Na AMINA KASHEBA
KIKOSI cha Yanga kimeondoka nchini jana kwenda Algeria kuifuata kibabe JS Kabylie, katika mchezo wake wa pili wa makundi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFC).
Yanga itashuka dimbani Ijumaa kupambana na JS Kabylie, katika mchezo wa pili wa CAFCL, hatua ya makundi.
Katika mchezo huo Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda bao 1-0 dhidi ya As Far Rabat ya Morocco huku JS Kabylie ikiwa imetoka kupoteza mabao 4-1 mbele ya Al Ahly.
Akizungumza kabla ya kuondoka nchini Meneja wa Yanga, Walter Harrison alisema katika safari yao watapitia Dubai na watafika Algeria kesho wataanza mazoezi kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.
“Tutafika Algeria Jumatano, hivyo tutafanya mazoezi kwa siku hizo kabla ya kikosi kushuka dimbani kupambana katika mchezo mwingine wa hatua ya makundi,” alisema.
Meneja huyo aliwaomba mashabiki wa Yanga kuwaombea dua ili wafanye vyema katika mchezo huo na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele hatua ya robo fainali ya CAFCL msimu huu.
“Mashabiki wanapaswa kuwa na imani na timu yao kwani tangu droo iipopangwa tulikuwa tunafanya machakato wa kuhakikisha tunafanya vizuri, wanapaswa kuamini benchi lao la ufundi.
“Tuna imani tutafanya vizuri katika kurusha karata yetu ya pili ambao ni muhimu wa michuano hii kuhakikisha tunajiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele,” alisema.
Meneja huyo alisema wanashukuru Mungu mchezo wao wa wiki iliyopita ulimalizika salama na hawakupata mchezaji yoyote mwenye majeraha.
“Hakuna majeruhi yoyote jambo ambalo tunashukuru, unapokuwa na majeruhi huwa inaleta changamoto kwa benchi la ufundi kuanza kuandaa mchezaji mwingine,” alisema.




