Na MWANDISHI WETU
BAADA ya kushinda mabao 7-1 dhidi ya Polisi Tanzania juzi, klabu ya Yanga imefichua siri kuwa, kuendelea kuimarika kwa kikosi chake ndiyo sababu ya kupata ushindi huo.
Yanga ilipata ushindi huo katika mchezo wa mtoano wa Kombe la FA uliopigwa Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Kutokana na ushindi huo, sasa miamba hiyo itachuana na TMA All Stars katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya kombe hilo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema amefurahia kiwango cha timu yao.
Kamwe aliweka wazi kuwa, asilimia kubwa ya wachezaji waliopewa nafasi ya kucheza katika mtanange huo, walicheza vyema.
“Mechi ilikuwa hatari baada ya dakika tano tulikosa mabao matatu hii inaonesha ni namna gani timu yetu imebadilika kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Kamwe alisema baada ya kumalizika mchezo huo, hivi sasa wanajipanga kwa mechi zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga keshokutwa itachuana na Mbeya City katika mtanange wake wa 13 wa Ligi Kuu.
Naye beki wa Yanga, Ibrahim Hamad Bacca, aliwapongeza wachezaji wenzake kwa kuonyesha kiwango kizuri katika mtanange huo.
“Nimefurahi tumeshinda mabao mengi, kwangu nimejisikia fahari kuwaongoza wenzangu na tumeshirikiana vizuri na kupambana hadi tumepata ushindi,” alisema.




