Na MUSSA YUSUPH,
Bunda
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Steven Wasira, ametoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya kikundi cha watu wachache wanaoleta chokochoko katika mitandao ya kijamii.
Amesema kikundi hicho ni miongoni mwa wachache wasioridhika hata hivyo, kamwe hawatoweza kutimiza dhamira yao ovu.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za Urais uliohutubiwa na Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, alisema amani na utulivu, itaendelea kutawala nchini.
“Zipo chokochoko nyingi ambazo hazipo kwa watu, zipo kwa wachache wanaotumia mitandao ya kijamii. Naomba msome ile mitandao kwa makini sana. Kuna watu hawaridhiki.
“Kinamama wanaopika maharage, wanafahamu yapo maharage hata ukiyapika vipi yatatokea machache yakielea. Hayo hayaivi, ndiyo watu wanaosumbua,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa: “Watu hao, hawawezi kuisumbua nchi, namwambia mgombea wetu (Dk. Samia), asibabaishwe na watu hao wachache, hata ukifanya vizuri namna gani, wao wananuna, ndivyo walivyo.
“Wapo watakaokumbuka kwa wema wenye nia njema, Dk. Samia amefanyakazi kubwa, jinsi mnavyomuunga mkono hapa, ndivyo anavyoungwa mkono Tanzania nzima.”
Wasira alisema CCM imewaletea mgombea Urais mwenye mafanikio makubwa ya utekelezaji ilani ya uchaguzi iliyopita na siyo mwenye uwezo mdogo.
“Hatuwaletei mgombea Urais ‘lena’ tunawaletea mgombea Urais aliyefanya kazi ya urais kwa mafanikio makubwa,” alisisitiza.
Alisema Dk. Samia, aliingia madarakani katika misukosuko mikubwa wakati ambao, taifa lilikumbwa na ugonjwa wa Uviko 19, kufariki dunia kwa Rais aliyekuwa madarakani (Hayati Dk. John Magufuli) na kushuka kwa uchumi.
Alieleza kuwa, Dk. Samia alipoingia madarakani alitumia maneno mawili ambayo ni ‘Kazi Iendelee’.
“Alipewa mtihani mkubwa, aliachiwa miradi mikubwa ya nchi yetu. Aliachiwa reli haijakamilika na leo imekamilika hadi Makutupora ya Singida kilometa 722 kutoka Dar es Salaam.
“Aliachiwa Bwawa la Mwalimu Nyerere, lilikuwa chini ya asilimia 30, hata hivyo, asilimia 70 imejengwa chini ya usimamizi wa Rais Samia na Tanzania, ina umeme wa kutosha,” alibainisha.
Kwa upande wa elimu, Wasira alisema katika Wilaya ya Bunda, Dk. Samia, amejenga shule 13 za msingi, shule 15 za sekondari, zahanati 20, vituo vitatu vya afya na hospitali moja mpya.
Alisema Dk. Samia, ametoa mchango mkubwa kupunguza vifo vya kinamama na watoto kwani alipoingia madarakani alikuta katika kila vizazi hai 100,000 vizazi 500 vilifariki dunia kila mwaka na leo vimeshuka kufikia 100.
Awali, Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, alisema alipokabidhiwa Wizara ya Maji, alipewa maagizo na Dk. Samia, kuhakikisha hakuna mwanamke atakayeteseka kwa kukosa maji.
Alisema hali ya maji miaka minne iliyopita katika wilaya hiyo, ilikuwa mbaya, kwani miradi iligeuka kichaka cha watu kufanya ubadhirifu.
Aweso, alisema Dk. Samia alimwagiza kufika wilayani Bunda kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo huku akitoa fedha sh. bilioni 10 kutekeleza mradi wa maji Nyabeho.
Alisema mradi huo, umekamilika na wananchi wanapata maji safi na salama.
“Hapa tuna miradi mingi ambayo ipo iliyokamilika na mengine ipo katika hatua mbalimbali kwa gharama ya sh. bilioni 20. Zaidi ya wananchi asilimia 87 eneo la Bunda Mjini wanapata huduma ya maji,” alieleza.
Alieleza kuwa, maeneo yaliyokuwa na changamoto ya maji ni vijijini ambapo Dk. Samia amechukua hatua kuhakikisha huduma hiyo inapatikana.
Pia, alisema Dk. Samia ametoa fedha zaidi ya sh. bilioni 100 kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Bunda na Tarime.




