Na ATHNATH MKIRAMWENI
JUMLA ya wanafunzi wa shule 705,091 kati ya 811,074 wenye matokeo sawa na asilimia 86.93 wamefaulu kuendelea kidato cha tatu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne.
Pia, jumla ya wanafunzi 1,324,970 kati ya 1,490,314 wenye matokeo sawa na asilimia 88.91 wamefaulu na kuendelea na darasa la tano mwaka huu kwa kupata madaraja A hadi D.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed alisema katika mtihani wa kidato cha pili ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1,52 huku wavulana wakiwa na ufaului mzuri kuliko wasichana.
Profesa Mohamed alisema ufaulu kwa darasa la nne umeongezeka kwa asilimia 2.67, huku wasichana wakifanya vizuri zaidi kuliko wavulana.
KIDATO CHA PILI
Profesa Mohamed alisema wanafunzi wa shule 705,091 kati ya 811,074 wenye matokeo sawa na asilimia 86.93 wamefaulu kuendelea kidato cha tatu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne.
Alisema mwaka 2024, wanafunzi waliofaulu walikuwa 680,574 sawa na asilimia 85.41, hivyo ufaulu kuongezekwa asilimia 1.52.
“Kati ya wanafunzi 705,091 waliofaulu kuendelea kidato cha tatu, wasichana ni 392,599 sawa na asilimia 85.89 na wavulana ni 312,492 sawa na asilimia 88,28 hivyo wavulana kuwa na ufaulu mzuri kuliko wasichana.
“Kwa kuzingatia mitaala, wanafunzi waliosoma kwa mtaala ulioboreshwa wamefaulu 1,975 sawa na asilimia 89.85 na wanafunzi waliosoma kwa mtaala wa awali wamefaulu 703,116 sawa na asilimia 86.93,” alisema.
Alisema wanafunzi wa kujitegemea waliofaulu upimaji na kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne ni 5,027 sawa na asilimia 67.69.
“Katika mwaka 2024, wanafunzi wa kujitegemea 4,205 sawa na asilimia 55.94 walifaulu na kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne, hivyo kuna ongezeko la asilimia 11.75 ya wanafunzi waliofaulu na kupata fursa ya kujiandaa kwa mtihani wa kidato cha nne,” alisema.
UBORA WA UFAULU
Alisema ubora wa ufaulu kwa kuzingatia madaraja waliyoyapata wanafunzi wa shule unaonesha kuwa jumla ya wanafunzi waliopata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi tatu ni 240,469 sawa na asilimia 29.64.
Mwaka 2024, wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja kwanza hadi tatu walikuwa 239,707 sawa na asilimia 30.08, wavulana wana ubora wa ufaulu wa madaraja ya kwanza hadi tatu mzuri ikilinganishwa na wasichana ambapo wavulana ni 129,940 sawa na asilimia 36.71 na wasichana 110,529 sawa na asilimia 24.18.
Alisema ubora wa ufaulu wa wanafunzi kwa kuzingatia mitaala unaonesha kuwa wanafunzi 1,085 sawa na asilimia 49.36 wa mtaala ulioboreshwa (mkondo wa amali) wamepata daraja la kwanza hadi tatu ikilinganishwa na wanafunzi 239,384 sawa na asilimia 29.59 wa mtaala wa awali.
“Hivyo ubora wa ufaulu kwa wanafunzi waliofanya mtaala ulioboreshwa uko juu zaidi ya asilimia 19.77 kuliko wa wanafunzi waliofanya mtaala wa awali,” alisema.
UFAULU WA SHULE KATIKA MAKUNDI YA UMAHIRI
Profesa Mohamed alisema idadi ya shule katika makundi ya umahiri inaonesha kati ya shule zote 6,223 zenye matokeo, shule 6,198 sawa na asilimia 99.60 zimepata wastani wa daraja A hadi D ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.06 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Alisema idadi ya shule 1,649 sawa na asilimia 26.50 zimepata wastani wa daraja A-C.
MATOKEO YA DARASA LA NNE
Vilevile,Profesa Mohamed ametangaza kuwa jumla ya wanafunzi 889,264 wa shule walisajiliwa kushiriki Upimaji wa Kitaifa, ambapo 886,997 walikuwa wa Mtaala wa Awali na wanafunzi 2,267 wa Mtaala Ulioboreshwa (Mkondo wa Amali).
Kati ya waliokuwa Mtaala wa Awali, wasichana walikuwa 492,062 sawa na asilimia 55.48, huku wavulana wakiwa 394,935 sawa na asilimia 44.52. Kwa upande wa Mkondo wa Amali, wasichana walikuwa 794 sawa na asilimia 35.02 na wavulana 1,473 sawa na asilimia 64.98.
Profesa Mohamed alisema jumla ya wanafunzi 811,575 sawa na asilimia 91.26 walifanya upimaji, ambapo wasichana walikuwa 457,313 sawa na asilimia 92.79 na wavulana 354,262 sawa na asilimia 89.37, huku wanafunzi 77,689 sawa na asilimia 8.74 hawakushiriki upimaji.
Aidha, kwa wanafunzi wa kujitegemea 9,454 waliosajiliwa, wanafunzi 7,437 sawa na asilimia 78.67 walifanya upimaji huku 2,017 sawa na asilimia 21.33 wakishindwa kufanya.
Katika matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne, jumla ya wanafunzi 1,324,970 kati ya 1,490,314 wenye matokeo sawa na asilimia 88.91 walifaulu kuendelea na Darasa la Tano mwaka 2026 kwa kupata madaraja ya A hadi D.
Profesa Mohamed alisema ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 2.67 ikilinganishwa na mwaka 2024, ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 86.24.
“Takwimu zinaonesha kuwa wasichana wameendelea kufanya vizuri zaidi kuliko wavulana. Kati ya wanafunzi waliofaulu, wasichana ni 703,287 sawa na asilimia 90.10, huku wavulana wakiwa 621,683 sawa na asilimia 87.59, hali inayoonesha wasichana wamefaulu zaidi kwa tofauti ya asilimia 2.51,” alisema.
Kwa upande wa ubora wa ufaulu, wanafunzi 931,090 sawa na asilimia 62.48 walipata madaraja ya A hadi C, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.63 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Kwa ngazi ya shule, Profesa Mohamed alieleza kuwa kati ya shule 20,508 zilizoshiriki, shule 13,414 sawa na asilimia 65.41 zilipata wastani wa daraja la A hadi C, huku shule 20,364 sawa na asilimia 99.30 zikipata wastani wa daraja la A hadi D.
Katika masomo, ufaulu wa lugha ulikuwa mzuri kwa Kiswahili, French na Kichina ukiwa kati ya asilimia 92.10 hadi 95.73, wakati English Language ilifikia asilimia 72.71 na Kiarabu asilimia 80.45.
Masomo ya Sayansi Jamii nayo yalifanywa vizuri ambapo Jiografia na Mazingira, Sanaa na Michezo yalipata ufaulu wa asilimia 83.22 na Historia ya Tanzania na Maadili asilimia 82.99.
Pia, Sayansi ilipata asilimia 87.93 na Hisabati asilimia 81.44, ikiwa imeongezeka kwa asilimia 10.04 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Hata hivyo, Baraza la Mitihani la Tanzania lilifuta matokeo ya wanafunzi 41 wa Darasa la Nne na 29 wa Kidato cha Pili kwa udanganyifu pamoja na waliobainika kuandika matusi, huku likitoa pongezi kwa wasimamizi, walimu na wanafunzi kwa kuendesha na kushiriki upimaji kwa ufanisi.




