Na MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Mgombea Urais kupitia Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu, Dk. Samia Suluhu Hassan, atapigiwa kura nyingi kwa sababu, wananchi wameiona kazi kubwa aliyoifanya kuleta maendeleo kwa miaka minne iliyopita.
Amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030, imejikita kusimamia uchumi na kuhakikisha inawagusa wananchi kila sekta.
Wasira, amesema hayo jana Simanjiro mkoani Manyara, akiwa katika ziara ya kuitafutia ushindi wa kishindo CCM kupitia Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani.
“Ndiyo maana tunaandika Ilani, ukitazama mafanikio yaliyopatikana wala sihitaji kutumia takwimu, maana Watanzania hata wa Simanjiro wanajua mafanikio yaliyofanyika hapa, wanajua kiwango cha vituo vya afya vilivyojengwa, wanajua madarasa yaliyojengwa hapa, wanajua majosho yaliyojengwa ya wafugaji na juzi Mama Samia ametoa ruzuku ya kuchanja mifugo,” alisema.
Amesema wananchi wa Tanzania wanajua jitihada zilizofanywa na Chama huku akitolea mfano, Simanjiro kumekuwa na matatizo makubwa ya maji na yanashughulikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Kwa hiyo, nimekuja kutoa wito kwa wananchi wa Simanjiro, kuhakikisha wapigakura wote wanatoka kwenda kupiga kura, wasisahau na wakumbuke kumpigia kura Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Tukamilishe safu kwa mafiga matatu, halafu tukimaliza tunawatuma kusikiliza Ilani.
“Ilani katika siku zijazo, tunataka kusimamia uchumi wa watu wa Tanzania, kama ni wafugaji tunataka kuwasaidia wafugaji ili ufugaji wao uwalipe, kama ni wakulima tunataka kuwasaidia wakulima tuwape zana, tulete miradi ya umwagiliaji walime waondokane na umaskini, kama ni wavuvi tutawapa vifaa vya kuvua na tunaka kuanzisha viwanda kulingana na malighafi inayopatikana.
“Hapa Simanjiro malighafi yake ni mifugo, kwa hiyo ukitaka kuanzisha viwanda utaanzisha vya nyama,” ameeleza.
Amesema kila wilaya itakuwa na viwanda vyake kutokana na mazao yanayozalishwa eneo husika na kwamba, hivyo ndivyo Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyosema shabaha ikiwa kuleta maendeleo kwa wote.
Amesisitiza kuwa, serikali inatumia fedha na gharama kubwa kwa wananchi wakiwemo wa vijijini kuhakikisha maisha yao yanazidi kuwa bora.
Hivi hapa Simanjiro ambapo vijiji vyenu vipo kilometa 70 kutoka mjini nani alijua umeme utaenea hadi ufike kijijini, lakini umefika vimebaki labda vitongoji tu. Vijiji vyote vya Tanzania vina umeme, tutaendelea kujenga vitu hivi kujenga uchumi na shabaha kubwa ni kusaidia uchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Ndugu zangu nilitaka niyaseme hayo na kubwa kuliko yote ni kwamba, lazima tushinde uchaguzi,” ameeleza.