Na VICTOR MKUMBO
SERIKALI imeipongeza klabu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii msimu huu, baada ya kuifunga Simba kwa bao 1-0, katika mchezo uliofanyika, Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Bao pekee lililoipa Yanga ubingwa katika mchezo huo liliwekwa kimiani dakika ya 55 na staa wake Pacome Zouzoua baada ya kupiga shuti lililojaa wavuni moja kwa moja.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amesema anaipongeza Yanga kutokana na kuonyesha kiwango bora na kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
Hata hivyo timu zote zilionyesha ushindani wa aina yake kutokana na kufanya usajili bora msimu huu.
Waziri Mchengerwa amesema hiyo yote imetokana na serikali kuendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya michezo na kuhakikisha Tanzania inakuwa moja ya nchi zenye ligi bora.
Amesema kuwa ameshashuhudia mechi zilizozikutanisha Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, lakini mchezo wa juzi wachezaji wote walionyesha kiwango cha hali ya juu.
Amesisitiza katika mchezo huo wachezaji walionyesha kiwango kizuri na kutoa burudani kwa mashabiki zao tofauti na wengi walivyotarajia.
Amesema katika fainali lazima mshindi apatikane, hivyo anaamini Simba watakwenda kujipanga upya kuhakikisha wanarudi kivingine msimu ujao.
“Ninawapongeza Yanga kwa kubeba taji la mchezo wa Ngao ya Jamii msimu huu kwani walionyesha kiwango cha hali ya juu.
“Hii imetokana na serikali kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kuhakikisha mchezo wa soka unakuwa moja ya ajira kwa vijana.
“Timu zote zilionyesha kiwango bora na kila mmoja alionyesha jitihada, hivyo ninaamini Simba watakwenda kujipanga na kurudi kivingine katika mechi zinazo,” alisema Mchengerwa.
Huo ulikuwa mchezo wa 11 kwa timu hizo kukutana katika Ngao ya Jamii, huku ukiwa mchezo wa 21 tangu kuanza kwa kombe hilo mwaka 2021.
Yanga inakuwa timu ya kwanza kuweka rekodi ya kushinda mara sita taji hilo na kujiwekea rekodi ya kushinda mara nyingi zaidi ya mpinzani wake kwani michezo 10 iliyopita kila timu ilishinda mara tano.
Yanga waliifunga Simba mabao 2-1 (2001), mikwaju ya penalti 3-1 (2010), bao 1-0 (2021), mabao 2-1 (2022) na bao 1-0 msimu uliopita kabla ya juzi kushinda bao 1-0.
Simba ilishinda mechi zake za Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga mabao 4-1 (2002), ikiifunga mabao 2-0 (2005), 2-0 (2011), mikwaju ya penalti 5-4 (2017), kabla ya kushinda tena kwa mikwaju ya penalti 3-1 (2023) mechi pekee iliyofanyika Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.