• ePaper
Thursday, April 16, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home AFYA

MAGEUZI MAKUBWA HOSPITALI YA OCEAN ROAD

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
March 9, 2026
in AFYA, Habari, Kitaifa, RIPOTI MAALUMU
0
MAGEUZI MAKUBWA HOSPITALI YA OCEAN ROAD
0
SHARES
12
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na MWANDISHI WETU

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Diwani Msemo, amesema katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, serikali imewekeza zaidi ya sh. bilioni 40 katika miundombinu kwa lengo la kuboresha huduma za matibabu nchini.

Dk. Msemo amesema uwekezaji huo umeiwezesha taasisi hiyo kununua mashine za kisasa, kuboresha majengo na kupanua huduma za matibabu ya saratani, hatua inayowawezesha wagonjwa kupata huduma bora, huku uelewa mdogo kwa miongoni mwa wananchi ukitajwa kusabababisha baadhi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji, hali inayowachelewesha kwenda hospitali kufanyiwa vipimo kubaini tatizo mapema.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipofanya mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu huduma za matibabu ya saratani zinazotolewa na taasisi hiyo kwa Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Katika kipindi cha Awamu ya Sita, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amewekeza zaidi ya shilingi bilioni 40 katika miundombinu pekee ya taasisi hii. Tafsiri yake ni nini kwa wagonjwa?

“Inamaanisha wagonjwa wanapata nafuu na unafuu wa gharama, kwa sababu asilimia kubwa tayari serikali imegharimia na huu ndiyo uhalisia.

“Ukienda katika nchi zilizoendelea, mashine kama PET Scan katika ukanda wa Afrika Mashariki, sisi (Ocean Road) tuna aina ya kisasa zaidi kuliko watu wengine,”alisema.

GHARAMA ZA MATIBABU

Dk. Msemo alisema matibabu ya saratani yanagharimu fedha nyingi, jambo linaloifanya serikali kuwekeza kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa gharama nafuu.

Alitoa mfano matibabu ya mionzi kwa mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi au matiti huchukua takribani wiki tano na kwa kawaida hugharimu sh. milioni tano, huku mgonjwa akitakiwa kuchangia sh. 100,000 na gharama inayobaki hubebwa na serikali.

“Kwa hiyo shilingi milioni 4.9 ni ya ORCI, maana yake ni serikali, ambayo ina jukumu la kulipa mishahara na posho. Unaweza kuona jinsi gani ambavyo inasaidia.

“Pamoja hayo, hata wasiomudu kulipa kiasi hicho bado tuna Kitengo cha Ustawi wa Jamii ambacho hukaa nao na kufanya tathmini ya hali yao kama kweli hawawezi kulipa shilingi 100,000,” alisema Dk. Msemo.

Alisema kitengo hicho huchunguza hali ya maisha ya mgonjwa kubaini kama anamudu kulipa hata sh. 50,000 au hawezi.

“Uchangiaji ni suala la kisera. Hakuna mtu anayerejeshwa nyumbani bila kupata matibabu kwa sababu ameshindwa kuchangia. Kuna wengine tunawapa dawa ambazo ni ghali na anayelipia ni serikali,”alisema.

Dk. Msemo aliipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika taasisi hiyo, akisema katika nchi nyingine mambo kama hayo hayajafanyikia kiwango hicho.

“Mimi nimezunguka katika nchi nyingi za Afrika na hata katika nchi zilizoendelea. Inapofika katika suala la saratani ni jambo gumu. Kwetu tumejitahidi kulipa kwa kiwango kikubwa kutokana na rasilimali tulizonazo. Uwekezaji uliofanyika una umuhimu,” alieleza.

UNUNUZI WA DAWA

Dk. Msemo alisema serikali katika kila mwaka hutenga kati ya sh. bilioni saba hadi 10 kwa ununuzi wa dawa za saratani ambazo nyingi huzalishwa nje na zina gharama kubwa.

“Tunashukuru hivi sasa kuna mpango mkubwa wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wa kuanzisha viwanda vya dawa. Nadhani mpango huo utajumuisha pia uzalishaji wa dawa za saratani. Dawa hizi ni ghali na nyingi hutoka nje,”alisema.

Kwa upande wa teknolojia, alisema ORCI imepiga hatua kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini katika utoaji huduma za saratani kutokana na kuwepo mashine za kisasa.

Alisema miongoni mwa mashine hizo ni PET Scan yenye gharama ya zaidi ya sh. bilioni 18, CT Scan, MRI pamoja na mashine nyingine za kisasa za matibabu.

“Pengine katika Afrika Mashariki na hata Kusini mwa Afrika, ukiondoa Afrika Kusini, Tanzania ndiyo nchi yenye huduma za saratani zilizo katika kiwango cha juu. Kenya wana baadhi ya huduma hizo, nyingi ziko katika hospitali binafsi na mtu anaweza kusubiri hadi miezi tisa kupata matibabu ya mionzi,” alisema.

MASHINE MPYA

Dk. Msemo alisema awali mgonjwa ilimpasa kusubiri takribani wiki 10 kupata tiba ya mionzi, lakini kuanzia mwezi ujao muda huo utapungua hadi wiki mbili baada ya kuanza kufanya kazi mashine tatu mpya.

“Tunatarajia kuzindua mashine tatu mpya za mionzi mwishoni mwa mwezi huu, jambo litakalopunguza muda wa kusubiri matibabu.

“Hata katika baadhi ya nchi zilizoendelea siyo rahisi kupata tiba ya mionzi ndani ya wiki mbili, kwa sababu ni tiba ghali na inahitaji mambo mengi,” alisema.

HUDUM MPYA

Mkurugenzi mtendaji huyo alisema taasisi hiyo yenye historia ndefu ya utoaji huduma za saratani nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, wiki mbili zilizopita iliadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.

Kwa mujibu wa Dk. Msemo, katika kipindi cha miongo mitatu taasisi hiyo imeendelea kupanua huduma zake na hivi sasa inatoa karibu huduma zote muhimu zinazohitajika kwa wagonjwa wa saratani.

“Tunatoa karibu huduma zote za matibabu ya saratani. Huduma pekee ambayo hatukuwa tunatoa ni upasuaji wa saratani, kuanzia mwezi ujao tutaanza kuitoa,”alisema.

Alisema tayari wamekamilisha ujenzi wa chumba maalumu cha upasuaji na ununuzi wa vifaa vya kisasa vitakavyotumika katika huduma hiyo.

HUDUMA ZINAZOTOLEWA

Dk. Msemo alisema hivi sasa ORCI inatoa huduma za matibabu ya saratani ikiwemo tiba ya mionzi (radiotherapy), tiba ya kemikali (chemotherapy) pamoja na tiba za homoni kwa wagonjwa wa saratani.

Mbali na matibabu, Dk. Msemo alisema wana Kitengo cha Kudhibiti Saratani kinachojihusisha na uchunguzi wa awali kwa wananchi kugundua dalili za saratani mapema.

Alisema kupitia huduma za mkoba za Rais Dk. Samia, taasisi hiyo imefanikiwa kuwafikia zaidi ya Watanzania 200,000 vijijini katika kipindi cha miaka minne na nusu kwa kutoa elimu kuhusu saratani na kufanya uchunguzi wa awali bila malipo.

“Wanaogundulika wana viashiria vya saratani katika hatua za awali, hususan saratani ya shingo ya kizazi au matiti kwa kinamama, hupatiwa matibabu mapema.

“Wale ambao ugonjwa umeanza kuwa katika hatua za juu zaidi huletwa hapa (ORCI) kwa matibabu zaidi. Kwa hiyo tuna Kitengo cha Kudhibiti Saratani kinachofanya kazi hizo,” alisema.

MAFUNZO

Dk. Msema alisema taasisi hiyo ina jukumu la kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya katika eneo la saratani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Alisema hadi hivi sasa wamesomesha madaktari bingwa wasiopungua 80 wa saratani tangu kuanzishwa programu za mafunzo, tofauti na miaka ya nyuma ambapo wataalamu wengi walilazimika kwenda kusoma nje.

“Wakati mimi (Dk. Msemo) nasoma ilibidi niende nje ya nchi kupata elimu ya saratani. Hivi sasa tuna programu za mafunzo hapa nchini, ambapo tunasomesha madaktari bingwa, wauguzi pamoja na wataalamu wa teknolojia ya mionzi,” alisema.

Alisema wameanzisha programu maalumu ya kusomesha mafundi wa mitambo ya matibabu ya saratani katika eneo la ‘Medical Physics’ kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

CHANGAMOTO

Akizungumzia changamoto, Dk. Msemo alisema bado kuna tatizo la uelewa mdogo kwa baadhi ya wananchi kuhusu ugonjwa wa saratani.

Alibainisha baadhi ya watu wanaamini saratani husababishwa na mambo ya kishirikina, hali inayowafanya kuchelewa kwenda hospitali, badala yake hutafuta tiba kwa waganga wa kienyeji.

“Bado kuna changamoto ya uelewa katika jamii. Wapo wanaodhani saratani ni mambo ya kishirikina au wanaamini taarifa zisizo sahihi zinazozagaa mitandaoni,” alisema.

Alitoa mfano wa taarifa zilizokuwa zinasambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuchukua sampuli ya kinyama (biopsy) kunasababisha saratani kusambaa mwilini, akifafanua taarifa hizo siyo sahihi.

“Haiwezekani kumwambia mtu ana saratani bila kuchukua sampuli na kuipima maabara. ‘Biopsy’ ndiyo njia sahihi ya kuthibitisha aina ya saratani na kupanga matibabu,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia programu za uchunguzi na uhamasishaji kwa kuongeza uelewa kuhusu saratani na umuhimu wa kufanya uchunguzi mapema.

AINA ZA SARATANI

Akizungumzia aina za saratani zinazoongoza nchini, Dk. Msemo alisema kwa wanawake saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na saratani ya matiti.

Kwa upande wa wanaume, saratani ya tezi dume ndiyo inayoongoza huku saratani ya utumbo mpana nayo ikianza kuongezeka hata kwa watu wenye umri chini ya miaka 50.

Dk. Msemo aliwataka wananchi kuzingatia kinga kwa kuepuka tabia hatarishi kama vile uvutaji sigara, unywaji pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi.

“Tunasisitiza kinga kwa sababu baadhi ya saratani zinaweza kuzuilika kwa kubadilisha mtindo wa maisha. Pia tunahamasisha watu kufanya uchunguzi mapema kugundua ugonjwa katika hatua za mwanzo ambapo matibabu huwa rahisi zaidi,”alisema.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema serikali imepanua huduma za saratani katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa kituo kipya cha matibabu ya saratani mkoani Mbeya.

Pia, Dk. Msemo alisema Kigoma na Mtwara nako ujenzi unatarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha ujao, huku katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, jengo likiwa linatarajiwa kukamilika.

“Uwekezaji huu unaofanyika hivi sasa ni mkubwa. Kwa miaka 30 ya uwepo wa taasisi yetu, uwekezaji uliofanyika kipindi cha miaka minne na nusu iliyopita ni mkubwa kuliko uliokuwa umefanyika katika miaka 26 iliyopita,” alisema.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kusogeza huduma karibu na wananchi na ni uwekezaji ambao pengine miaka 10 iliyopita ilikuwa ni kama ndoto.

CHANJO

Dk. Msemo alisema serikali imeingiza chanjo ya kirusi cha ‘Human Papillomavirus (HPV)’ katika Mpango wa Taifa Chanjo kusaidia kudhibiti saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka tisa hadi 12 waliopo shuleni.

“Ndiyo maana tunahamasisha watu wafanye uchunguzi kwa sababu mabadiliko yanapoanza katika shingo ya kizazi ni rahisi kuyaona na unaweza ukamaliza hilo tatizo. Saratani inayotibika kwa asilimia 100 ni shingo ya kizazi.

“Pamoja kwamba, inaathiri kinamama wengi na hatari ya kupoteza maisha. Hii saratani nayo imepata mwarobaini, kuna chanjo yake.

“Kuna chanjo zimeshaingizwa katika utaratibu wa Mpango wa Chanjo wa Kitaifa. Kwa hiyo utakapoambiwa binti yako mwenye miaka tisa 12 anatakiwa apewe chanjo na hii kampeni imeendelea hadi shuleni,”alisema.

Dk. Msemo alisema binti atapewa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi, hivyo wasikatae kwa sababu hiyo ni njia mojawapo ya kudhibiti, kwani itadhibiti asilimia 70 hadi 80.

“Hivi sasa hizo asilimia chache ambazo zitakuwa zimebaki ukifanyiwa ‘screening’ mapema, utagundulika utatibiwa. Kuna baadhi ya saratani ambazo kwa kweli ushughulikiaji wake ni mwepesi. Ni watu kuwa na uelewa na kwa kufanya hivyo,”alisema.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, ORCI hutumia kati ya sh. bilioni 40 hadi 50 kila mwaka kwa uendeshaji wa shughuli zake ikiwemo kulipa mishahara ya wafanyakazi, kununua dawa na kutoa huduma za matibabu.

“Kwa nchi yenye uchumi kama wetu hizi siyo fedha ndogo. Serikali inaendelea kuwekeza kuhakikisha huduma za matibabu ya saratani zinaboreshwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” aliongeza.

Previous Post

CCM NDIYO BABA WA DEMOKRASIA – KIHONGOSI

Next Post

RAIS DK. SAMIA AMPA   ZAHIR ZORRO MILIONI 10/-

Next Post
RAIS DK. SAMIA AMPA   ZAHIR ZORRO MILIONI 10/-

RAIS DK. SAMIA AMPA   ZAHIR ZORRO MILIONI 10/-

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

DK. SAMIA AONGOZA KIKAO MAALUMU CHA KAMATI KUU YA CCM

DK. SAMIA AONGOZA KIKAO MAALUMU CHA KAMATI KUU YA CCM

5 months ago
TRENI ZA JIJI DAR, DODOMA ZANUKIA

TRENI ZA JIJI DAR, DODOMA ZANUKIA

5 months ago

Popular News

  • PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SERIKALI YAFUTA LESENI 40 ZA UTAFITI  WA MADINI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TIMU OFISI YA MAKAMU WA RAIS, WIZARA YA MAJI KUCHUANA MEI MOSI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SIMBA, FOUNTAIN GATE SIKU YA HESHIMA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AKAGUA MJI WA AFCON FUMBA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?