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla kumpa kura za kishindo Mgombea Urais wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza wa Urais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, Tanzania izidi kusonga mbele.
Msigwa amebainisha hayo, alipozungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM zilizofanyika viwanja vya Furahisha, wilayani Nyamanga, mkoani Mwanza, ambazo Mgombea Mwenza wa Urais wa chama hicho, Balozi Dk. Nchimbi, alizindua kampeni hizo mkoani humo.
“Katika kipindi cha miaka minne tumeona utendaji wake mahiri kwa kulifanya taifa letu liendelee kuwa moja, kushikamana, kufanya shughuli za kimaendeleo, hakika Rais wetu ameonesha weledi mkubwa.
“Ukizungumzia amani, uvumilivu, maendeleo, maji, miundombinu, umeme, barabara, afya unamwona Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo mambo hayo yamefanyika katika kipindi kifupi,” alisema.
Msigwa amesema Tanzania iendelee kuwa na amani na utulivu, Rais Dk. Samia alimwona Balozi Dk. Nchimbi.
“Ukimwona Balozi Dk. Nchimbi unaona busara, weledi, hekima nchi yetu iendelee kusonga mbele inahitaji CCM, inamwitaji Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akisaidiana na Nchimbi katika kuleta maendeleo.
“ Ndugu zangu wa Mwanza, kwanini Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Nchimbi, Tanzania ipo salama katika mikono ya Chama. Nimetoka Iringa kushirikiana na wana-Mwanza na Watanzania tumuunge mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Nchimbi, Tanzania yetu izidi kusonga mbele,” amesema.
Msigwa aliongeza kuwa: “Watu wa Mwanza mliona jinsi ambavyo daraja la Busisi limekamilika, mmeona jinsi ujenzi wa SGR unakwenda kasi. Mmeona meli kubwa ya Hapa Kazi inakaribia asilimia 90 kukamilika, hayo yote ni mambo ya Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Nchimbi ambao wataendeleza mbele zaidi,”
Kada huyo aliwasihi Watanzania katika kuhakikisha Tanzania inabaki salama kwamba, hawana budi kuwapa kura za kutosha na za kishindo mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Samia na mgombea mwenza Dk. Nchimbi kwa kuwapa imani kubwa waendelee kuijenga nchi.