Na WAANDISHI WETU, Dodoma
ZIKIWA zimepita siku nane (Sawa na saa 192), tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan awaapishe mawaziri na naibu mawaziri, wametaja vipaumbele vyao katika utekelezaji wa majukumu yao vyenye dhamira ya kuwatumikia wananchi.
Baadhi ya mawaziri baada ya kukabidhiwa vijiti vya kuongoza wizara zao, wameeleza walivyojipanga kutimiza ahadi zilizotolewa na Rais Dk. Samia, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025 – 2030.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao walitoa wito kwa watendaji wa wizara zao, kujifunga mkanda tayari kuanza mchakamchaka wa kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na Naibu Waziri, Wanu Hafidh Ameir, walisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini.
Profesa Mkenda, alieleza kuwa, wizara imejipanga kuhakikisha elimu inayotolewa, inawawezesha vijana kupata maarifa, stadi stahiki na ujuzi ili waweze kujiajiri na kushindana katika soko la ajira.
Profesa Mkenda, aliongeza wizara itasimamia kikamilifu elimu katika ngazi mbalimbali na kuweka mkazo mafunzo ya amali.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Wanu, aliahidi ushirikiano kufanikisha mageuzi, huku akihimiza kuendeleza utamaduni wa ushirikiano na weledi katika kazi, kuhakikisha malengo ya serikali ya kutoa elimu bora kwa wote, yanafanikiwa.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, aliwataka watumishi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, kuzingatia maslahi na utu wa Mtanzania wanapotoa huduma kwa wananchi.
Alisema ni muhimu watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia utu na maslahi ya wananchi kwa kutoa huduma bora.
“Wananchi wanatuhitaji kwa yale tuliyoaminiwa kuyatekeleza kwa niaba ya Watanzania milioni 61. Ni jukumu letu kuwawezesha waendelee kuishi vizuri kama kawaida,” alisema Dk. Kijaji.
Alifafanua kuwa, Ilani ya CCM, imeweka mkazo katika ustawi wa watu na huo hauwezi kupatikana endapo changamoto, wakiwemo wanyamapori waharibifu, hazitatatuliwa.
“Mkulima amelima ekari 20 za mbaazi, zimekomaa, halafu zinaharibiwa na tembo, ustawi haupo hapo. Hivyo, lazima tufikirie mbali kulinda ustawi wao,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa, falsafa ya Kazi na Utu ya Rais Dk. Samia inahitaji mtumishi kumweka mwananchi mbele.
WAZIRI WA AFYA
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, aliwataka watendaji wa wizara hiyo, kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema huu ni wakati wa watumishi kuongeza juhudi na kutobweteka, kuendelea kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya afya.
“Nawasisitiza watumishi wote, kuacha kufanya kazi kwa mazoea, tubadilike na kutekeleza majukumu kwa ufanisi, kuhakikisha taifa letu linasonga mbele katika sekta ya afya,” alisema.
WAZIRI WA NISHATI
Naye Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, aliwaagiza watumishi wa wizara hiyo, kufanya kazi kwa bidii, kutimiza vipaumbele vya serikali katika sekta ya nishati, ikiwemo kufikia megawati 8,000, ifikapo mwaka 2030.
Alisema watumishi wa Wizara ya Nishati, ndiyo watendaji wakuu wenye dhamana ya kuhakikisha malengo ya serikali yaliyowekwa, yanatimia kwa kufanya kazi kwa bidii.
WAZIRI DK. GWAJIMA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, aliwataka watumishi wa wizara hiyo, kuongeza bidii na kasi zaidi katika kutimiza wajibu wao kuharakisha maendeleo ya jamii.
Dk. Gwajima, alisema katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita, kilitumika kuijenga wizara mpya kwa kuanzisha mifumo ya uendeshaji, uwajibikaji, kutunga sera mbalimbali, mikakati, miongozo ya kisera na programu kadhaa za utekelezaji na kuitambulisha wizara katika jamii na wadau wa maendeleo.
Aliongeza katika kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita, kitajikita kujenga ushirikiano na mshikamano wa wadau wote, kuelimisha jamii kuhusu uwepo wa fursa mbalimbali za kiuchumi na kuwasaidia kuzifikia.
“Mheshimwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuniamini na kuniteua tena kuongoza wizara hii.
“Imani hii na heshima hii ni yenu pia, kwa kuwa, mlinipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu.
“Hivyo, basi nawaomba tena, tuendelee kufanya kazi kwa spidi zaidi, ari na ufanisi kutimiza azma ya serikali,” alisema Dk. Gwajima.
WAZIRI SIMBACHAWENE
Kwa upande wake, baada ya kukabidhiwa ofisi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alitoa wito kwa watumishi wa wizara hiyo, kufanya kazi kwa ushirikiano.
“Siamini katika sifa ya mtu mmoja, naamini katika uongozi wa kimfumo unaoheshimu utaratibu uliopo ili jambo likiwa zuri, liwe ni letu sote, kwa hiyo ni wajibu kushirikiana na kukumbushana,” alisema Simbachawene.
WAZIRI AWESO
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliwaagiza watendaji wa wizara hiyo, kuhakikisha wanashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kukomesha wizi wa mita za maji ambao unawagharimu wateja.
“Kuna mambo ambayo yapo katika wizara lakini hayazungumzwi sana, ukiwemo wizi wa maji, mita za maji na uharibifu wa miundombinu ya maji.
“Mamlaka nyingi sasa hivi, tumeshuhudia na kuona mwananchi anafungiwa mita yake ya maji kesho haipo, niombe mamlaka za maji zishirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha tabia hii inakoma.
Alisisitiza: “Haiwezekani mwananchi amelipa fedha yake anafungiwa mita yake apate huduma kijana nani anapita anachukua mita sijui wanakwenda kufanyia shughuli gani, wizi umekuwa mkubwa halafu bado anatakiwa kulipa mita huyohuyo mwananchi haiwezekani.”
Pia, waziri huyo, aliagiza wananchi wanaokamilisha utaratibu wa kuunganishiwa maji, kazi hiyo kufanyika ndani ya siku saba, badala ya kuzungushwa na baadhi ya watumishi.
“Haipendezi kuona mwananchi anaomba kuunganishiwa maji miezi sita hadi saba, akitoa rushwa, anaunganishiwa kesho hapana, hii ni taasisi ya serikali tusimamie misingi ili watu wapate maji kwa usawa bila usumbufu.
“Wapo baadhi ya watumishi wachache wanachafua taswira ya taasisi yenu, leo mtu anaomba kuunganishiwa maji anataka
rushwa, mnajidhalilisha, kufifisha heshima ya taasisi, acheni tabia hiyo waunganishieni watu maji ndani ya siku saba,” alisema Aweso.




