Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
KASI ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo imeendelea kuwavutia wananchi visiwani humo, wakieleza kuwa hana mbadala kwa miaka mitano ijayo.
Wamesema utekelezaji wa miradi hiyo ni kielelezo cha uungwana na uaminifu wa Rais Dk. Mwinyi, ambaye ameendeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 kupitia kaulimbiu yake ya “Yajayo Yanafurahisha.”
Kauli hiyo imetolewa na wananchi mbalimbali walipozungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea miradi ya maendeleo katika mikoa tofauti ya Zanzibar.
Mwajuma Zanuni Omar, mnufaika wa makazi bora baada ya kupisha ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mangapwani, alisema Rais Dk. Mwinyi ameonyesha dhamira ya dhati ya kuijenga Zanzibar mpya na kuifanya kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda huu.
“Mimi ni mkazi wa Shehia ya Kidanzini, Wilaya ya Kaskazini B ambako kunajengwa Bandari ya Mangapwani, baada ya kupisha ujenzi huo tunajengewa nyumba za kisasa zenye kila hali ya kuitwa bora, awali tuliziona tu kwenye televisheni na picha lakini sasa tutazimiliki tunamshukuru Dk. Mwinyi, ” alisema.
Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Kidanzini, Mzee Salmin Mbaruku, alisema mradi wa bandari ya Mangapwani ni kielelezo cha maendeleo ya kweli yenye kuwagusa wananchi.
Amesema ujenzi wa bandari hiyo imekuja na fusa mbalimbali miongoni mwa hizo ni wananchi kupata makazi bora na ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hamada Sharif Vuai alelisema, katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Dk. Mwinyi, mkoa huo umefanikiwa kupata miradi mingi ya maendeleo iliyotatua changamoto za wananchi.
Miongoni mwa miradi hiyo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Pangatuputu ambayo imewaondolea wananchi adha ya kwenda umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu.
Pia, serikali imejenga za kisasa za msingi ma sekondari ikiwemo ya Misufini iliyozinduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Januari mwaka huu ikiwa na mahitaji yote ya msingi kwa mwanafunzi kujifunza.
Lakini pia mradi wa masoko ya kisasa ambayo yamewaondoshea adha wajasiriamali ya sehemu ya kufanyia biashara zao.




