Na AMINA KASHEBA
RAIS DK. Samia Suluhu Hassan, amempatia sh. milioni 10 mwanamuziki nguli wa dansi, Zahir Ally Zorro na kumtakia pole kutokana na maradhi yanayomsumbua.
Mzee Zorro aliyewahi kung’ara na nyimbo mbalimbali zikiwemo Safari, Ripoti Za Mtaani (Fid Q), Cleopatra na Homa Ya Mapenzi (Ukonga Jazz Band), amepatiwa fedha hizo kama salamu za pole na faraja huku akimtakia kheri apone haraka.
Gwiji huyo alikabidhiwa fedha hizo na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma jana alipomtembelea nyumbani kwake, Kigamboni, Dar es Salaam, kumjulia hali na kufikisha salamu za Dk. Samia.
“Serikali inaendelea kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na wasanii wakongwe katika kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Tanzania.”alisema.
Mwnjuma alisema wasanii hao ni hazina muhimu ya taifa, hivyo wanastahili kuenziwa na kupewa faraja wakati wanapokumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya au kijamii.
Naye mkongwe Zorro alitoa shukrani kwa serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia kwa upendo na kujali hali yake ya kiafya.
“Msaada huu ni faraja kubwa kwangu na kwa familia yangu katika kipindi hiki ninachokipitia,” alisema.




