Na MUSSA YUSUPH
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa sababu zitakazomwezesha mgombea huyo kupata ushindi wa kishindo.
Dk. Migiro alieleza hayo, alipozungumza katika mkutano wa kampeni wa CCM, uliofanyika Uwanja wa Hamburu, Jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambao Mgombea urais kupitia CCM, Dk. Samia alihutubia maelfu ya wananchi.
Alisisitiza mafanikio ya filamu hiyo, yameongeza thamani ya utalii, kuimarisha uchumi na kuonesha wazi dira ya maendeleo ya viongozi hao.
“Katika kazi nyingi walizofanya, hatuwezi kusahau mchango mkubwa wa Rais Dk. Samia katika kuandaa filamu ya Tanzania The Royal Tour. Ilikuwa kielelezo cha kuipeleka Tanzania kiuchumi na leo tumeona matokeo yake,” alisema Dk. Migiro.
Aliongeza Zanzibar imenufaika zaidi kupitia filamu hiyo, kwani ni kisiwa chenye utajiri wa viungo, manukato na vivutio vya kipekee vinavyoongeza mvuto wa kitalii duniani.
“Ulipokuwa waziri wakati wa Rais Karume, ulitangaza vema Zanzibar na sasa uzoefu huo umetumika katika Royal Tour. Mwinyi ameendeleza misingi hiyo na utalii leo ni injini ya uchumi wa kisasa,” alisema.
Aliongeza wagombea wa CCM, Dk. Samia na Mwinyi wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu’, ambapo wameweka msisitizo kupitia uwekezaji wa rasilimali watu, elimu, afya na maji.
“Dk. Samia ameonesha kwa dhati anataka kuitimiza kaulimbiu ya Kazi na Utu. Tumeona jitihada katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, elimu, maji na afya. Haya ni mafanikio yasiyopingika,” alisema.
Dk. Migiro alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kuimarisha miundombinu, akitolea mfano ujenzi wa barabara na miradi mbalimbali.
Alisema wananchi wameanza kumuita ‘Hussein Mabati’ kutokana na mabati mengi yanayozungushiwa katika maeneo ambayo miradi ya maendeleo inatekelezwa.
“Ujenzi wa kisasa unaendelea. Zanzibar inaelekea kuwa na uchumi wa kisasa. Tuna kila sababu ya kuwaunga mkono wagombea hawa,” alisisitiza.