Na ABDUL DUNIA
WAKATI mechi za pili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) zikichezwa wiki hii, Yanga itakuwa na kibarua kizito kuhakikisha inavunja rekodi ya ushindi ya JS Kabylie katika dimba lake la nyumbani.
Yanga itachuana na JS Kabylie ya Algeria katika mechi ya kundi B itakayochezwa Ijumaa hii katika Uwanja wa Hocine Aït Ahmed, Tizi Ouzou nchini Algeria.
Katika mtanange huo wa aina yake, Yanga inayonolewa na Kocha Pedro Goncalves inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote kuendelea kukaa katika nafasi nzuri katika kundi hilo.
Hata hivyo, miamba hiyo kutoka mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo jijini Dar es Salaam, itakutana na kibarua kizito kuhakikisha inamaliza mechi bila ya kupoteza dhidi ya timu hiyo kutoka Algeria.
JS Kabylie katika dimba lake la nyumbani hadi sasa msimu huu, ina rekodi ya ushindi wa asilimia 100, ikishinda mechi mbili kati ya mbili ilizocheza katika hatua ya kwanza na ya pili za mtoano.
Katika hatua hizo za awali, JS Kabylie ilifunga jumla ya mabao saba na kuruhusu bao moja pekee katika uwanja wake wa nyumbani.
Ikiwa nyumbani, miamba hiyo ya Algeria ilipata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Bibiani Gold Stars ya Ghana katika hatua ya kwanza na ushindi wa 2-1 ilipochuana na US Monastir ya Tunisia katika hatua ya pili.
Hata hivyo, Yanga nayo itaingia katika mtanange huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 ugenini iliyoupata dhidi ya Wiliete ya Angola katika hatua ya kwanza na kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers ya Malawi katika hatua ya pili ya mtoano.
Katika kundi B, Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu sawa na kinara Al Ahly zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, AS FAR Rabat ya Morocco inafuatia bila ya pointi sawa na JS Kabylie. Katika mtanange wa kwanza, Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya AS FAR wakati JS Kabylie ikifungwa mabao 4-1 ilipocheza na Al Ahly.




