Na NASRA KITANA
WAKATI timu za Simba na Yanga zikiondoka nchini jana, viongozi wa timu hizo wameweka wazi kuwa akili zao zote ni katika mechi za kimataifa ili waweze kupata ushindi na kurudi na pointi tatu muhimu.
Yanga imeondoka kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wake wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), dhidi ya Wiliete ya nchini humo, mchezo utakaochezwa Septemba 19, mwaka huu Uwanja wa 11 de Novembro.
Hata hivyo, Simba pia wameondoka kwenda Botswana kwa mchezo wa CAFCL dhidi ya Gaborone United utakaopigwa Septemba 20, katika Uwanja wa Obed Itani Chilume.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa klabu ya Simba na Yanga walisema kuwa akili zote kwa hivi sasa wameziamishia katika mechi za kimataifa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa wametoka kupoteza dhidi ya Yanga lakini ana imani kubwa na kikosi chao kinaenda kufanya vizuri na kufika mbali katika michuano ya kimataifa.
Alisema kuwa anajua mchezo utakuwa mgumu na wenye changamoto nyingi lakini watapambana kuhakikisha hawapotezi.
“Tumeelekea nchini Botswana kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Goborone United, hautakuwa mchezo rahisi kwetu lakini tutapambana kwa kila namna ili tuweze kupata matokeo,” alisema Ahmed.
Ahmed alisema kuwa matokeo ambayo wameyapata dhidi ya Yanga wameachana nayo na hivi sasa akili na mawazo yao yote ni kuelekea katika mchezo wa kimataifa.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanakwenda kupata ushindi japokuwa na kurejea nyumbani na pointi tatu.
Kamwe alisema kuwa anajua hautakuwa mchezo mwepesi kwao lakini hawatakubali kupoteza kwani lengo lao ni kuona wanashinda katika kila mchezo watakaocheza.
“Tumetoka kupata ushindi dhidi ya Simba hii ni kubwa kwetu na ni mwanzo mzuri kuelekea katika mechi yetu ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikubwa tunahitaji ushindi ambao ni muhimu,” alisema Kamwe.
Ofisa Habari huyo aliwataka mashabiki na wapenzi wa timu yao kutokuwa na hofu kwani wanakwenda kupambana kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Katika hatua nyingine, Singida Black Stars nayo iliondoka nchini jana kwenda Rwanda katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (CAFCC), dhidi ya Rayon Sports huku Azam FC ikiwa nchini Sudan Kusini kuivaa Al Merreikh katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya michuano hiyo mechi zote zikichezwa Septemba 20, mwaka huu.