Na MUSSA YUSUPH
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, ametaja sababu za mikutano ya mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, kufurika maelfu ya wananchi kumsikiliza kiongozi huyo akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025 – 2030).
Amesema kukubalika kwa mgombea huyo wa Urais kupitia CCM, ndiyo, sababu ya mikutano yake kujaza wananchi tofauti na mikutano ya vyama vingine vya siasa nchini.
Akizungumza katika mahojiano maalumu kabla ya kuanza mkutano wa kampeni uliofanyika Mlima wa Reli, Mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, Kihongosi amesema hakuna mgombea mwingine wa Urais kutoka vyama vingine vya siasa mwenye uwezo wa kumfikia Dk. Samia.
“Samia ni mgombea wa mfano, ana uzoefu wa ndani na nje ya nchi. Anayejua kazi, anapendwa na wananchi na ndiyo sababu mikutano ya kampeni ya CCM inajaza watu wengi tofauti na vyama vingine.
“Wananchi wanakipenda CCM na wagombea wake, wanapenda kiendelee kuwepo madarakani kiendekee kuwatumikia, sasa ukija na hoja dhaifu kuwa CCM inabeba watu, CCM haijibu hoja dhaifu bali tunajibu hoja nzito ambazo zinakwenda kutoa majawabu kwa Watanzania, wajibu wa CCM ni kutatua kero za wananchi,” amesema.
Kihongosi amebainisha kuwa, ndani ya miaka minne, Dk. Samia amefanya mambo makubwa na kila kata, wilaya, mikoa imepelekewa fedha za kutekeleza miradi katika sekta mbalimbali.
Katika kuthibitisha hilo katika mkutano huo wa kampeni, idadi kubwa ya wananchi walimiminika katika uwanja wa Mlima wa Reli hali ambayo iliwalazimu wengine kubaki nje ya uwanja kufuatilia mkutano huo.
Shauku ya wananchi hao ilijikita zaidi kumshuhudia kiongozi huyo ambaye ameleta mapinduzi makubwa katika wilaya hiyo ambayo tangu ilipoanzishwa miaka ya 1980 haikuwa na hospitali ya wilaya, ndani ya miaka minne ya uongozi wa Dk. Samia, imejengwa hospitali ya kisasa yenye kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za mama na mtoto.
Pia, mji huo mdogo umenufaika na ujenzi katika sekta ya maji, amesema sh. bilioni 4.8 zimewekezwa katika mradi wa Ilulu utakaoleta maji safi na salama katika eneo la Mbalizi.
Kuhusu elimu, amesema sh. bilioni 9.3 zimetumika kujenga shule na nyumba za walimu huku sh. bilioni 13.9 zimetumika kujenga madarasa 29 na maabara 14.