Na MUSSA YUSUPH,
Pemba
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kutikisa kisiwani Pemba kwa kufanya mkutano mkubwa wa kampeni katika viwanja vya Gombani ya Kale.
Mkutano huo, utakaofanyika Septemba 20, 2025, maelfu ya wakazi wa kisiwa hicho, watapata fursa kusikiliza ahadi mbalimbali zitakazotolewa na mgombea huyo wa Urais.
Tayari mitaa mbalimbali ya Pemba, imepambwa kwa bendera za CCM huku mabango yenye picha za Dk. Samia zikipendezesha maeneo mbalimbali zikiwemo barabara mashuhuri kisiwani hapa.
Wakizungumza kuhusu mkutano huo baadhi ya wananchi wameeleza matarajio yao kwa Dk. Samia ambapo mfanyabiashara wa Chakechake, Ali Masoud Mzee, alisema anatarajia Dk. Samia atatoa msisitizo zaidi kukifungua kisiwa hicho kiuchumi.
“Pemba kwa sasa imeanza kufunguka, lakini kwetu wafanyabiashara tunaamini fursa zaidi zikifunguka ndipo mzunguko wa fedha utaongezeka,” alieleza.
Naye, Kombo Issa Kombo, alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika kisiwa hicho.
“Amani imetawala siyo kama kipindi cha zamani wakati wa uchaguzi hali inachafuka, lakini sasa kampeni zinafanyika kwa ustaarabu na ulinzi umeimarishwa,” alisisitiza.
Pemba ni miongoni mwa maeneo yaliyonufaika kupitia miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha maisha na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Miongoni mwa miradi hiyo ni kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyozinduliwa kisiwani hapa Mei tano mwaka huu na kuwanufaisha wananchi kwa kupata huduma za kisheria.
Vilevile, kisiwa hicho kimenufaika kupitia mradi wa hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambao unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT).
Wilaya za Pemba zilizonufaika kupitia mradi huo ni Wete na Micheweni ambao umejikita kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula kwa gharama ya sh. bilioni 1.2.
Kadhalika, kisiwa hicho kinaendelea kunufaika na fedha zitolewazo na wadau wa maendeleo kupitia SJMT ambapo baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya Chakechake hadi Wete kupitia kwa Binti Abeid na ujenzi wa shule, hospitali na masoko.
Pia, Serikali ya Dk. Samia kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutekeleza mradi wa kuboresha mawasiliano katika baadhi ya vijiji. Miongoni mwa vijiji vilivyonufaika ni Kojani, Kinyikani, Kidundo na Wete mjini vilivyopo Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kwa upande wa nishati, serikali ipo katika mpango wa kuimarisha njia zinazosafirisha umeme kwa njia ya bahari kwa lengo la kuongeza kiwango cha upatikanaji nishati hiyo Unguja na Pemba.
Kazi hiyo inafanywa kwa ushirikiano baina ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ambapo njia ya umeme inayotoka Tanga hadi eneo la Wesha kisiwani Pemba itaimarishwa.
Juzi, Dk. Samia alihitimisha mikutano yake ya kampeni mjini Unguja kwa kuhutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika uwanja wa Hamburu, Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika mkutano huo, Dk. Samia alisema Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ndiye mgombea sahihi atakayeshirikiana naye kuleta maendeleo kwa manufaa ya pande mbili za muungano.
Alisisitiza kuwa matokea ya ukuaji uchumi na utekelezaji ahadi za CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, umeonekana dhahiri uwezo wa kiongozi huyo katika kuwaongoza Wazanzibar.
“Pamoja na majanga yote tuliyopitia ikiwemo Covid, tumeweza kufanyakazi kubwa pamoja katika sera za kifedha na uchumi na ndiyo maana hatukuweza kukwamisha miradi yetu.
“Kwenye sera za kifedha na sera za kiuchumi, Dk. Hussein ameweza kusimamia na kuimarisha uchumi ambao kwa sasa unakuwa kwa kasi kubwa,” alisisitiza.
Rais Dk. Samia alibainisha kuwa ukuaji uchumi kwa Tanzania bara umeongezeka kwa asilimia sita huku Zanzibar ukiwa juu zaidi kwa asilimia 7.1 kwa mwaka.
“Zaidi uchumi umekuwa hata mifukoni kwa kila mwananchi. Wakati nilipokuwa nikiwasili Nungwi nilikuwa nikitazama kila pande na kujionea namna ambavyo kumejengeka nyumba nzuri za makazi, biashara zinafanyika na mambo yanaenda vyema kwa amani na utulivu,” alisisitiza.