Na NJUMAI NGOTA,
Mara
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Mgombea Urais wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi kubwa ya kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
Aidha, Balozi Dk. Nchimbi amewashukuru viongozi wa CCM, mkoani Mara kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa kishindo.
Balozi Dk. Nchimbi ameyasema hayo wilayani Bunda, mkoani Mara, alipowahutubia wananchi wa Bunda, waliokuwa wamesimama njiani kuupokea msafara wake uliokuwa ukitokea wilayani Magu, mkoani Mwanza.
Mgombea huyo yupo mkoani humo katika kampeni za uchaguzi wa CCM za kunadi Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya mwaka 2025-2030 na kuomba ridhaa kwa wananchi kuwachagua Rais Dk. Samia, wabunge na madiwani wa Chama katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu, kwa kukiipa ushindi wa kishindo, wapate ridhaa ya kuiongoza nchi kipindi kingine cha miaka mitano.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo, Balozi Dk. Nchimbi amesema Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa ya kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo maeneo mbalimbali.
“Rais Dk. Samia na wasaidizi wake wamezisimamia fedha hizo kuhakikisha zinaleta maendeleo kwa wananchi,” amesema.
MAFANIKIO YALIYOPATIKANA BUNDA
Mgombea Mwenza wa Urais Dk. Nchimbi, ameyataja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana wilayani humo kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia ni kukamilika kwa ujenzi wa Shule ya Msingi ya Chifu Manyori, bweni la watu wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Madaraka.
Pia, ujenzi wa Kukirango na mradi mkubwa wa maji wa Mugango–Kiabakari unaendelea.
WALICHODHAMIRIA MIAKA MITANO IJAYO
Balozi Dk. Nchimbi amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo iwapo watapata ridhaa ya kuongoza nchi wamedhamiria kujenga soko la wilaya na stendi ya Kiabakari.
ASISITIZA AHADI SIKU 100 ZA KWANZA
Mgombea huyo ameendelea kusisitiza ahadi za siku 100 zilizotolewa na Rais Dk. Samia katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika viwanja vya Tanganyika Packers, jijini Dar es Salaamu.
Amezitaja baadhi ya ahadi hizo ni kukomesha utaratibu wa kuzuia maiti hospitalini kwa kigezo cha gharama , Bima ya afya kwa Wote hususan kwa wajawazito, wazee, watoto, watu wenye ulemavu na ajira kwa watumishi 5,000 wa kada ya afya.