Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Sera ya Nishati ya Zanzibar ya 2025, inalenga kukuza uwekezaji katika utafiti, teknolojia na uvumbuzi maeneo ya nishati safi, matumizi bora na teknolojia za kisasa zinazopunguza gharama na kuongeza ufanisi.
Dk. Mwinyi, aliyasema hayo Mjini Unguja, akizindua sera hiyo katika Ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa Ndege.
Alisema sera hiyo, inahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kupunguza moshi na kemikali hatarishi, zinazotokana na matumizi ya kuni, makaa na mafuta yasiyo safi.
Aidha, alisema hatua hiyo, itapunguza magonjwa ya mfumo wa kupumua na matatizo mengine ya kiafya.
Dk. Mwinyi, alibainisha kuwa, sera hiyo, itawawezesha wanawake kwa sababu, mara nyingi wanahusika na shughuli za kupikia, kwani matumizi ya nishati safi, inawapa nafasi zaidi ya kushiriki shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
Pia, alisema sera hiyo, imeandaliwa kuleta mageuzi na mwelekeo mpya katika sekta itakayoimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Alisema lengo la sera hiyo ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu ya uhakika kwa wananchi wote, kuongeza usalama wa nishati kupitia vyanzo vya ndani na usambazaji wa aina za nishati.
Alitaja lengo lingine ni kuendeleza matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira kwa kuhamasisha uzalishaji umeme wa jua, upepo, biofuel na gesi, nyuklia na kushirikisha sekta binafsi kupitia uwekezaji na ubia.
“Serikali imeweka dhamira ya dhati ya kuijenga Zanzibar yenye uchumi shindani, kijani na jumuishi, kuhakikisha nishati ya uhakika, inaendelea kuimarika nchini, kwani sekta hii, ndiyo injini ya maendeleo ya viwanda, utalii, kilimo cha kisasa, teknolojia ya habari na maisha ya kila mwananchi,” alibainisha.
Akizungumzia Mpango Mkuu wa Umeme wa Zanzibar 2025-2050, alisema umeandaliwa kwa mara ya kwanza nchini, ukiwa na lengo la kutoa picha ya utabiri wa mahitaji ya umeme ya Zanzibar hadi mwaka 2050.
Alisema kupitia mpango huo, upatikanaji wa taarifa zinazohusiana na mahitaji ya umeme Unguja na Pemba, utakuwa rahisi kufikia mwaka 2050.
“Kwa msingi huo, miradi mikubwa ya kuzalisha nishati itaendelezwa, ikiwemo ya nishati ya jua, upepo, mitambo ya gesi na mifumo ya akiba ya umeme kupitia teknolojia za battery storage,” alisema.
Mbali na hayo, alisema matarajio ya utekelezaji wa sera hiyo na mpango mkuu wa umeme Zanzibar, ni kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo, kwa jamii, hasa maeneo ya vijijini na yasiyo na umeme wa uhakika.
Pia, alisema kuweka mkazo katika matumizi ya vyanzo vya nishati safi kama vile ya jua na upepo na kuendeleza miundombinu ya umeme ikiwemo mitambo ya kuzalisha umeme, usambazaji na mifumo ya akiba ya umeme.
Alisema ni kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya nishati, kuhakikisha ufanisi na uwazi katika shughuli za nishati na kuchangia maendeleo ya uchumi wa buluu kwa kutumia nishati endelevu na kuimarisha mazingira.
Alitaja matarajio mengine ni kuweka mikakati ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa nishati safi na ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi, kwa kuvutia wawezekaji kupitia sera rafiki na mazingira bora ya biashara.
Alisema matarajio hayo, yanatarajiwa kuimarisha maisha ya wananchi, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kulinda mazingira na hatimaye kuchangia kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu ifikapo mwaka 2050.
Aliwataka viongozi na taaissi zote, zilizoguswa katika utekelezaji wa sera hiyo kushirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Madini, kufanikisha utekelezaji wa malengo ya sera hiyo na kuimarisha ustawi wa maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza washirika wa maendeleo, wakiwemo Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), Benki ya Dunia na washirika wengine wa kikanda na kimataifa kwa msaada wao katika kuendeleza jitihada mbalimbali za sekta hiyo.
Naye Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kazi nzuri anayofanya kwa wananchi wa Zanzibar katika kuwaletea maendeleo.
Mapema, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Kilangi, alisema sera hiyo, inayolenga kuhakikisha Zanzibar inakuwa na huduma ya nishati ya uhakika, endelevu na salama ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Alisema kupitia sera hiyo, Zanzibar imetoa kipaumbele kuhusu ujenzi na matumizi ya miundombinu imara ya nishati inayohimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na mikakati ya dharura kuhakikisha huduma ya nishati inaendelea kupatikana bila kukatika.
Dk. Rhonda Jordan Antoine ni Mtaalamu Mwandamizi wa Nishati, alisema Benki ya Dunia ni mshirika wa karibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mkakati wa benki hiyo wenye thamani inayokaribia dola milioni 400 unaotekelezwa katika maeneo ya maendeleo ya miji, nishati, elimu, utalii na ustahimilivu.
Aidha, alisema benki ya dunia ipo tayari kusaidia utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.