Na MUSSA YUSUPH,
Nzega
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema siri ya mafanikio katika uongozi wake ni usimamizi madhubuti wa fedha za maendeleo na mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema katika mataifa yaliyokithiri vitendo vya rushwa ni vigumu kusikia masimulizi ya utekelezaji miradi ya maendeleo kama yaliyopatikana nchini.
Akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Samora wilayani Nzega mkoani Tabora, Dk. Samia alisema Watanzania wanapaswa kujivunia mafanikio yanayoendelea kupatikana nchini.
“Niseme moja kubwa ambalo sijalisema kokote, kazi zote hizi, tutazozizungumza zimetumia fedha nyingi sana inayokusanywa ndani, tunayokopa nje na ile tunayopewa na marafiki.
“Miradi imewezekana kujengwa Tanzania nzima, kila unaposimama, hadithi ni nyingi kwamba, tumeleta maji, tumeleta umeme, tumeleta kilimo na afya. Imewezekana kwa sababu tumesimamia matumizi mazuri ya fedha,”amesema.
Amesema serikali imesimamia matumizi mazuri ya fedha na watumishi kuwekwa katika mazingira ya kuepuka rushwa.
“Tungeacha mianya ya rushwa na kutokusimamia vizuri fedha hizi, miradi tunayoizungumza leo isingekuwepo. Tumefanya kazi kubwa kupunguza rushwa na hata tafiti zinazofanywa na mashirika ya kimataifa kila mwaka, Tanzania inapanda juu katika viwango vya kupunguza rushwa ndani ya nchi.
“Kwa pamoja, tuwapongeze watumishi wa serikali hata waliopo sekta binafsi, wamesimamia vyema kupunguza viwango vya rushwa na ndiyo maana maendeleo yanaonekana.
“Nchi zilizotawaliwa na rushwa hawazungumzi tunayoyazungumza leo sisi, ndugu zangu Tanzania yetu tujipongeze sana,”amesema.
AHADI KWA WANANCHI
Pia, Dk. Samia, alitoa ahadi ya ujenzi wa machinjio manne na majosho sita ya wafugaji wilayani Nzega.
Alisema serikali itaendelea kutoa ruzuku ya chanjo kwa mifugo na kuwaomba wafugaji kupeleka mifugo yao kupatiwa chanjo.
“Hatua hiyo, itaifanya Tanzania itambulike, iingie katika ramani ya kimataifa katika masuala ya ufugaji. “Tutaendelea kuimarisha upatikanaji maji na tunakwenda awamu ya pili ya mradi wa Ziwa Viktoria,” alieleza.
Alisema kupitia mradi huo, maji yatapelekwa katika maeneo ya Kata za Bukene, Mwamala, Itobo, Isanzu, Kasela, Buduka, Shinyanga na Itindwa.
Alibainisha kuwa, lengo ni kuwasaidia wananchi 85,607 wanaokwenda kufaidika na mradi huo, pindi CCM ikipewa ridhaa.
Kuhusu miundombinu, alisema barabara ya Nzega – Itobo – Kagongwa yenye urefu wa kilometa 65, serikali imejipanga kutekeleza na kukamilisha mradi huo.
MWENYEKITI WA CCM, TABORA
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Said Nkumba, alisema wamejipanga kuhakikisha Dk. Samia, anapata kura za kishindo.
K0auli hiyo, aliitoa Uwanja wa Barafu, wilayani Igunga, alipomwombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Samia.
“Tunawakumbusha kila aliyejiandikisha apige kura na kazi hiyo tutafanya. Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Tabora, ikifika Oktoba 29, twendeni tukampigie kura Dk. Samia,” alisema.
MAOMBI YA BASHE
Akijibu maombi ya mgombea ubunge Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe, Dk. Samia, alisema ameyachukua kwenda kuyafanyiakazi.
“Mwenyewe anajua ndiyo maana kaniambia usinijibu hapa, yabebe ukayafanyie kazi. Kwa hiyo kuna halmashauri, kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kujengwa Nzega, hili la mkoa tutakwenda kuyafanyia kazi,” alisema.
Dk. Samia, alilazimika kutoa majibu hayo baada ya Bashe kumwomba kuzingatia ombi la kuugawa Mkoa wa Tabora.
Alisema Mkoa wa Tabora ni mkubwa kiutawala, kwani wananchi wa maeneo ya mbali kama Bukene, hulazimika kusafiri zaidi ya kilomita 220 kufuata huduma za mkoa.
“Tunakuomba Mkoa wa Nzega. Ukichukua Igunga, Manonga, Nzega DC na Uyui Kaskazini, watu ni zaidi ya milioni 1.8.
“Tunaomba mkoa huu ugawanywe kwa sababu ni mkubwa mno. Ombi hili, tumelilia kwa muda mrefu na litakuwa kumbukumbu kwako, Mama Samia,” alisema Bashe.
Akizungumzia miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Samia, Bashe alisema kata zote 10, vijiji 21 na vitongoji 176 vya Nzega Mjini, vina huduma ya maji safi na salama.
“Zaidi ya kaya 14,000 zimeunganishiwa maji kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria. Wakati anaingia madarakani, kulikuwa na sekondari nne tu, lakini sasa zimefikia 16 na hakuna kata isiyo na shule ya sekondari.
“Kata zote zina umeme. Urefu wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 160 hadi 517. Barabara ya kutoka Kitangiri hadi Mwanayagula imejengwa, ikirahisisha usafiri na biashara kwa wakazi wa vijijini,” alisisitiza.
Katika kilimo, alisema serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kusaidia wakulima nchini.
AUNGURUMA IRAMBA
Awali, akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Iramba mkoani Singida, Dk. Samia alisema baada ya kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa miaka mitano iliyopita, CCM imejiamini kwa ujasiri kurudi kwa wananchi kuomba ridhaa ya kutekeleza ilani ya uchaguzi 2025 – 2030.
“Kwa upande wa utekelezaji ilani iliyopita, wabunge wameeleza vizuri kwenye afya tumefanya mambo mazuri lakini bado tutaendelea kwa sababu tunatambua mahitaji bado yapo.
“Tutaendelea na ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa zahanati lakini kubwa zaidi kusimamia upatikanaji matibabu na dawa kwa wananchi,” alisisitiza.
Dk. Samia alisema serikali inakwenda kuanza majaribio ya bima ya afya kwa wote na kwa maradhi ambayo wananchi wasiokuwa na uwezo kugharamia matibabu serikali itakwenda kugharimia.
“Wale wasiokuwa na uwezo, serikali itakwenda kugharamia kwa asilimia 100. Kama mkulima wa choroko, mbaazi na dengu umeuza na fedha ipo, tunakutaka ununue bima yako ya afya.
“Kwa wale ambao hawana uwezo kabisa serikali inakwenda kusimamia wananchi wake,”alisema.
Akizungumzia elimu, Dk. Samia alisema serikali imefanya mengi kwa kujenga vyuo vya ufundi na itaendelea kujenga shule kadri mahitaji yanavyoongezeka.
Kwa upande wa maji, alieleza kuwa serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini hata hivyo inatambua baadhi ya maeneo kutofikiwa na huduma hiyo.
Kuhusu umeme, alieleza serikali iliahidi kuweka umeme vijiji vyote ambavyo ahadi hiyo imeikamilisha.
Dk. Samia alisema kwa sasa huduma hiyo inaunganishwa katika vitongoji.
Alieleza kuwa nishati hiyo, imewafikia hadi wachimbaji wadogo kuwawezesha kupata urahisi wa uchimbaji na kujiimarisha kiuchumi.
UANZISHWAJI SOKO LA MADINI
Alisema serikali imeahidi uanzishwaji soko la madini ambalo limeshaanzishwa eneo la Shelui wilayani Iramba.
Alisema zaidi ya gramu milioni 1.5 zimeuzwa kwa thamani ya sh. bilioni 192.
“Niwaombe wachimbaji tumeweka soko lile ili dhahabu inayochimbwa, vito vinavyopatikana viuzwe ndani ya soko badala ya kuchepusha na kupeleka nje bila kuuza ndani ya nchi,” alieleza.
Kwa upande wa Iramba Mashariki, alisema serikali itakamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika Kijiji cha Ishishi, Kata ya Msingi kwa gharama ya sh. bilioni 34.
Alisema lengo ni wakulima walime mara mbili kwa mwaka.
“Tulipokuwa tunategemea mvua ya Mwenyezi Mungu wakulima walilima mara moja kwa mwaka, sasa watakwenda kulima mara mbili kwa mwaka,”alisema.
Kadhalika, alisema anafahamu kuna uhitaji kuufungua Mji wa Kiomboi kwa kuimarisha mawasiliano kati ya Wilaya ya Iramba na Mkalama.
Hivyo, alisema serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara za Iguguno hadi Sibiti na ya Kiomboi hadi Mtulia.
DK. MWIGULU
Mgombea Ubunge Jimbo la Iramba Magharibi, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema Dk. Samia anastahili kuungwa mkono na kupewa kura za ushindi.
Alisema Dk. Samia ni kiongozi mwadilifu katika kusimamia mapato ya nchi, uwazi katika matumizi ya fedha za umma na kuleta maendeleo.
Dk. Mwigulu ambaye ni Waziri wa Fedha, alisema tangu Dk. Samia alipoingia madarakani mapinduzi makubwa ya kiuchumi yameshuhudiwa.
Aliyataja baadhi ya mafanikio ni ongezeko la mapato ya serikali kutoka sh. trilioni 1.2 hadi sh. trilioni tatu kwa mwezi.
Alieleza kuwa, uongozi wa Rais Dk. Samia umefanikiwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato kupitia kodi, jambo ambalo limewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Mgombea ubunge Jimbo la Iramba Mashariki, Jesca Kishoa, alieleza kuwa, kazi nzuri alizozifanya Dk. Samia kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wake amedhihirisha kuwa, anaweza.
Naye, mgombea ubunge Jimbo la Manonga Abubakari Ally, alisema wananchi wa Manonga wamenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo.