NA MUSSA YUSUPH
KISHINDO cha Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mikoa 10, ambayo amefanya mikutano ya kampeni, kimethibitisha kuwa ataibuka na ushindi mkubwa.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa, Mbeya, Njombe, Singida, Tabora, Kigoma na Songwe.
Baada ya kuhitimisha kampeni katika mikoa hiyo, Dk. Samia Suluhu Hassan, kesho ataanza mikutano Zanzibar.Aliwasili juzi mjini Unguja na kupokewa na mamia ya wananchi na viongozi mbalimbali.
Safari ya Dk. Samia kuanza kusaka kura za Urais, ilianzia jijini Dar es Salaam, alipozindua kampeni za Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Katika mkutano huo, Dk. Samia alitaja vipaumbele 13 ambavyo serikali yake itavitekeleza ndani ya siku 100, ikipata ridhaa ya wananchi.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo ambavyo vimewagusa wananchi ni uanzishwaji bima ya afya kwa wote ambayo itagharamia makundi ya wasiojiweza, ajira 12,000 na kupiga marufuku hospitali kuzuia maiti.
Alipomaliza uzinduzi wa kampeni Dk. Samia, alianza safari ya kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025 – 2030), mkoani Morogoro.Juzi, Kigoma ulikuwa mkoa wa 10 kabla ya safari ya kwenda Zanzibar.
KIGOMA SIYO MWISHO WA RELI
Katika mkutano wake uliofanyika Uwanja wa Katosho mkoani Kigoma, Dk. Samia, alisema miaka iliyopita watu walizoea kusema Kigoma ni mwisho wa reli, ila kwa kasi ya maendeleo yanayoonekana mkoani humo, ni kitovu cha uchumi na biashara.
Alibainisha kuwa, hata ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR) hautoishia Kigoma bali utakwenda hadi Burundi kisha kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hivyo mkoa huo siyo tena mwisho wa reli.

Alisema Agosti mwaka 2022 alifika wilayani Kakonko kuzindua miradi mitatu muhimu ambayo ni barabara ya Kabingo – Nyakanazi, mradi wa maji Nyamfisi na hospitali ya wilaya.
Alieleza kuwa hayo ni sehemu ya maendeleo ambayo yalianzia katika kipindi cha awamu ya tano kisha akaikamilisha na kuzindua huku akitumia fursa hiyo kuahidi hakuna miradi itakayosimama.
Alitaja miongoni mwa ahadi ambazo CCM na serikali yake iliweka kwa wananchi mkoani Kigoma ni kuutoa kutoka pembezoni hadi kuufanya kuwa wa kimkakati.
ASISITIZA KUGUSA MAKUNDI YOTE
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Nanenane Ipuli mkoani Tabora, Dk. Samia, alisema CCM imedhamiria kujenga uchumi jumuishi unaozingatia ustawi wa wananchi maeneo ya mijini na vijijini.
Alisisitiza huo ndiyo msingi mkuu wa kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu’ yenye dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa, taifa lenye kujitegemea na kuneemesha watu wake.
Pia, aliahidi neema ya ujenzi wa madaraja 133 na taa za barabarani 2,500 katika barabara za kimkakati ndani ya mkoa huo kinara kwa kilimo cha tumbaku.
Vilevile, alisisitiza serikali yake itaendelea kuimarisha huduma za afya, elimu, nishati, maji na miundombinu.
Alisema mmoja wa waasisi na Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisoma katika mkoa huo.
Dk. Samia alisema hayo yanathibitisha namna ambavyo CCM ina historia kubwa mkoani Tabora.
TRILIONI TISA ZAINEEMESHA DODOMA
Maelfu ya wananchi, Dodoma walidhihirisha kuwa, CCM imeendelea kukubalika kwa kishindo baada ya kujitokeza katika mikutano ya mgombea Urais kupitia CCM.
Katika mikutano ya kampeni ndani ya mkoa huo, iliyoanzia Kibaigwa wilayani Kongwa, Chamwino, Chemba, Kondoa kisha kishindo kikuu kuhitimishwa ndani ya Jiji la Dodoma ambako watu wengi, walihudhuria viwanja vya Tambukareli huku viongozi mbalimbali wakiungana na Dk. Samia kuwaomba wananchi kura zote kwa wagombea wa CCM.
Katika hotuba yake, Dk. Samia alisema: “Awamu ya tano tulifanya maamuzi ya kuhamia Dodoma, awamu ya sita tumekwenda kuendeleza kuhamia Dodoma, taasisi zote za serikali zipo Dodoma, maamuzi yote makubwa sasa yanafanyika hapa.”
Aliongeza: “Tumemimina sh. trilioni 9.5 kwa miradi 3,093 ndani ya Mkoa wa Dodoma, mbali na kuongeza majengo na kuipa hadhi Hospitali ya Benjamin Mkapa, wilaya za Dodoma zina hospitali za kisasa ambazo vipimo vyote vinapatikana huko.”
Pia, alisema serikali yake imejitahidi kufungua fursa za ajira kupitia uwekezaji kwa kujenga viwanda, kutengeneza fursa kwa wafanyabiashara wadogo huku mradi wa reli ya kisasa (SGR) ukiongeza kasi ya ukuaji uchumi.
Kuhusu umeme, alisema serikali inaendelea na kazi ya kumalizia vitongoji kila mtu apate nishati hiyo kufanyakazi na kulinda usalama wao.
Vilevile, alisema Chama kimejipanga kutatua uhaba wa maji kwa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na kumalizia ujenzi bwawa la Farkwa kusaidia kuleta maji Dodoma.
Alitoa ahadi ya kuongeza kasi ya upimaji na usajili ardhi kutatua migogoro, kukamilisha ujenzi wa kiwanja kikubwa cha mpira wa miguu na kuwa, tayari mkandarasi ameshapatikana.

YAJAYO YANAFURAHISHA
Akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Bombadia Singida Mjini, Dk. Samia alisema uwekezaji unafanyika nchi nzima kujali utu wa mtu.
Alisema yote yanayofanyika ni katika kujali utu wa Mtanzania na kuwaomba Watanzania kukipa ridhaa CCM kikafanye makubwa zaidi yanayomjali Mtanzania.
Akizungumzia miradi ya maendeleo katika mkoa huo, alisema CCM iliahidi kufikisha umeme katika vijiji vyote 441 mkoani hapa kazi ambayo imekamilika.
Alieleza kuwa, serikali inaendelea kusambaza umeme katika vitongoji kazi ambayo inatarajiwa kukamilishwa ndani ya miaka mitano ijayo.
Katika kilimo, alisema mkoa huo unasifika kwa kilimo na kulikuwa na skimu tatu za umwagiliaji, hata hivyo kulikuwa na uhitaji wa skimu zingine zaidi.
IRINGA NA NJOMBE NEEMA TUPU
Mikutano ya Dk. Samia katika mikoa ya Njombe na Iringa imeacha neema kwa wananchi. Alipoingia mkoani Iringa, msafara wa Dk. Samia ulianza kupokelewa eneo la Nyololo ambako alihutumia wananchi waliosimama kando ya barabara ya TANZAM.
Dk. Samia ambaye anasifika zaidi kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya miaka minne na nusu ya uongozi wake, aliendelea kukidhi kiu ya wananchi na kueleza mambo mbalimbali ambayo serikali yake itayafanya akiingia madarakani.
Akiwa mkoani wilayani Mafinga mkoani Iringa, alisema anataka kila Mtanzania anufaike katika sekta zote za maendeleo.
Alisema serikali yake, imedhamiria kila Mtanzania apate umeme kumrahisishia kufanya shughuli za kiuchumi, pia kulinda usalama wa maeneo.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo mjini Makambako mkoani Njombe, alisema ndani ya mwezi huu NFRA watafungua vituo vya ununuzi mazao.

MOROGORO YA VIWANDA
Akiwa katika mji huo maarufu kwa shughuli za kilimo, Dk. Samia aliwaeleza wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo maarufu kwa shughuli za kilimo kujitokeza kumuunga mkono Dk. Samia aliponadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuahidi kuurejesha mkoa huo kuwa wa viwanda.
Alisema katika miaka mitano ijayo, serikali itawekeza zaidi katika sekta ya afya mkoani humo kwa kujenga vituo vya afya 28 na zahanati 97 huku Manispaa ya Morogoro vitajengwa vituo viwili vya afya na zahanati 11.
Pia, alisema serikali itakamilisha maabara, jengo la upasuaji na Kituo cha Afya Tungi pamoja na wodi ya mama na mtoto eneo la Mafiga.
Alisema CCM kupitia ilani yake imepanga kujenga vituo vya kupoza umeme, Tungi, Msavu, Kilosa na Mvomero.
BARABARA YA TANZAM
Akiwa mkoani Songwe, Dk. Samia alitangaza mpango wa uboreshaji wa barabara ya TANZAM na reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) lengo likiwa kumaliza msongamano wa malori yanayokwenda nchini Zambia kupitia mpaka wa Tunduma.
Alisema barabara hiyo, imeanza kujengwa kwa njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa kilometa 75 hatua ambayo itaimarisha shughuli za usafirishaji mizigo katika njia hiyo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Tunduma mkoani Songwe, Dk. Samia alisema uboreshaji uliofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, umechochea ongezeko la mizigo kutoka tani milioni 15 hadi tani milioni 28 kwa mwaka.
Alisema ukarabati huo, umeanza kwa njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma kwa urefu wa kilometa 75 huku mazungumzo ya kukarabati na kuimarisha reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) yakiendelea.
RUZUKU KWA WAKULIMA
Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni katika uwanja wa Mlima wa Reli uliopo Mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, Dk. Samia, alisema ruzuku hiyo inatolewa kwa wakulima wote nchini.

Aliyataja baadhi ya mazao ambayo mbolea na mbegu za ruzuku zinatolewa ni mahindi, mpunga, tumbaku na parachichi.
Kuhusu wafugaji, alisema serikali itakamilisha ujenzi wa machinjio ya mifugo ya kisasa Utengule.
Alisema serikali inaendelea na kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo yenye lengo la kuongeza hadhi ya mifugo kutoka Tanzania katika masoko ya kimataifa.
KAULI ZA WANANCHI
Katika mikoa hiyo ambayo Dk. Samia amefanya mikutano ya kampeni, wananchi walieleza imani yao kwa mgombea huyo wa Urais.
Akizungumza na gazeti hili, mkazi wa Tabata Segerea, Maimuna Aloyce, alisema CCM imefanya utafiti wa kutosha kwa wananchi kwani baadhi ya mambo yaliyoelezwa ndiyo miongoni mwa kero zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Naye, Mkazi wa Isimani mkoani Iringa, Mkama Bushiri alieleza namna Dk. Samia alivyogusa kundi la wazee ambalo mara nyingi ndilo limepata changamoto katika kupata matibabu.